*NSSF kuanzisha miradi mikubwa jijini
*Mizigo bandarini kuondolewa kwa treni tano
*Mwisho wa malori kuingia jijini wawadia
*Nyumba zote Manzese, Vingungu kuvunjwa
Sura ya Jiji la Dar es Salaam itabadilishwa na kugeuka jiji la kisasa ndani ya miaka minne ijayo kutokana na mpango mzito ulioandaliwa na Mfuko wa Hifadhi za Jamii (NSSF).
Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, ameliambia Jamhuri mjini Zanzibar mwishoni mwa wiki kuwa Mfuko huo umenunua ekari 1,000 za ardhi huko Kisarawe ambazo watajenga Bandari Kavu. Kutokana na hatua hiyo, mizigo yote bandarini itatolewa moja kwa moja kutoka melini na kupelekwa Kisarawe.
Dk. Dau anasema katika kusafirisha mizigo hiyo watatumia treni tano zenye behewa 20 kila moja, kwa maana ya behewa 100, na hivyo mizigo itatolewa kwa kasi bandarini kuliko wakati wowote katika historia ya nchi hii.
“Nisingependa kuwa msemaji wa bandari, lakini najua kwa sababu nimefanya kazi pale, bandari ya Dar es imepitwa na wakati. Bandari ya Dar es Salaam ipo kwenye daraja la pili, Mombasa wameboresha wapo daraja la tatu, lakini bandari nyingine duniani zipo kwenye 7th generation (daraja la saba).
“Bandari makini inapaswa kuwa sehemu ya uzalishaji mali. Inapaswa kuwa imezungukwa na viwanda vidogo vidogo. Dubai bandari yao imezungukwa na viwanda vya kutengeneza washing machines, tv na vitu vingine ambavyo baada ya kutengenezwa tu vinasafirishwa,” amesema Dk. Dau.
Ameliambia Jamhuri kuwa chini ya mpango ulioandaliwa na NSSF, meli ikiingia bandarini inapakua mzigo na kuweka kwenye treni na mzigo huo unasafirishwa moja kwa moja kwenda Kisarawe. Kufanikisha mpango huu NSSF watajenga hoteli, vituo vya mafuta na maduka huko Kisarawe ambapo malori karibu 3,000 yanayokwenda bandarini sasa yote hayataingia jijini Dar es Salaam.
“Hii itapunguza msongamano kwa kiwango kikubwa. Clearance ya mizigo yote haitafanyika tena hapa bandarini, bali itafanyika huko Kisarawe,” anasema Dk. Dau.
Anasema mbali na kwamba NSSF watapata fedha kutokana na mradi huu, anaamini kuwa Mfuko utakuwa umetimiza jukumu la msingi la huduma kwa jamii ambayo inapaswa kupunguziwa matatizo kwa njia kama hizo. Mradi huu unaanza mwaka huu wa fedha. Dk. Dau hakutaja kiasi kitakachotumika kugharamia mradi huu kwa maelezo kuwa bado wataalam wanaendelea na uchambuzi wa gharama.
NSSF kuboresha makazi
Mkurugenzi wa Miradi wa NSSF, Yacoub Kidula, aliwambia wahariri mjini hapa kuwa Mfuko unaanzisha mradi wa kujenga nyumba za kisasa katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam ambapo nyumba zilizojengwa bila mpangilio zitavunjwa na kujenga nyumba zenye viwango.
Utaratibu ulioandaliwa na NSSF chini ya mradi huu ni wa kujenga nyumba za dharura kwa watu wote watakaohamishwa katika makazi yao na kuwaweka katika nyumba hizo, kisha kutumia miezi 24 kujenga nyumba katika eneo walipohamishwa wakazi hawa na baada ya hapo wanarudishwa kwenye nyumba zao.
Kutakuwapo utaratibu wa kuwalipa fidia wenye nyumba wakati wa kuwahamisha, lakini baada ya ujenzi kukamilika waliokuwa wamiliki wa nyumba zilizovunjwa watapewa fursa ya kununua nyumba mpya zilizojengwa kwa bei nusu ya gharama. Nyumba za ziada zinazojengwa katika maeneo hayo zitauzwa kwa bei ya soko na hivyo kufidia gharama zilizotumika.
Katika Jiji la Dar es Salaam, Wilaya ya Temeke nyumba zitakazovunjwa na kujengwa upya chini ya utaratibu huu ni zile zilizopo katika maeneo ya Mtongani, Kichangani, Keko, Chang’ombe na Mbagala.
Kwa Wilaya ya Kinondoni, mradi huu utaanza kwa kuvunja na kujenga nyumba za Magomeni, Kigogo Mbuyuni, Mkwajuni, Mwananyamala, Mburahati, Manzese, Msasani, Kinondoni Shamba na Mwenge.
Mradi huu mkubwa kwa Manispaa ya Ilala nyumba zitakazovunjwa na kujengwa upya ni za Mchikichini (mradi umeishaanza), Vingunguti, Buguruni na Gongolamboto.
Hospitali ya Apollo yaja Dar
Dk. Dau ameliambia Jamhuri kuwa kufikia Februari mwakani, wagonjwa waliokuwa wanapelekwa India kwa uchunguzi wa afya wataweza kupata huduma hiyo hapa nchini.
Amesema kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa Muhimbili, tayari wameingia mkataba na Hospitali ya Apollo ya India, ambayo itafunga mitambo ya kisasa ya kuchunguza afya na kufanya matibabu ya msingi katika Jengo la NSSF Bibi Titi, Dar es Salaam.
“Katika jengo letu hili wamechukua ghorofa tatu za chini na wanafunga vifaa vipya kabisa. Vifaa hivi vitatumiwa kufanya uchunguzi wa afya kuanzia kichwani hadi kwenye kisigino. Hatutakuwa na sababu tena ya kumpeleka mtu India kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa afya isipokuwa kwa magonjwa yaliyoshindikana tu,” amesema.
Ameongeza kuwa Apollo wamesisitizwa kuwa gharama ya matibabu isiwe kubwa. Kwa mfano yeye aliwahi kupima kipimo cha mwili mzima kinachogharimu dola 200 (Sh 360,000) huko India, hivyo akasema kila mtu anastahili kupata huduma hii kwa gharama nafuu.
Kwa miradi hii iliyotajwa ikikamilika Jiji la Dar es Salaam litabadilika sura na kuwa la kisasa sawa na majiji mengi duniani ya nchi zilizoendelea.