Watu wengi wamekuwa na tabia ya kupuuzia baadhi ya dalili ndogo zinazojitokeza
kwenye afya zao pasipo kujua chanzo hasa cha dalili hizo. Ifahamike kuwa tabia
hii ni hatari sana kwa sababu matatizo yote makubwa ya kiafya huwa yanaanza
na dalili ndogo ndogo ambazo wengi wamekuwa wakizidharau.
Nitakueleza baadhi ya dalili zinazojitokeza kwenye afya zetu, japo zinaonekana ni
ndogo, lakini hupaswi kuzifumbia macho kwa sababu zinaashiria tatizo fulani
kwenye mwenendo wa afya kwa ujumla.
Dalili ya kwanza ni udhaifu wa kwenye miguu na mikono kunakoambatana na
ganzi. Ikiwa sehemu za mikono na miguu zinadhoofika, zinakosa nguvu na kupata
ganzi na hasa dalili hizi zikitokea hadi usoni, inaweza kuwa ni dalili ya kiharusi na
hasa kama hali hii inatokea upande mmoja tu wa mwili.
Sambamba na dalili hizi, kiharusi pia huambatana na dalili kama vile unakosa
balansi wakati wa kutembea, unapata kizunguzungu, na kushindwa kutembea
vizuri.
Nikukumbushe tu msomaji, kiharusi ni ugonjwa unaosababishwa na matatizo ya
usambazwaji wa damu kwenye ubongo kutokana na kuziba au kupasuka kwa
mirija inayosambaza damu kwenye ubongo na kusababisha chembechembe za
damu kufa.
Kiharusi kwa kitaalamu kinaitwa ‘stroke’ na ni maarufu sana kwa jina hili. Kiharusi
ni moja ya magonjwa yanayoongoza kusababisha vifo vya ghafla kwa miaka ya
hivi karibuni.
Hivyo, pata msaada wa kitabibu haraka sana ikitokea unapatwa na dalili hizi
pamoja na dalili nyingine kama kutoona vizuri, maumivu makali ya kichwa, kuhisi
kuchanganyikiwa au kupata shida katika kuongea.
Lakini dalili nyingine ni mkojo unaoambatana na damu. Yapo matatizo mengi
ambayo yamezoeleka yanayoweza kusababisha kutoa mkojo uliochanganyika na
damu, kama vile mambukizi ya kwenye njia za mkojo na hata maambukizi ya
baadhi ya magonjwa ya zinaa ikiwa yamedumu kwa muda krefu bila tiba.
Lakini pia ikiwa unatoa mkojo uliochanganyika na damu, na hasa ukiambatana na
maumivu ya mgongo au hata maumivu ya chini ya kitovu, hii ni ishara tosha kuwa
unashambuliwa na baadhi ya maradhi ya figo na hasa uwepo wa mawe madogo
madogo kwenye figo ambao kitaalamu tunaita ‘kidney stones’.

Tatizo hili hutokea wakati ambapo aina hii mawe yanajitengeneza na kujikusanya
kwenye figo baada mkojo kuchujwa na yale mabaki ya mkojo kutengeneza mawe
haya yatokanayo na ile chumvi chumvi.
Mawe haya hulazimika kutoka kupitia njia ile ile inayotumika na mkojo kutoka
kwenye figo ndani hadi kwenye njia ya mkojo ya nje iliyoambatana na via vya
uzazi. Hivyo kupitia mchakato huu, wakati mwingine mawe haya huchubua njia ya
mkojo wakati yakiwa yanalazimika kutoka nje na kusababisha majeraha madogo
madogo kwenye njia ya mkojo na kutokwa na damu.
Ni vyema kumuona daktari ili kuangalia uwepo wa aina hii ya mawe kwenye
figo. Lakini tatizo jingine kubwa, mkojo uliochanganyika na damu mara nyingi
huashiria saratani ya kibofu na hasa ikitokea hauambatani na maumivu yoyote.
Hivyo ni vyema kuwahi kupata vipimo ili kuliwahi tatizo hili katika hatua zake za
awali.