* Wizara yapeleka vijana 20 China, Brazil kusomea uzamili kuhusu mafuta, gesi
* Katibu Mkuu awaasa makubwa, asema nchi inawategemea warudi kuisaidia
Dalili njema zimeanza kuonekana katika Wizara ya Nishati na Madini Tanzania, baada ya vijana 20 wazawa kuchaguliwa kwenda China na Brazil kusomea shahada ya uzamili (masters) kuhusu fani za mafuta na gesi.
Hatua hiyo imefikiwa baada ya Tanzania kuziomba China na Brazil zikakubali kuipatia msaada wa kugharamia masomo hayo kwa vijana hao. Vijana 10 kutoka mikoa mbalimbali watakwenda China na wengine 10 watakwenda Brazil.
Kwa upande mwingine, hatua hiyo ni utekelezaji wa ahadi iliyotolewa na Serikali ya kuhakikisha inawasomesha wazawa kuhusu fani za mafuta na gesi, kwani hadi sasa Tanzania inahitaji wataalamu zaidi wa aina hiyo.
Lengo la jitihada hizo za Serikali ni kuwapata wataalamu wa kutosha watakaosimamia shughuli za utafiti, uchimbaji na usimamiaji mavuno ya nishati za mafuta na gesi hapa nchini.
Wanaokwenda China
Tayari Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini imekamilisha maandalizi ya kuwasafirisha vijana wanane wanaoondoka hapa nchini leo kwenda masomoni China kwa muda wa miaka miwili.
Hafla ya kuwaaga vijana hao ambao wote ni wahitimu wa shahada ya kwanza katika vyuo mbalimbali hapa nchini, iliongozwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliakim Maswi, katika ofisi za wizara hiyo Dar es Salaam, Ijumaa iliyopita.
Wanafunzi watakaonufaika na ufadhili wa kwenda masomoni China na vyuo vyao vikiwa katika mabano ni Yazidi Iddi, Paul Nsulangi, Grace Mkongwa, Maggi Mtaki, Januarius Matata (China University of Geosciences-Wuhan), Tekla Mponda (Wuhan University of Technology) na Cosmas Gamba (China University of Petroleum).
“China imekubali kugharamia kila kitu kwa vijana hawa kwa muda wa miaka miwili watakayokuwa masomoni, sisi kama Serikali kupitia Wizara ya Nishati na Madini tumewalipia nauli na kuwapa fedha za kujikimu huko wakati wakisubiri Serikali ya China ianze kuwalipa posho zao,” amesema Maswi.
Kwa mujibu wa Katibu Mkuu huyo, vijana hao wanakwenda kusoma fani za utafiti, uvunaji na usimamiaji wa madini, petroli, gesi na usimamiaji sheria ya mazingira na rasilimali. Wamechaguliwa katika kundi la watu 56 walioomba nafasi hiyo kupitia Wizara ya Nishati na Madini.
Wanaokwenda Brazil
Maswi amewataja vijana wengine 15 walioingia fainali ya ushindani wa kuchaguliwa kwenda kwenye masomo ya fani za mafuta na gesi nchini Brazil kuwa ni Nusura Adam, Sarah Mbwilo, Christina Magambo, Jacqueline Mackanja na Ernest Mulaya.
Wengine ni Makoye Didas, Wilson Ngole, Joseph Mathayo, Seleman Shemlugu, Nasibu Shonza, Revocastus Mafungu, Joseph John, Fortunatus Kidayi, Katabaro Daudi na Zahoro Athuman.
Maswi amefafanua kuwa vijana hao ni miongoni mwa watu 86 walioomba nafasi hiyo na kwamba mchujo wa mwisho utafanyika ili kuwapata vijana 10 watakaokwenda masomoni nchini Brazil.
Hata hivyo, amesema Ubalozi wa Brazil hapa Tanzania umeagiza kuwa vijana 10 watakaochaguliwa watalazimika kufundishwa lugha ya Kireno kwa muda wa miezi sita katika ubalozi huo kabla ya kuondoka hapa nchini.
“Ubalozi wa Brazil hapa nchini umesema itabidi kwanza vijana hao wafundishwe Kireno kwa miezi sita kwa sababu vyuo vya kule [Brazil] vinafundisha masomo kwa kutumia Kireno,” amesisitiza.
Maswi awaasa
Akizungumza katika hafla ya kuwaaga vijana wanaokwenda masomoni nchini China, Maswi aliwataka kuhakikisha wanakuwa mabalozi wazuri wa Tanzania katika Taifa hilo.
“Nendeni mkasome kwa bidii ili mrudi kuchangia ipasavyo kufanikisha mpango huu wa maendeleo ya Taifa. Tunahitaji wataalamu zaidi katika fani za mafuta na gesi.
“Mhakikishe mnakuwa waadilifu na kuzingatia masomo. Tumieni nafasi hiyo vizuri ili tupate wataalamu wa kusimamia sekta za nishati na madini.
“Wizara hii [Nishati na Madini] ni yenu, mkiwa na shida msisite kuwasiliana nasi. Ili muwe mabalozi wazuri lazima tuwe karibu na ninyi,” amesema Maswi.
Akijibu swali lililoulizwa na JAMHURI kutaka kujua ukubwa wa tatizo la upungufu wa wataalamu wa sekta hiyo hapa nchini, Maswi amesema; “Tunahitaji wataalamu wengi katika fani za mafuta na gesi, si chini ya wataalamu 200, hawa [vijana 20] wanaokwenda kusoma ni tone tu.”
Maswi ameongeza kuwa Tanzania inahitaji pia wataalamu wa masuala ya uchumi wa mafuta, gesi na wahasibu wa sekta hiyo.
“Mwaka jana tulipeleka Watanzania wawili kusomea sheria ya mafuta na gesi, mwaka huu pia tumepeleka wawili kusomea sheria hiyo nchini Uingereza,” amesema.
Changamoto wizarani
Katibu Mkuu huyo wa Wizara ya Nishati na Madini ametaja changamoto kuu katika wizara hiyo kuwa ni kuwezesha upatikanaji wa umeme wa uhakika na kuendeleza sekta ndogo ya gesi.
Changamoto nyingine ni kuongeza uwezo endelevu wa sekta ya gesi na kuwekeza katika miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme, na kudhibiti upotevu wa umeme wakati wa kuusafirisha na kuutumia.
“Changamoto nyingine tulizonazo ni kuendeleza vyanzo mbadala vya nishati ya umeme badala ya kutegemea maji, ambayo uzoefu unaonesha wakati wa kiangazi uzalishaji umeme unapungua kutokana na kina cha maji kupungua,” amesema.
“Wizara yetu [Nishati na Madini] ni miongoni mwa wizara zilizopo katika mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (Big Results Now-BRN) katika sekta ya nishati. Ili kuutekeleza ipasavyo tunahitaji wataalamu wazalendo waliobobea katika fani za mafuta na gesi,” ameongeza.
Wanafunzi wanena
Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti mara baada ya hafla ya kuwaaga, mmoja wa vijana wanaokwenda masomoni nchini China aliahidi kuonesha fadhila kwa Serikali baada ya kuhitimu masomo hayo.
“Kwanza niseme nimefurahi sana kupata nafasi hii. Nitakapohitimu masomo huko China nitarudi hapa nchini kuonesha shukurani kwa Serikali na uzalendo kwa nchi yetu.
“Lazima niwe na uchungu na nchi yetu, nitahakikisha ninarudi nyumbani [Tanzania] kuitumikia nchi yetu kukidhi matarajio ya Serikali yetu,” amesema Grace Mkongwa.
Kwa upande wake, Januarius Matata ameahidi kuwa tayari kulisaidia Taifa letu kulingana na taaluma atakayoipata nchini China.
Matarajio ya Wizara ya Nishati na Madini na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kwamba vijana wazawa wanaopelekwa kusoma fani za mafuta na gesi nje ya nchi, wataleta teknolojia itakayosaidia kupata ufumbuzi wa changamoto zinazoikabili nchi yetu, hususan katika kuendeleza sekta hiyo.