Miongoni mwa mambo yanayowatesa mabinti wengi ni kutokujua ni mwanaume gani hasa anayempenda kwa dhati, kwa sababu kuna mstari mwembamba sana unaotofautisha mwanaume mwenye mapenzi ya kweli na ‘tapeli’. Ungana na mimi mwandishi wako Isri Mohamed

Anakuweka karibu na Mungu

Kwanza kabisa ya mwanaume anayekupenda kweli na mwenye malengo na wewe ni kukusogeza karibu na Mungu, Yaani kama amekukuta na vijitabia vyako visivyompendeza Mungu basi lazima atapambana kukubadilisha, kama ulizoea kuvaa nguo fupi zisizo na maadili basi ujue taratibu ataanza kukuonesha kuwa hapendezwi nazo na atakununulia nguo zenye stara mpaka utamuelewa, kama ulikuwa mlevi wa kupindukia basi atahakikisha umeacha na atambatana na wewe kanisani ama msikitini, au kukukumbusha kila unapofika muda wa ibada.

Mawasiliano

Msingi mkuu wa mahusiano ni mawasiliano, hii ni dalili ya kwanza kukuonesha kuwa unapendwa, Namna anavyowasiliana na wewe, licha ya ubize wake lakini anahakikisha anakutafuta kukujulia hali, kujua umeamkaje, unaendelea na siku yako imeendaje, asikudanganye mtu hakuna mwanaume aliye bize kwa mwanamke anayempenda, ukiona hakupigii wala kukutumia meseji asubuhi mpaka jioni, kila siku wewe ndiye unamuanza na anakujibu shoti shoti, anafupisha maongezi, ujue hupendwi kukubaliana na hali halisi na uanze safari mapema, usisubiri akutamkie hiyo pekeyake inatosha kuwa ‘Red Flag’

Mazungumzo

Ukiona mwenzi wako akizungumza anatamka neno ‘Mimi’ na sio ‘sisi’ ujue hapo kuna walakini, mwanaume anayekupenda kweli atakuhesabu kwenye kila sentesi yake, atazungumza mipango yake yai maisha kwa kukujumuisha, atakupa nafasi ya kushauri na kuamua nini mfanye, atakwambia yanayomsumbua kichwa kwa sababu wewe ni sehemu ya maisha yake, utamsikia akiizungumzia kesho yenu, sio mtu anakwambia atakayekuoa atafaidi sana, halafu na wewe bado upo tu.

Wivu

Hii ni dalili ambayo watu wengi huipuuzia lakini ni nguzo muhimu sana ya kuitazama ukitaka kumjua mwanaume anayekupenda kweli, kama mwanaume hakuonei wivu, chochote utakachofanya sawa tu kwake, popote utakapoenda hana wasiwasi, wala hakuulizi utarudi muda gani, hakuna kitu kinachompa presha kwako weka alama ya kuuliza hapo, kwa kawaida mwanaume akikupenda lazima awe na wivu, wengine hukagua simu kila mnapoonana, kuna wale wanaoenda kupekua kwenye kurasa zako mitandaoni, mwingine anakupeleleza kwa watu wako wa karibu, ataanza kukuzuia kuwa karibu na marafiki zako wa kiume aliokukuta nao na mambo mengine mengi yenye viashiria vya wivu..

Yupo huru na wewe

Ukiona mpenzi wako hakufichi kama bangi yupo huru na wewe, hana hofu ya kuongozana na wewe popote, anakutambulisha kwa watu wake wa karibu hata wa kike bila kigugumizi basi ujue wewe ndiye mwenyewe, kwa kifupi anajivunia kuwa na wewe popote na mbele ya mtu yeyote, Dada huyo Mkaka anakupenda sana.

Anajitolea

Kama kuna nyakati za kujua nani anastahili kuwa ndugu yako basi ni nyakati za matatizo, hivyo hivyo hata kwenye mapenzi ili ujue mwanaume uliyenae anakupenda kweli basi ni katika kipindi hicho, anawezaje kujitolea kukusaidia ama kukufariji, anashikamana vipi na wewe kwa wakati huo, na hapa simaanishi anayetoa pesa tu, uwepo wake ni muhimu pia, sio ukiumwa mpenzi anatuma pesa tu hakanyagi hospitali na wakati yupo, umefiwa yeye ni kutuma rambirambi tu unalilia kwenye mikono ya watu wengine, kuna wakati pesa inakuwa sio muhimu kama uwepo wa mtu, mchunguze vizuri uliyenae anaweza kujitolea kwa hali na mali kwako?

Anakuheshimu

Neno heshima lina uwanda mpana sana kulielezea, lakini nataka kukwambia mwanaume akikupenda Atakuheshimu sana, sijasema hatachepuka ila atakuheshimu, hautawahi kuona vitu ambavyo vitahatarisha mahusiano yenu, atakuweka mbali navyo kabisa, haitatokea ukakosea na akakudhalilisha barabarani au mbele za watu popote pale, atatafuta njia nzuri ya kukueleza kwa nidhamu, hata mkigombana hautasikia kauli za kidhalili, ambazo zitabaki akilini mwako hata baada ya ugomvi kuisha.

Atakukuza kiuchumi

Najua mlivyoona hii mmefikiria moja kwa moja kwamba anatakiwa akupe pesa, La hasha, Mwanaume akikupenda kweli atakusapoti kwenye kukuza uchumi wako kwa njia zote, ushauri, kukuongezea mtaji kama ni mfanyabiashara, kukutafutia masoko na wateja, kukuonesha mbinu za kukuza biashara yako, kukutia moyo mambo yanapoenda kombo na kwa njia nyingine nyingi ilimradi zitakuongezea kipato, hatataka uwe Aishi Manula nyumbani ukisubiri kuletewa tu.

Atakuvumilia

Kuna ule msemo unasema ukiona mahusiano yamedumu kwa muda mrefu basi ujue mwanamke ni mvumilivu, hiyo ndiyo sifa yetu wanawake, lakini ukweli ni kwamba hata mwanaume akikupenda kwa dhati lazima atakuvumilia, na uvumilivu si tu wa tabia, unaweza kuwa upo mbali kimasomo au kikazi kwa miaka kadhaa na ukarudi ukamkuta akikusubiri na mkaendelea na maisha yenu, unaweza kuwa na vijitabia vyako vinamkera lakini kwa sababu anakupenda atavivumilia akikurekebisha taratibu taratibu.

Hatasikiliza watu wa pembeni

Ataamini yeye ndiye mtu pekee anayekujua vizuri, na maneno ya watu wengine pembeni hayana maana kwake, hataruhusu kusikiliza na hata akiambiwa hatayaweka akilini, sio marafiki wala hata ndugu zake watakaoweza kuvuruga akili yake kwa maneno, mwanaume akikupenda ana sifa ya kuwa na msimamo mkali juu yako, ni kama nyumba yenye zege haiwezi kudondoshwa na upepo.

Zipo dalili nyingi hata zaidi ya hizo kumi nilizokuorodhoshea hapo lakini hizo ndizo imara ambazo kama huyo mwanaume hana basi ujue unapoteza tu muda wako.