Zaidi ya mashabiki 20, walipata mshtuko Jumamosi iliyopita wakati mchezo wa Ligi Kuu kati ya Simba na Yanga iliyotoa uwanjani na ushindi wa mabao 2-0.
Ajabu ni kwamba kati ya hao, 15 walikuwa ni wa Yanga licha ya timu yao kushinda mabao hayo mawili katika mchezo huo uliovutia maelfu ya mashabiki kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Daktari wa JAMHURI, Dk. Mohamed Abubakar, mashabiki wengi wa Wanajangwani hao walikuwa na hofu kubwa ya kufungwa.
Anasema kwamba kuzimia au shock ni upungufu wa mfumo wa mzunguuko wa damu na maji mwilini, matokeo yake sehemu muhimu mwilini hasa kwenye ubongo na moyo kukosa hewa aina ya oksijeni ya kutosha. “Hali hii inahitaji huduma ya haraka ili kuzuia uharibifu mkubwa wa ubongo na kifo,” anasema Dk. Abubakar aliyezungumza na JAMHURI juzi.
Anasema kwamba kilichokuwa kikifanywa na wahudumu hao wa afya ni sahihi kwa kuwalaza chali ili kuzuia utokaji mwingi wa damu.
“Sasa kama amepoteza fahamu, mgonjwa anatakiwa alazwe chali na kuinua miguu juu ukiiegemeza, ili damu nyingi yenye oksijeni isukumwe kuelekea kwenye ubongo,” anasema daktari huyo na kuongeza kuwa, “Hizi ni hatua hata ikimtokea mtu mwingine.” Anasema, “Pia mgonjwa inatakiwa afunikwe nguo nzito ili kuuweka mwili joto joto ukisubiri msaada wa kumpeleka hospitali.”
Kabla ya kuivaa Yanga, timu ya Simba ilifanya vema kwenye michuano sita mfululizo hadi kufikia kuongoza msimamo wa ligi huku Yanga ikiwa imepata sare moja kabla ya kufungwa na Coastal Union.
Mmoja wa watoa huduma ya kwanza, anasema Vijana wa Skauti, walithibitisha kuwa mashabiki wengi walikuwa ni wa Yanga kutokana na mavazi ya njano na kijani.
Katika mechi hiyo ya ‘debi’ mashabiki wa Simba walionesha kuwa na imani ya kushinda, lakini kibao kiliwageukia hasa baada ya Beki wa Simba, Abdi Banda kulimwa kadi nyekundu.