Daktari raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 37 ambaye amekuwa akisomea Shahada ya Uzamili ya Udaktari katika Upasuaji katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala amefariki dunia kutokana na ugonjwa wa Ebola, Chama cha Madaktari wa Upasuaji Uganda kimetangaza.

Kulingana na gazeti la The monitor nchini Uganda, haijabainika jinsi Dkt.Mohammed Ali aliambukizwa lakini kifo chake kinajiri saa chache baada ya Wizara ya Afya siku ya Ijumaa kutangaza kwamba idadi ya waliofariki kutokana na mlipuko wa Ebola nchini imeongezeka hadi saba.

“Ni kwa masikitiko makubwa tumepokea taarifa za kufariki kwa Dk Mohammed Ali, raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 37 ambaye alikuwa akisomea Shahada ya Uzamili ya Upasuaji katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Kampala. Dk. Ali alishindwa katika vita dhidi ya Ugonjwa wa Virusi vya Ebola,” Chama cha Madaktari wa Upasuaji Uganda kiliandika kwenye Twitter Jumamosi.

Waziri wa Afya, Dkt. Jane Ruth Aceng alisema Dk Ali alipimwa na kuwa na Ebola Septemba 26, 2022 na alifariki dunia alipokuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Fort Portal. Alikufa saa 3 asubuhi siku ya Jumamosi, The monitor ilimnukuu akisema..

“Dkt. Ali ndiye Daktari wa kwanza, na mhudumu wa afya wa pili kuugua Ebola. Wa kwanza alikuwa mkunga kutoka Kliniki ya St Florence, kisa kinachowezekana, kwa sababu alifariki kabla ya kupimwa,” Dkt. Aceng alitweet Jumamosi

Hata hivyo Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu amethibitisha kifo cha daktari Muhammed Ali (37) raia wa Tanzania kilichotokana na ugonjwa wa Ebola huko nchini Uganda.

Mohammed ambaye alikuwa anasoma shahada ya pili nchini humo, anakuwa daktari wa pili kupoteza uhai kufuatia ugonjwa wa virusi vya Ebola vilivyozuka wiki mbili zilizopita nchini Uganda.