Mahakama Kuu Kanda ya Tabora imemhukumu Amos Mathias, mkazi wa Kijiji cha Nhungulu, Wilaya ya Nzega mkoani hapa kifungo cha miaka 15 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuua bila kukusudia kwa kujifanya daktari.
Hukumu hiyo imetolewa juzi na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tabora Athuman Matuma baada ya kusikiliza shauri hilo na kujiridhisha pasipo shaka kuwa mtuhumiwa anastahili adhabu hiyo.
Amesema kitendo cha mtuhumiwa kujifanya daktari na kumfanyia upasuaji wa tumbo na sehemu za siri Mzee mwenye umri wa miaka 78 aliyekuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa ngiri kinyume na maadili ya utumishi.
Jaji Mfawidhi Matuma amebainisha kuwa mahakama imepitia hoja za pande zote mbili, upande wa Jamhuri na upande wa utetezi na kujiridhisha kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo pasipo kukusudiwa.
Ameongeza kuwa kitendo cha mtuhumiwa kuwatoza ndugu wa marehemu kiasi cha sh laki 2 kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji mgonjwa wao wakati anajua hana taaluma hiyo na ni uongo na udanganyifu ni kosa kisheria.
Amesema licha ya kuomba kiasi hicho wanandugu walitanguliza kiasi cha sh laki moja na elfu arobaini ila baada ya kuona tatizo linazidi kuwa kubwa na hali ya mgonjwa inazidi kuwa mbaya aliomba wamkimbize hospitali kwa matibabu zaidi.
Jaji Mfawidhi Matuma amebainisha wazi kuwa mahakama imetoa hukumu hiyo ili iwe fundisho kwa wale wote wenye tabia kama hizo na kuongeza kuwa hatua za kisheria zitaendelea kuchukuliwa kwa yeyote anayetumia vibaya taaluma yake ili kukomesha tabia hiyo.