NA MWANDISHI WETU 

Moja ya mechi nzuri iliyojaa ufundi mwingi na utulivu mkubwa. Ama kwa hakika mashabiki wa soka nchini wameona ukuu wa timu hizi mbili katika soka la Tanzania. Asanteni Simba na mabingwa Yanga kwa burudani nzuri ya weekend ya mwisho wa mwezi.

Tukianza na Yanga, kwa ujasiri mkubwa ninapenda kuwaambia wanachama na wapenzi wa Yanga, msimu huu wa 2021-22 wana timu nzuri kwa ajili ya kuutafuta ubingwa ambao umekuwa ndoto kwa misimu kadhaa.

Nabi alikiingiza kikosi chake kwa mfumo wa 4-3-3; eneo la ulinzi wakisimama Djuma kulia na Kibwana kushoto, huku kati akicheza Job na nahodha Mwamnyeto.

Safu ya kiungo Nabi alitumia double pivot ya Bangala na Aucho, ambapo juu yao alisimama huru Feisal kutengeneza triangle ya midfield kwenye low blocking approach. Juu wakicheza Mayele kama striker kati huku kulia akicheza Malick na kushoto Moloko. 

Nabi alikuja na mfumo huu akijua ubora wa Simba SC eneo la kati na kwenye wings, hivyo alihitaji uwezo wa kukaba (double pivot), kumiliki mpira na kuhakikisha mpira unahama kwa kasi box moja kwenda jingine.

Hapo ndipo pattern ya Feisal na Aucho ilipokuwa inatumika pale kati huku Malick na Moloko wakitembea kwenye wings

Kimbinu na kiufundi alifanikiwa sana Nabi, kwa kuwa ilimfanya kuvunja muunganiko wa viungo wa Simba SC pale kiasi cha Lwanga muda mwingi kucheza kama lone defensive midfielder, hali iliyomfanya kucheza rafu muda mwingi ili kupunguza alternation ya Feisal na Aucho.

Uwezo huo wa kuimudu Simba kati na kwenye wings hususan dakika 20 za mwanzo ndiko kulisababisha Yanga kupata goli zuri dakika ya 11 ya mchezo kupitia kwa Fiston Mayele baada ya pasi nzuri kutoka kwa Malick.

Nisifu pia jicho la Nabi kwenye pattern yake, licha ya kuanza na 4-3-3 lakini alihakikisha wingbacks wake hawapandi mara kwa mara kuepuka counter za Simba SC kutokana na quality ya wachezaji wao ambao wana uwezo mzuri sana wa kucheza pasi za kasi na kuhama upande mmoja kwenda mwingine kwa kasi.

Hapa alidhamiria kukata kasi ya Kanoute, Sakho na Bwalya ili forward line ya Simba kwa Mugalu muda wote iwe tactically off balance, ndiyo maana Mugalu muda mwingi alikuwa anaingia kwenye yard 18 akiwa hana muda mzuri wa kufanya uamuzi.

Tukija kwa Simba SC, waliingia uwanjani na mfumo wa 4-1-2-3 Gomez akidhamiria kuweka balance kwenye kujilinda na kushambulia.

Nyuma akianza na Kapombe kulia na Zimbwe Jr kushoto. Kati walisimama Joash na Wawa. Joash aliumia na kuingia mwamba Kennedy.

Thadeo Lwanga alicheza kiungo cha chini akisaidiwa na Kanoute kama box to box midfielder huku pembeni yake akisimama Dilunga na mbele alisimama Mugalu kama striker akizungukwa na Sakho na Bwalya. 

Kwa umbo, Simba SC walikuwa vizuri lakini kimbinu walipwaya kwa kuanza na pattern ya Kanoute na Lwanga.

Viungo wa Yanga walimzunguka Lwanga kukata umeme wake na Kanoute ambaye ni aina ya viungo ambao wanatembea na mpira, yaani anahama na movements za mpira kitu ambacho kiliwapa uhuru viungo wa Yanga kuikata Simba kati na kuondoa ile balance ambayo Gomes aliitaka.

Dilunga aliliona hilo akawa anasaidia sana kwenye marking na kupandisha mipira juu, kitu ambacho kilimfanya muda mwingi kuwa chini na Simba ku-struggle kwenda mbele ikiwa na umbo zuri la kushambulia. 

Mabadiliko ya kuwatoa Dilunga, Kanoute, Sakho na Zimbwe Jr ilikuwa ni kulitafuta umbo la kushambulia kutokea chini, ambalo Yanga walikuwa wanalivunja muda wote. 

Bocco aliingia kujaribu kuituliza safu ya ushambuliaji ambayo ilikuwa inayumba kwa Mugalu. Muzamiru kusaidiana na Lwanga kwenye marking ili Bwalya arudi kwenye play making kwenye forward line ingawa Lwanga aliishia kula red card. 

Si kwamba Simba ilikuwa mbovu, bali ni ubora wa Yanga hususan kwenye approach yao na approach ya Gomes eneo la kiungo kukataa. Ndiyo maana ninasema kwa ujasiri mkubwa kwamba ilikuwa mechi bora ambayo ufundi wa makocha umeamua matokeo.