*Kaimu Rais afurahia walimu kupandishwa madaraja, ajira mpya

*Baada ya madarasa, aiomba Serikali sasa kugeukia nyumba za walimu

*Katibu Mkuu: Wingi wa walimu umepunguza mzigo wa ufundishaji

*Atoa wito kwa walimu akisema: Sasa twendeni tukachape kazi 

DODOMA

Na Mwandishi Wetu

Wakati Watanzania wakiungana na mamilioni ya watu duniani kote kusherehekea Sikukuu ya Wafanyakazi (Mei Mosi), Chama cha Walimu (CWT) kimeonyesha kuridhishwa na mwenendo wa serikali katika kuboresha masilahi ya walimu pamoja na mazingira ya ufanyaji kazi.

Akizungumza na JAMHURI katika makao makuu ya muda ya CWT jijini Dodoma siku moja kabla ya sherehe za Mei Mosi, Kaimu Rais wa chama hicho, Mwalimu Dinah Mathamani, anasema katika kipindi cha mwaka mmoja walimu wameshuhudia mambo makubwa yakifanyika.

“Kama chama, mazungumzo kati yetu na serikali katika kutetea masilahi ya walimu wote nchini yamekuwa na matokeo chanya. Ndani ya mwaka huu mmoja tangu sherehe kama hizi za mwaka jana, walimu wamepandishwa vyeo na madaraja,” anasema.

Mwalimu Dinah aliyekuwapo jijini Dodoma kushiriki maadhimisho ya mwaka huu, anasema yapo mengi ya kujivunia kwa CWT, walimu na hata watumishi wote wa umma kwa ujumla wao.

Anasema kwa mwalimu na mtumishi wa umma kupandishwa cheo ni zaidi ya kuongezwa mshahara kwa kuwa cheo huendana na nyongeza ya mshahara na malupulupu mengine.

Mbali na vyeo na madaraja, Mwalimu Dinah anasema madai mbalimbali yaliyokuwapo miongoni mwa walimu yamefanyiwa kazi, akiyataja baadhi kuwa ni malimbikizo ya (posho za) likizo na matibabu.

“Yote haya yamelipwa na ndiyo maana ninasema, Rais Samia Suluhu Hassan anawapenda walimu na watumishi wa umma,” anasema.

Anasema kupitia fedha zilizotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) kwa ajili ya kupunguza madhara yaliyosababishwa na UVIKO – 19, serikali imejenga madarasa ya kutosha, hivyo kuboresha mazingira ya ufundishaji.

Awali, wanafunzi walikuwa wakijazana katika darasa moja na kumpa mwalimu wakati mgumu na sasa anasema:

“Hilo limepata suluhu. Muhimu sasa ni kwa serikali kugeukia nyumba za walimu. Walimu, hasa wanaopangiwa kufanya kazi vijijini hukumbana na tatizo la makazi na kupata usumbufu mkubwa,” anasema mama huyo.

Anasema tatizo lililopo vijijini ni kwamba unakuta shule haina nyumba na bahati mbaya hata nyumba ya kupanga pia hakuna.

JAMHURI linafahamu kwamba kuna nyakati walimu wapya wanaopangiwa kazi vijijini hulazimika kuishi kwa muda nyumbani kwa maofisa wengine wa serikali, kama watendaji au wenyeviti wa vijiji.

Mwalimu Dinah anatamani kuuona mwaka unaofuata ukitatua tatizo la makazi kwa kujenga nyumba za walimu karibu na shule wanakofanyia kazi.

Katibu Mkuu amuunga mkono

Kauli ya Mwalimu Dinah inaungwa mkono na Katibu Mkuu wa CWT, Mwalimu Deus Seif, anayefafanua kwa kusema kuwa ndani ya miezi 12 ya Rais Samia, walimu 227,000 wamepandishwa vyeo.

Anasema bado kuna walimu wengine watakaopandishwa madaraja na vyeo kuanzia Julai Mosi mwaka huu, kwa mujibu wa Bajeti iliyowasilishwa bungeni na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Jenista Mhagama.

“Sasa ukipiga hesabu za walimu walionufaika ndani ya mwaka huu mmoja, utaona kwamba ni asilimia 92 hivi ya walimu wote. Yaani hiyo asilimia 7.2 iliyosalia ni wale waajiriwa wapya,” anasema Mwalimu Seif. 

Akizungumzia ajira mpya, Mwalimu Seif ambaye ofisi yake ndiyo hushughulika na kazi za kila siku za CWT, anasema serikali imetoa vibali vinne tofauti vya kuajiri jumla ya walimu 39,000.

“Hii ni asilimia 15 ya wote waliopo kwa sasa serikalini. Ni hatua kubwa sana. CWT tunajivunia katika hili na kuipongeza serikali, kwa kuwa wingi wa walimu hupunguza mzigo wa ufundishaji.

“Ifahamike kwamba walimu wanaostaafu nao pia ni wengi, hivyo lazima kuwa na ajira za mara kwa mara kuziba mapengo yanayoachwa wazi,” anasema.

Mwalimu Seif anaungana na kauli ya Mwalimu Dinah akisema kitu muhimu kwa sasa ni kuelekeza nguvu kwenye ujenzi wa nyumba kwa ajili ya makazi ya walimu.

Anasema zipo nyumba 809 (mbili kwa moja) zimejengwa, lakini hizo zina uwezo wa kuwahifadhi walimu 1,600 tu, hivyo juhudi za makusudi zinapaswa kuelekezwa eneo hilo.

“Lazima tuishukuru serikali kwa kuwa madarasa tayari, na hata vitabu pia vipo vya kutosha,” anasema.

Yaliyoahidiwa Mei Mosi 2021

Awali, Mwalimu Dinah ametoa wito kwa serikali kuangalia shule ambazo zina walimu wachache ndiko ipeleke walimu wengi, hususan walimu wa masomo ya sayansi na kuboresha maabara.

“Maabara nyingi hazijakamilika, hivyo ni muhimu zikakamilishwa kwa wakati ili tuwajenge vizuri watoto wetu na hatimaye waweze kuingia katika soko la ajira la dunia wakiwa wamekamilika,” anasema na kuongeza:

“Kwa ujumla yaliyosemwa Mei Mosi mwaka jana mengi yamefanyiwa kazi. Kwani kwa sasa walimu wanapata ruhusa ya kwenda kusoma, hakika tunapaswa kutoa pongezi kwa serikali.”

Wito kwa walimu

Kutokana na uboreshaji uliofanyika katika maeneo mbalimbali kwenye sekta ya ualimu, Kaimu Rais wa CWT anawaomba walimu sasa kufanya kazi kwa bidii, akisema wanapoomba ongezeko la mishahara wazingatie pia utendaji wenye tija.

“Kaulimbiu ya CWT ni ‘Haki na Wajibu’. Kwa hiyo na sisi sasa tukachape kazi. Tuwajibike,” anasema na kuungwa mkono na Mwalimu Seif.

Mwalimu Seif anasema: “Kwa kusema ukweli sasa walimu tunapaswa kufundisha. Tena kwa umakini mkubwa. Tukatimize wajibu wetu kwani serikali imefanya wajibu wake.”

Pia ametoa wito kwa wanafunzi kusoma kwa bidii na kufuata sheria za shule zilizopo, akiweka wazi kuwa nidhamu kwa mwanafunzi huchangia kufanya vema katika masomo.

Mwalimu Commercial Bank

Kwa upande mwingine, Mwalimu Seif amewaomba walimu kuitumia Benki ya Mwalimu (MCB) ili waweze kunufaika na uwepo wake.

Mwalimu Seif anasema iwapo walimu watapitisha mishahara MCB, benki hiyo itasimama imara na kuendelea kuwahudumia kwa kuwapa mikopo nafuu.

“Walimu wamekuwa waathirika wa ‘mikopo umiza’ ndiyo maana tukaanzisha MCB. Ni vema wakatambua kwamba wao ni wamiliki wa benki hii na kwamba kwa mujibu wa sheria, mwajiriwa ana haki ya kuchagua benki ya kupitishia mshahara wake.

“Kwa hiyo walimu pitisheni mishahara MCB. Hii ndiyo benki pekee mnayoimiliki,” anasema.

Anasema katika zama hizi za teknolojia, MCB ina uwezo wa kuhudumia walimu wote nchini.