Maji yanazidi kuchemka ndani ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), huku mkataba wa kinyonyaji wa mshauri wa mradi wa ujenzi na madeni kwenye Mfuko wa Jamii wa PSPF, yakiwa ni miongoni mwa mambo yanayoendelea kwenye chama hicho.

 JAMHURI limebaini CWT iliingia mkataba wa kinyonyaji na Kampuni ya Settlements De Popolo Consultants wenye gharama ya Sh milioni 960, lakini kutokana na masharti mengine ya kimkataba kiasi hicho kimeongezeka hadi Sh bilioni 3.

Tayari mkataba huo umevunjwa kwa barua yenye kumbukumbu namba TTU/004/DE POPOLO/2019 ya Februari, mwaka huu iliyosainiwa na Katibu Mkuu wa CWT, Mwalimu Deus Seif.

Waliotia saini mkataba huo ni aliyekuwa Katibu Mkuu wa CWT, Yahya Msulwa na kushuhudiwa na Mussa Mnyazi, ambaye alikuwa Mhasibu wa chama hicho.

Kwa upande wa Settlements De Popolo Consultants waliosaini mkataba huo ni Simkuru Tamila akiwa ni Msanifu Majengo Mkuu na kushuhudiwa na Benedict Mullungu ambaye naye ni Msanifu Majenzi Mkuu.

Kampuni ya Settlements De Popolo Consultants iliyosajiliwa hapa nchini iliingia mkataba huo Septemba 7, 2016. Ulihusu kusimamia ujenzi wa majengo ya CWT katika mikoa ya Geita, Songwe, Katavi, Njombe, Simiyu na Dar es Salaam.

JAMHURI limebaini kuwa katika kipindi ambacho mtaalamu mshauri alikuwa anaendelea na kazi hiyo, gharama zake zilikuwa hazitofautiani na za mkandarasi wa ujenzi wa majengo hayo. Hadi Februari, mwaka huu wote walikuwa wamelipwa kiasi kinacholingana, yaani Sh zaidi ya bilioni 3.

Gharama halisi za mradi zikiwa ni Sh milioni 960, ambazo kwa mujibu wa mkataba zilihusisha huduma za mwanzo ambazo kwenye mkataba zimeorodheshwa katika kipengele cha 1.1 na 1.6. Gharama hizo ni sawa na asilimia 10 ya gharama ya mradi, yaani Sh milioni 516. 

Vipengele 1.1 na 1.6 vya mkataba huo baina ya CWT na Settlements De Popolo Consultants vinasomeka kama ifuatavyo; kile cha 1.1 kinasomeka: msanifu majengo atajadili mahitaji ya mteja ikiwa ni pamoja na ukubwa na uwezo wa kifedha; huku kipengele 1.6 kikisomeka: msanifu majengo atashauri kuhusu kiwango cha watenda kazi katika eneo la mradi.

Kipengele kingine kilichozingatiwa ni huduma za msingi ambazo zilitengewa asilimia 3.5 ya fedha za mradi ambazo ni Sh 309.321. Kiwango hicho cha fedha kikafafanuliwa kwenye kipengele 1.9 na 1.10. Sh milioni 134.4 zilitengwa kwa ajili ya huduma nyinginezo. Gharama zote hizo hazikuwekewa Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT).

 Imebainika kuwa gharama kubwa za mshauri wa mradi huo zilifichwa kwenye kipengele cha 4.32 cha mkataba huo. Kipengele hicho kinasema gharama zitakazotozwa na msanifu majengo (mshauri wa mradi) zitahusisha: kuchapisha, gharama za kununua nyaraka zote, michoro, ramani, picha na kumbukumbu zote zilizotumika baina ya msanifu majengo, mteja, washauri wa mradi na makandarasi.

Mambo mengine ni pamoja na CWT kulipia gharama za hoteli na usafiri, ikiwa ni pamoja na kutoa fedha za mafuta ya magari kwa viwango vilivyopo. Jambo jingine ambalo lilikuwa ni jukumu la CWT kwenye mkataba huo ni malipo yote yaliyofanywa kwa niaba ya mteja (CWT), kama vile gharama alizoingia mshauri wakati wa kutangaza zabuni.

 Hivyo ni baadhi ya vipengele vilivyojificha ambavyo vimeitafuna CWT kwa miaka mitatu kuanzia mwaka 2016 hadi Februari, mwaka huu. Kipengele cha 4.32 cha mkataba huo ndicho kimeiumiza CWT.

 Gazeti la JAMHURI limemtafuta na kumpata Rais wa CWT, Leah Ulaya; hata hivyo, amegoma kuzungumzia undani wa suala hilo kwa kile alichosema kuwa Jumamosi huitumia kushinda kanisani.

Mhandisi Simkuru Tamula ambaye ndiye aliyesaini mkataba huo anasema kampuni yake ililipwa kwa mujibu wa mkataba waliosaini Septemba, 2016 na CWT.

 “Kuhusu suala la kulipwa fedha kiwango sawa na mkandarasi, hilo sidhani kama ni kweli. Tumeshangaa CWT wamevunja mkataba wetu ghafla…tumefanya kazi tangu mwaka 2016, ninashangaa wamevunjaje mkataba. 

“Baada ya kuvunja mkataba tuliomba kulipwa fedha zetu kiasi cha Sh milioni 134. Lakini pia tumeangalia sababu ya kuondolewa kwetu, kwa kweli inaacha maswali mengi. Yaani kama kweli CWT ilikuwa inapitia kipindi kigumu cha fedha si wangetushirikisha kwa vile sisi ndio washauri wa mradi husika,” amesema Tamula.

Anasema kama kweli CWT walikuwa wanamaanisha kuhusu suala la ukata, Kampuni yake ya Settlements De Popolo Consultants ingeweza kuwashauri waendelee na ujenzi kwa mikoa michache badala ya kusimamisha kazi. 

“Katika uzoefu wangu wa kazi sijawahi kukutana na jambo kama hilo, yaani kunyang’anywa kazi wakati tukiwa tunaelekea mwishoni…hiyo imetokea kwenye Chama cha Walimu Tanzania tu,” amesema Tamula.

Katibu Mkuu wa CWT, Mwalimu Seif, ambaye ndiye aliyesaini barua ya kusitisha mkataba na Settlements De Popolo Consultants, anasema sababu za uamuzi huo ziko wazi.

 “Mtu asipokuwa makini hawezi kuelewa, kwenye mkataba kiasi cha fedha kinachoonyeshwa ni Sh milioni 960, ila kutokana na vipengele vingine ndani ya mkataba huo CWT ikajikuta imeshalipa zaidi ya Sh bilioni 3. Ni mwendawazimu tu anaweza kuendelea na mkataba wa kinyonyaji namna hiyo.

“Kwenye mkataba mpaka kuna vipengele kwamba huyo mshauri wa mradi akienda kukagua kazi zinavyoendelea alipwe na Chama cha Walimu…kwa masilahi mapana ya chama tuliona bora tuusitishe ili kupata ahueni.

 “Mwaka jana tuliangalia malipo ya jumla ya mradi huo, tukagundua yalikuwa nusu kwa nusu, yaani mshauri amelipwa sawa na mkandarasi. Katika masuala ya ujenzi nadhani jambo hilo lilikuwa linafanyika CWT pekee. Tukaona hiyo ni shida, maana chama wakati kinatakiwa kubana matumizi na kutumia vizuri, hali ilikuwa tofauti,” anasema Mwalimu Seif. 

Anasema kimsingi CWT haijasema kwamba mshauri hafai, isipokuwa gharama zilizokuwa zimefichwa kwenye mkataba ndizo zilikuwa kikwazo; na kwamba kuna vikao vinaendelea Dodoma ili kuweka utaratibu wa kuwaita mkandarasi na mshauri kuweka mambo sawa.

 “Tutawaita Suma JKT ambao ndio makandarasi na Settlements De Popolo Consultants ili tulizungumze suala hili; lengo kubwa likiwa kushusha gharama na kumaliza kazi husika kwa wakati,” anasema.

 

Hifadhi ya jamii

Katika kipindi cha miaka miwili CWT ilishindwa kulipa michango ya kisheria kwenye Mfuko wa Hifadhi ya Jamii wa PSPF.

Katibu Mkuu aliyepita, marehemu Yahya Msulwa, aliacha deni hilo likiwa Sh bilioni 1.2 (Novemba 2017), lakini hadi Juni, mwaka jana deni hilo liliumuka na kufikia Sh bilioni 2.5. JAMHURI limebaini fedha za michango zilichotwa kutoka CWT. 

Chanzo chetu kinasema fedha za malipo hayo zitakuwa zimetoka mara mbili, kwani Katibu Mkuu mpya alilazimika kulipa madeni yote.

Katibu Mkuu anasema: “Tumelipa michango yote ya nyuma na sasa rekodi zetu zimekaa vizuri. Ni kweli kwamba kiasi cha Sh bilioni 2.5 kiliidhinishwa kwa ajili ya malipo hayo ya kisheria ila fedha hizo hazikulipwa, si busara kuzungumzia mambo yaliyofanywa na watu wengine, itoshe kusema tumerekebisha. 

“Tumelazimika hata kubadili mfumo wa utoaji fedha za mabaki kwa wanachama wetu wanaostaafu, sasa tunalipa fedha kwenye akaunti za wahusika…awali udanganyifu ulikuwa mkubwa sana, mfumo huo umefanya kazi kuanzia mwaka 2015 hadi Desemba 2018 tulipoubadilisha.

 “Ilifikia hatua wilaya zinaleta takwimu za walimu hewa, ilifikia kipindi tukaletewa kwamba walimu 144 wamestaafu kwa mwezi mmoja kutoka kwenye wilaya moja,” amesema Mwalimu Deus.

 “Kuna mambo yanakera sana hapa CWT, simuoni hata Katibu Mkuu akiweza kuvunja mtandao wa wapigaji ndani ya chama, maana anaonekana yuko peke yake…anajaribu kukirudisha chama ila anaitwa majina ya kumkatisha tamaa. 

“Juni, mwaka huu (2019) tulikuwa na kikao na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Ajira, Kazi na Watu Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama, mambo haya yalizungumzwa, lakini bado watu hawasikii wanadhani bado CWT ni shamba la bibi,” kimesema chanzo chetu. 

Kuna madai kwamba baadhi ya viongozi waandamizi wa CWT wamejilimbikizia mali kinyume cha sheria katika Mkoa wa Dar es Salaam, mmoja wa mikoa magharibi mwa nchi.

 

Kutorudisha masurufu

 Ndani ya CWT kumewapo tabia ya baadhi ya maofisa wake kuandikiwa na kupewa masurufu kwa safari ambazo hawaendi.

Katibu Mkuu wa CWT ameandika barua ya kuwataarifu viongozi wa chama hicho katika ngazi zote ambao walichukua fedha za safari, lakini hawakwenda; wahakikishe wanazirejesha.

 

Usuli

Wakati sasa yakijitokeza hayo, huko nyuma Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aliwahi kukagua na kubaini upungufu kadhaa. Baadhi ya mambo yaliyojitokeza ni:

Katiba ya CWT haijaweka bayana ushirikishwaji wa kila mwanachama katika ngazi mbalimbali za uongozi kwenye kutoa maoni na mapendekezo ya kuboresha katiba ya chama.

Hivyo, CAG alishindwa kuthibitisha kama wanachama wa CWT walitoa mawazo yao katika kuboresha katiba ya chama ya mwaka 2014 ambayo imeonekana kuwa na upungufu.

 2. Katiba ya CWT na kanuni zake zinakinzana juu ya majukumu ya Bodi ya Wadhamini katika usimamizi wa mali za chama; kulingana na katiba ya chama, Ibara ya 35(b), wadhamini ni waangalizi na wadhibiti wa mali za chama wakati kanuni ya chama Na. 37(a) inasema mali zote za chama zitaandikishwa kwa jina la Wadhamini wa Chama. Hii inaleta mkanganyiko juu ya majukumu halisi ya Bodi ya Wadhamini katika mali za chama, pia inaweza kuleta mgongano wa kimasilahi katika mali za chama.

 3. Uchunguzi umebaini kuwa mali za CWT hazijasajiliwa kwenye daftari/rejesta ya mali za kudumu, yakiwemo magari, majengo, kompyuta, samani na kadhalika.

4. Katiba ya CWT ina upungufu katika ukomo na unufaikaji kwa mwanachama aliyefariki dunia au kustaafu, kwani Ibara ya 9.2 imeeleza kwamba mwanachama akikoma kuwa mwanachama hatarudishiwa ada zake, lakini wakati huo huo Kanuni ya CWT Na. 29 imeeleza kuwa mwanachama akistaafu akiwa amechangia CWT miaka 15 mfululizo atapewa mkono wa kwaheri, lakini mkono huo haukuwekwa bayana kuwa ni wa kitu gani au kiasi gani cha fedha. Hali hii inaweza kuleta upendeleo au migogoro katika chama.

5. Uchunguzi haukuweza kujiridhisha kwenye mchakato uliofanywa na CWT pamoja na vigezo vilivyotumiwa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi. Kwenye utoaji wa mkataba wa kukitambua Chama cha Walimu Tanzania kama chama kinachotetea haki na masilahi ya walimu wote Tanzania Bara pamoja na mkataba wa kutoa mamlaka kwa Chama cha Walimu juu ya utozaji wa Ada ya Uwakala kwa walimu wasio wanachama (Recognition and Agency Shop Agreements) ambapo mwaka 2014, mwezi Aprili chama kilionekana kuwa na wanachama zaidi ya 50% ya walimu wote Tanzania Bara, hali iliyokipa chama haki ya kutoza 2% ya mshahara wa kila mwalimu hata asiye mwanachama wa CWT. Taarifa hii iliombwa kwa Katibu Mkuu wa chama ili kujiridhisha uhalali wa taarifa hiyo, lakini hatukuweza kupatiwa.

6. Sheria ya Ajira na Uhusiano Kazini ya mwaka 2004, Kanuni za CWT za mwaka 2015 sehemu ya 4(C), Agency Shop na Recognition Agreements za mwaka 2014 zilihitaji chama kiwe na akaunti za benki tofauti za kuweka michango itokanayo na ada za wanachama na akaunti ya kuweka Ada ya Uwakala kwa walimu wasio wanachama ili kuweza kutofautisha kulingana na matumizi yatokanayo na shughuli zinazolenga wanachama na zile zinazolenga watoa Ada ya Uwakala. Kinyume cha matakwa hayo, chama hakijaweza kutenganisha akaunti hizi.

 7.  Hakuna ushahidi wa kisheria juu ya uwepo na umiliki wa Kampuni ya CWT iitwayo Teachers Development Company Limited (TDCL) ambayo ni kampuni yenye hati ya usajili namba 45719 na iliyoanzishwa na CWT kwa madhumuni ya kusimamia jengo la Mwalimu lililopo llala Boma, ikiwemo kupangisha, kukusanya mapato yatokanayo na kodi ya pango na kufanya ukarabati wa jengo hilo. Lakini baada ya kufuatilia kampuni hii haijasajiliwa kisheria na BRELA, kwani kampuni inayotambulika BRELA ni Teachers Development (T) Limited ambayo inatumia hati ya usajili namba 45719, lakini kumekuwa na utofauti wa majina yaliyotumika kwenye kuisajili kampuni hii wakati taarifa nyingi za Chama cha Walimu Tanzania hazijaonyesha kuwepo kwa kampuni inayotumia jina la Teachers Development (T) Limited, hivyo kuibua utata kama kweli hii ni kampuni halali ya CWT au kuna namna imefanyika kuondoa uhalali wa walimu kuwa na kampuni yao wanayoitambua kisheria.

Timu ya uchunguzi ilijaribu kuomba kama kuna nyaraka zozote ndani ya CWT, ambazo zimetumia jina la Teachers Development (T) Limited lakini liazikuwepo, hivyo kwa kutumia nyaraka zote za CWT na kutokuwepo kwa nyaraka zinazotumia Teachers Development (T) Limited ni dhahiri hii si kampuni ya CWT. Rejea majibu ya BRELA kwa barua Na. MITM/RC/MISC/2017/21 ya BRELA ya tarehe 7/5/2017.