Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Mtwara

Chama cha Wananchi (CUF) kimefanya uzinduzi wa kampeni zake kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Uzinduzi huo ulifanyikajana Vovemba 2w, 2024 katika mtaa wa Magomeni viwanja vya Soko Bati, Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Katika hotuba yake, Makamu Mwenyekiti wa CUF Tanzania Bara, Maftaha Nachuma, amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi na kuwachagua viongozi wa CUF ili kuweza kutekeleza mikakati ya haki sawa kwa wote na sera ya utajirisho.

Nachuma amesema kuwa sera ya utajirisho inakusudia kuwainua wananchi kiuchumi kwa kuwapa fursa ya kutumia rasilimali za taifa, kama vile gesi, na hivyo kuchochea maendeleo ya vijiji na vitongoji.

Aidha amesisitiza kuwa, wananchi wanapaswa kutoa kura ya ndio kwa wagombea wa CUF ili kusaidia kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya uchumi na maisha ya kila siku ya wananchi.


Kwa upande mwingine, Katibu wa CUF Mtwara Mjini, Saidi Kulaga, ameiomba taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mtwara kuchunguza na kutoa taarifa kuhusu tukio la aliyekuwa mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti Mtaa wa Tandika kupitia CUF, ambaye amehama chama hicho na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo Kulaga amesema kuwa mgombea huyo amekiuka kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa, ambazo zinataka mtu kujitoa kwa utaratibu maalum.

Aidha, Kulaga amewasihi wananchi kuendelea kupigania mabadiliko katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika Novemba 27, 2024.

Mwanachama wa CUF, Amina Liposwe, amewasihi wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi bora na kusisitiza kuwa mamlaka ya kusimamia uchaguzi inapaswa kutangaza matokeo kwa haki, bila upendeleo.