Wabunge 24 wa Chama cha Wananchi (CUF) wanaomuunga mkono aliyekuwa Katibu Mkuu wa chama hicho, Maalim Seif Shariff Hamad, ambaye amehamia Chama cha ACT – Wazalendo, wataendelea kushikilia ubunge wao hali inayoiweka CUF njia panda, JAMHURI limeelezwa.
Wabunge hao walijikuta katika mtihani wa kuchagua ama kuachana na ubunge wao wamfuate Maalim Seif ACT au wabaki CUF kulinda ubunge wao hadi mwakani, lakini wakiendelea kuishi katika mazingira magumu kisiasa ndani ya chama hicho.
Tayari Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alikwisha kuweka bayana nia ya kutaka wabunge hao kuendelea kuwamo ndani ya chama hicho ili washirikiane kukijenga chama chao.
Baada ya uamuzi wa mahakama kumtambua Lipumba dhidi ya Maalim Seif, Mwenyekiti huyo wa CUF alisema wabunge hao pamoja na viongozi wengine waandamizi waliokuwa wakimpinga yuko tayari kushirikiana nao “ili mradi tu waheshimu matakwa ya kikatiba ya chama chao.”
Mwezi Machi mwaka huu wakati Maalim Seif akitambulishwa kujiunga na ACT, aliweka bayana kuwa wabunge wanaomuunga mkono wanaweza kuchagua moja kati ya mawili, ama wajivue ubunge kumfuata au waendelee na ubunge, lakini wakitambua kuwa uamuzi huo utakuwa na madhara ya kisiasa siku za baadaye, hasa wakati wa kuchuja wagombea kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Lakini mwishoni mwa wiki, akizungumza na JAMHURI, Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT, Zitto Kabwe, ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Mjini, amesema ni jambo gumu kwa wabunge hao kujiondoa CUF kwa sasa, kwa kuwa waliaminiwa na wananchi moja kwa moja, na zaidi ya hapo, kujivua kwao ubunge kutaikosesha Pemba uwakilishi ndani ya Bunge la Jamhuri ya Muungano. Pemba kwa ujumla wake imekuwa na wabunge kutoka CUF baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, kwa hiyo kujiuzulu kwao kutawapora wananchi haki ya kuwakilishwa.
“CUF ndiyo iliyotwaa viti karibu vyote vya ubunge Pemba, kitendo cha wabunge hao kujiuzulu maana yake ni kwamba wananchi wa Pemba watakosa uwakilishi. Chama cha ACT – Wazalendo tunaelewa haki ya wananchi kuendelea kuwakilishwa bungeni, kwa hiyo ni busara zaidi kwa wabunge hao kuendelea na kazi yao ya uwakilishi ingawa chaguo ni lao kwa sasa,” amesema Zitto.
Ni zaidi ya mwezi mmoja sasa tangu Maalim Seif ajiunge na ACT, hatua ambayo ilisukumwa na mgogoro uliokuwapo kati yake na Mwenyekiti wa chama chake cha awali, Profesa Ibrahim Lipumba, kiasi cha kufikishana mahakamani huku viongozi wengine wa juu waandamizi kwenye chama hicho wakigawanyika katika mapande mawili, maarufu CUF – Maalim na CUF – Lipumba, ila hatimaye Seif akahamia ACT.
Hatua ya Seif kuhama CUF ilitanguliwa na uamuzi wa Mahakama Kuu kumpa ushindi wa uhalali wa kiuongozi Lipumba.
Maalim anatajwa kuwa mmoja wa wanasiasa wenye ushawishi mkubwa katika siasa za Zanzibar, akiwa amejiunga na ACT pamoja na baadhi ya wanasiasa waandamizi waliokuwa wakimuunga mkono CUF wakiwamo wabunge hao 24.
Kujiondoa kwa Maalim Seif CUF alikodumu kwa zaidi ya miongo minne kumeandika historia mpya katika medani za siasa visiwani Zanzibar, ikitarajiwa kuwa ACT ndicho kitakuwa chama chenye ushindani wa karibu na Chama Cha Mapinduzi (CCM) badala ya CUF kama ilivyokuwa awali.
Mara kwa mara katika Uchaguzi Mkuu uliopita, Maalim Seif amekuwa akilalamika kuporwa ushindi katika kinyang’anyiro cha urais wa Zanzibar huku akipata idadi ya kutosha ya wabunge na hata wajumbe wa Baraza la Wawakilishi. Hata hivyo, kwa sasa CUF haina wawakilishi ndani ya Baraza la Wawakilishi kutokana na kususia marudio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.
Katika tasnia ya siasa nchini, kumekuwa na mabadiliko kadhaa. Wakati Seif akijiunga na chama kingine cha upinzani, aliyekuwa mgombea urais wa kambi ya Upinzani chini ya ushirikiano wa kisiasa wa vyama vya siasa, maarufu kwa jina la UKAWA, Edward Lowassa, amerejea kwenye Chama chake cha zamani, CCM, akitokea Chama cha Demokrasia na Maendeleo ambako katika uchaguzi huo wa mwaka 2015 alikuwa mshindi wa pili katika kinyang’anyiro cha urais, akitanguliwa na Rais Dk. John Magufuli.
Hukumu iliyomchefua Maalim Seif hadi kuondoka CUF ilitolewa na Jaji Benhaji Masoud, wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, baada ya uamuzi wake wa kuidhinisha uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, kumtambua Lipumba kuwa Mwenyekiti halali wa CUF. Jaji Masoud pia alizitaka pande zinazovutana kukutana kwa ajili ya majadiliano ili kutatua tofauti zao.
Ni kesi ambayo kambi ya Maalim Seif walifungua mahakamani kupinga Msajili wa Vyama vya Siasa kumtambua Lipumba baada ya kujiuzulu na kurudi kwenye chama mwaka 2016.
Zitto: Tunamsubiri Lissu
Katika hatua nyingine, Zitto ameliambia gazeti hili kwamba chama chake kinasubiri kwa hamu kurejea nchini kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, ambaye amekuwa katika matibabu nje ya nchi kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa baada ya kushambuliwa kwa risasi na watu wasiojulikana Septemba 7, mwaka 2017.
Kauli hiyo ya Zitto inazingatia maelezo ya hivi karibuni ya Lissu kuwa wakati wowote kwa ruksa ya madaktari wake anaweza kurejea nchini.
“Tunamsubiri Lissu kwa hamu kubwa, mchango wake katika siasa za upinzani na taifa kwa ujumla ni wa umuhimu mkubwa. Kazi yake bungeni inahitajika zaidi katika kipindi hiki kigumu. Anahitajika bungeni na maeneo mengine katika taifa hili katika suala la kuimarisha utawala wa sheria,” amesema Zitto na kuongeza kuwa wanasiasa wazalendo wanahitaji kuunganisha zaidi maarifa yao kwa sasa ili kuimarisha haki nchini.
Lissu aliyewahi kuwa Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) amekuwa katika misukosuko na uongozi wa Bunge ambao miezi kadhaa nyuma ulitangaza kusimamisha malipo ya mshahara wake huku mbunge huyo akiapa kupigania haki yake hiyo kupitia kwa mawakili wake ambao aliwataka kufungua kesi mahakamani. Hata hivyo, taarifa zilizopo zinabainisha kuwa Lissu amekwisha kulipwa mishahara yake iliyosimamishwa, taarifa ambazo amekwisha kuzithibitisha yeye mwenyewe.
Akizungumzia hatua ya hivi karibuni ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuwataka ACT – Wazalendo wajieleze kwa nini chama hicho kisifutwe kwa kukiuka kile kilichotajwa kuwa masharti ya usajili, Zitto amesema licha ya kuwasilisha utetezi wao kwa Msajili ndani ya muda kama ilivyoelekezwa, bado hakuna majibu waliyokwisha kupata.
Hata hivyo, gazeti hili limeelezwa na vyanzo vyake kadhaa vya habari kuwa bado Msajili wa Vyama anaendelea kutafakari hatua za kuchukua kwa kuzingatia uzito wa maelezo ya utetezi ya ACT – Wazalendo, ingawa vyanzo hivyo vya habari vimebainisha kuwa huenda hatua ya kukifuta chama hicho isichukuliwe.
Kwa upande wake, JAMHURI limemtafuta Jaji Mutungi kujua atafikia uamuzi gani juu ya nia ya kuifuta ACT, lakini hakupatikana: “Kaka hili swali hapa ofisini halijibiki. Nakuhakikishia utakuja hapa hata mara 10, lakini hautapata jibu. Hata secretary (katibu muhtasi) sidhani kama utaonana naye. Hili ni kaa la moto hapa ofisini,” amesema ofisa aliyekutwa ofisi za Msajiili wiki iliyopita.