Na Mwandishi Wetu, JakhuriMedia, Dar es Salaam
MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, shule Kuu ya Biashara (UDBS), Patrolik Kanje, ameshauri utitiri wa tozo za mamlaka ya udhibiti zipunguzwe ili kuwapunguzia mzigo wazalishaji wa bidhaa nchini.
Alitoa ushauri huo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wanachama wa Shirikisho la Wenye Viwanda nchini (CTI).
Alikuwa akiwasilisha matokeo ya utafiti alioufanya kuhusu matatizo ya kisera na ya kikodi yanayozikumba sekta za mazao ya chakula, mazao ya pamba na nguo na kwenye dawa na vifaa tiba.
Alisema utafiti huo aliufanya kwenye mikoa mbalimbali kwa kuangalia wenye viwanda na kubaini kuwa gharama za kodi na ada mbalimbali ni kubwa kutokana na kwamba mamlaka za usimamizi nyingi zinachukua tozo kwa wazalishaji kwa kitu kile kile.
“Mfano unakuta mchakataji wa maziwa inabidi awe na leseni ya biashara kwenye halmshauri ambayo anafanyia kazi lakini pia anatakiwa apate leseni kwa msimamizi wa sekta ya maziwa ambayo ni bodi ya maziwa sasa hii inaongeza gharama za uzalishaji kwasababu mtu anaacha kazi zake anafuatilia leseni na anafuatilia kwa huyu na yule,” alisema
“Tunajua kwamba sheria, sera na miongozo mbalimbali inawekwa na serikali ili kuhakikisha mambo yanakwenda vizuri lakini utekelezaji wake umekuwa na ukakasi kidogo ndiyo maana tunashauri kwamba kusiwe na utitiri wa mamlaka za udhibiti kwenye kitu kile kile,” alisema
“Mfano mtu akifanya tathmini ya athari kwa mazingira ya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC, wengine wakija watumie ile iliyofanywa na NEMC kwasababu bila kufanya hivyo tutampotezea muda mwingi mzalishaji kwa mambo ambayo yameshafanyika,” alisema
Alisema licha ya kumpotezea muda mwingi mzalishaji kufanyiwa kaguzi za mara kwa mara pia zimekuwa zikiwaongezea gharama kwani kila wanapofanya tathmini ya athari kwa mazingira wanalazimika kulipa gharama kwa mamlaka husika au kwa mkandarasi mshauri anayemfanyia kazi.
“Kwa hiyo unakuta ni kitu kile kile ila kinalipwa kwa mamlaka zaidi ya moja kwa mfano kwenye suala la afya kwa wafanyakazi OSHA ndiye anasimamia, akija kwako atakukagua na utalipia cheti lakini bibi afya wa Manispaa atakuja naye atasema wafanyakazi wapimwe afya na akupe cheti sasa muda wa kupima wafanyakazi unapotea na analipa tena gharama,” alisema na kuongeza
“Hali hii inasababisha gharama za uzalishaji kupanda na bidhaa kushindwa kushindana na zile zinazotoka nje ambazo wakati mwingine zinakuwa nafuu na matokeo yake unakuta viwanda vyetu viunashindwa kushindana na vinafungwa,” alisema
Mtaalamu wa Sera ya Viwanda wa Shirikisho la Wenye Viwanda CTI, Isack Msungu alisema utafiti huo ulifadhiliwa na Shirikisho la Viwanda la Denmark (DI) kuangalia sekta ya pamba, dawa na vifaa tiba na vyakula ambavyo hazijafanya vizuri kama zinavyotakiwa kufanya na nini kifanyike ili kuziwezesha kufanya vizuri.
“Utafiti umeshafanyika na hapa tunawasilisha kwa wadau wetu yaliyotokana na utafiti huo kuangalia namna ya kuishauri serikali na kuishawishi kuchukua haya mapendekezo kwaajili ya utekelezaji ili kuziwezesha sekta hii ifanye vizuri zaidi,” alisema.
Alisema utafiti umebainisha changamoto za kila sekta na kikubwa ni urasimu wa taasisi nyingi kusimamia na kutoza tozo mbalimbali kwa masuala yanayofanana hali ambayo inawabebesha mzigo wazalishaji na kuwapotea muda wao wa kazi.