Thamani ya uwekezaji wa Shirika la Catholic Relief Services (CRS) Tanzania, itaongezeka hadi kufikia dola za Kimarekani milioni 17 mwaka kesho.

Kiasi hicho kitaliwezesha shirika hilo kuboresha huduma tofauti kwa watu wasiojiweza na wanaokabiliwa na majanga mbalimbali nchini.


Mwakilishi wa CRS Tanzania, Conor Walsh, aliyasema hayo katika sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya shirika hilo, yaliyofanyika Mikocheni jijini Dar es Salaam, wiki iliyopita.

 

“Mwaka 2013 shirika litaelekeza nguvu kubwa kwenye miradi ya afya, hasa kuhusu kinga na matibabu ya Ukimwi na kifua kikuu,” alisema Walsh na kuongeza: “Pia tutaongeza nguvu katika utoaji wa misaada ya mahitaji muhimu kwa watu wasiojiweza, hususan watoto yatima na kaya zilizoathiriwa na virusi vya Ukimwi, huduma za maji, usimamizi wa rasilimali na kilimo.”


Alisema lengo la shirika hilo siku zote ni kushikamana na Watanzania, kufanya kazi na Kanisa Katoliki, Serikali, mashirika mengine ya kiimani, asasi za kiraia na jamii kwa jumla kuwaongezea watu uwezo wa kujihudumia.


“Jukumu letu ni kuwezesha mabadiliko ya kupunguza umaskini katika jamii ya Watanzania, tunatoa msaada wa kitaalamu na uwezo wa kimaendeleo,” alisisitiza Mwakilishi huyo wa CRS Tanzania.


Alitaja miradi ya hivi karibuni inayohamasishwa kuwa ni kilimo cha maharage ya soya na masoko yake, ambapo shirika hilo linawaunganisha wakulima kwenye masoko ya ndani.


“CRS inafanya kazi na wakulima, tunawafundisha stadi za kazi kama vile utunzaji wa taarifa, usimamizi bora, ununuzi wa jumla na kufanya makubaliano ya bei na wanunuzi wa mazao,” alisema.


Walsh alitumia nafasi hiyo pia kuipongeza Serikali, Kanisa, wafadhili wa CRS na Watanzania wanaosaidia kufanikisha shughuli za shirika hilo.


Kwa upande wake, Rais na Ofisa Mtendaji Mkuu wa CRS Kimataifa, Carolyn Woo, alisema matumizi ya fedha za shirika hilo hufanyika kwa uwazi na usimamizi usiotoa mwanya wa hujuma yoyote. “Kiwango cha matumizi mabaya ya fedha za CRS ni sifuri,” alisema Woo.

 

CRS ni shirika la kimataifa la jamii ya Wakatoliki katika Umoja wa Mataifa, linalopunguza matatizo kwa kutoa misaada kwa watu wanaohitaji katika karibu nchi 100 duniani. Hadi sasa, CRS inafanya kazi katika mikoa 10 nchini katika za Ziwa, Kaskazini Mashariki, Kati na Kusini Magharibi, ikiwa imeajiri wafanyakazi 100 na kufungua ofisi katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha na Mwanza.


Likiwa na kaulimbiu ya Mshikamano Daina, shirika la CRS lilianzishwa nchini mwaka 1962 wakati wa ukame mkali ulioikabilia jamii ya wafugaji wa Kimaasai mkoani Arusha, ambapo uliwapatia watu 85,000 misaada ya kibinadamu ikiwamo ya chakula na kuanzisha miradi ya maendeleo ya uchumi.


Shirika hilo liliweza kusaidia pia miradi ya huduma za kibinadamu kwa wakimbizi kutoka nchi za Rwanda na Burundi, katika kambi ya magharibi mwa Tanzania.

 

Viongozi wengine waliohudhuria sherehe za maadhimisho ya miaka 50 ya CRS Tanzania ni maaskofu John Ricard na Franke Dewane kutoka Florida, Askofu John Wester kutoka Utah na Mjumbe wa Bodi ya shirika hilo, Askofu Kevin Boland kutoka Savannah, Umoja wa Mataifa.