Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KATIKA kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Benki ya CRDB imezindua huduma mpya iitwayo ‘Elle’ ambayo ni huduma ya wateja wa kidijitali saa 24.

Uzinduzi wa huduma hiyo umefanyika leo Oktoba 7, 2024 katika Makao Makuu ya Benki hiyo jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na zaidi ya wateja 200.

Akitambulisha huduma hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema inalenga kutoa usaidizi kwa wateja kwa njia ya mawasiliano ya ujumbe ‘Chatbot’ na ufanyaji miamala.

Amesema kupitia huduma hiyo mpya, wateja wa Benki ya CRDB wanaweza kupata msaada wa kibenki kwa haraka na kwa urahisi kupitia WhatsApp au kwenye tovuti ya Benki ya CRDB.

“Katika kuendelea kuboresha huduma zetu, Benki ya CRDB tumeamua kuja na huduma hii mpya inayotumia teknolojia ya akili mnemba (AI), iliyopewa jina la ‘Elle,’ ikiwa ni kifupisho cha ‘Ellephant’, inayowakilisha chapa ya Benki yetu…ambapo sasa wateja wetu wataweza kupata msaada wa haraka.

“Tunaimani kupitia Elle hakutakuwa na ucheleweshaji wa huduma kwa wateja wetu kwani mteja anapata majibu mepesi na magumu kwa haraka, na yale ambayo hajapata majibu yanapelekwa haraka kwa muhusika ili apate majibu. Tunaimani hakutakuwa na utoaji huduma na ucheleweshaji kwani CRDB tumejipanga kuhakikisha huduma zetu zinakuwa bora zaidi,” amesema.

Aidha Nsekela amewahakikishia wateja kuwa benki hiyo itaendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika teknolojia, ubunifu wa huduma na bidhaa, pamoja na mafunzo kwa wafanyakazi ili kuhakikisha huduma zinazotolewa ni bora na za kiwango cha juu.

Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja wa Benki ya CRDB, Yolanda Uriyo, amesema kuwa benki hiyo inaendelea kuimarisha mifumo yake ya kidijitali na kuwekeza zaidi kwenye mbinu za kisasa za kupokea maoni ya wateja kupitia mifumo kama QR-Code na USSD.

“Huduma bora kwa wateja kwetu ni ajenda ya kila siku na Elle ni sehemu ya mikakati ya Benki ya CRDB ya kutoa huduma za kibenki zinazoendana na mabadiliko ya teknolojia duniani.

“Kupata usaidizi au huduma kupitia Elle mteja anatakiwa kutembelea tovuti rasmi ya Benki ya CRDB (www.crdbbank.co.tz) au kuwasiliana kupitia WhatsApp namba (+255) 0714197700. Kupitia WhatsApp, Elle atasidia wateja kufanya miamala kwa urahisi ikiwamo kutuma fedha, kuangalia salio, kulipia ankara, kuangalia taarifa ya akaunti, pamoja na huduma nyingine nyingi. Mteja pia anaweza kuzungumza na ‘Elle’ kuhusu mambo mengine nje ya benki, jambo linalomfanya kuwa rafiki zaidi wa wateja,” ameongezea Yolanda.

Akielezea kuhusu maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja, Yolanda amebainisha kuwa katika mwezi huu wa Oktoba, Benki ya CRDB itafanya shughuli mbalimbali ikiwamo kuwasikiliza wateja wake na kufanyia kazi maoni yao, sambamba na kuendelea kusherehekea mafanikio katika kuboresha huduma kwa wateja.

Ahmed Zahoro, moja ya wateja wa Benki ya CRDB waliopata kushuhudia uzinduzi wa huduma hiyo ameipongeza benki hiyo kwa kuendeleza kuwekeza katika ubunifu kwa ajili ya kutoa huduma bora kwa wateja. “Tunaishukuru Benki yetu kwa kutujali. Elle itasaidia kutupa urahisi na unafuu wa kupata huduma na usaidizi kwa wakati,” aliongeza.

Wiki ya Huduma kwa Wateja mwaka huu inaadhimishwa kwa kaulimbiu ya ‘Above and Beyond’ ambayo inaendana na falsafa ya Benki ya CRDB ya kuhakikisha huduma zao zinakidhi na kuzidi matarajio ya wateja.

Benki ya CRDB inatambulika ndani na nje ya kama Benki kinara katika Huduma kwa Wateja nchini ambapo hivi karibuni Benki hiyo imetunukiwa Tuzo ya Ubora wa Huduma na Taasisi ya Utafiti wa Ubora barani Ulaya (European Society for Quality Research). Kuzinduliwa kwa Elle kunaendelea kuiweka Benki ya CRDB katika ramani ya Benki kinara katika huduma bora katika ukanda huu wa Afrika ya Mashariki na Kati.

Please follow and like us:
Pin Share