Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

KATIKA kuhakikisha inawainua wanawake kiuchumi, Benki ya CRDB imeendelea kuwawezesha kwa kufungua akaunti ya Malkia ambayo itakuwa ni yenye malengo yakinifu na manufaa kwa maendeleo kwa wanawake.

Akizungumza katika banda lao lililopo katika maonesho ya 48 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF) maarufu kama Sabasaba, Afisa Uhusiano wa CRDB Tawi la Temeke, Dorah Woisso, amesema pamoja na kutoa huduma za kifedha pia wanatoa elimu kwa wanawake jinsi ya kujiunga na akaunti hiyo ya Malkia.

“CRDB tumeshiriki katika maonesho ya Sabasaba tumeleta huduma mbalimbali kwa wateja wetu ikiwemo akaunti ya Malkia ambayo ni maalum kwa wanawake.

“Akaunti hii ni akaunti ya malengo ambapo mtu ataweka pesa kwa muda wa mwaka mmoja na kuendelea bila kutoa na faida za akaunti hii mteja atapata faida kila mwezi kulingana na kiasi kilichopo kwenye akaunti na pia haina makato yoyote kwa mwezi haina gharama za uendeshaji na mteja atakapokuja kufungua atahitaji kuwa na sh. 5000 tu,” amesema Dora.

Ametaja faida nyingine ambayo mteja ataipata ni kuweza kukopa kupitia akaunti hiyo hadi asilimia 90 ya kiasi ambacho kipo kwenye akaunti yake.

“Katika kutoa mkopo huo, hatutahitaji dhamana nyingine yoyote ya tofauti na akaunti yake ya Malkia,” amesema.

Pia ametaja akaunti nyingine inaitwa Dhahabu ambayo imewalenga watu wote huku yenyewe ikiwa ya malengo ya muda mrefu.

“Hii ipo tofauti kidogo na akaunti ya Malkia kwani malengo yake ni miaka mitatu na kuendelea. Lakini pia haina gharama za uendeshaji. Na mteja atakuwa anaweka fedha kila mwezi ili kuweza kufikia malengo yake ya muda mrefu na yenyew pia ina faida ya kupata riba Kila mwezi pamoja na kukopa asilimia 90 ya kiasi kilichopo.

“Tunawakaribisha wananchi wote kutembelea katika matawi yetu ya CRDB kuja kufungua akaunti, unahitaji kuja na kitambulisho cha Taifa(Nida), leseni au pasipoti ya kusafiria,” amesema