Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Tanga

KATIKA muendelezo wa kusheherekea miaka ya 30 ya uwepo wa Benki ya CRDB ambao umeleta mabadiliko chanya katika jamii, Benki ya CRDB imekabidhi madarasa mawili pamoja na vyoo sita katika Shule ya Msingi Misufini iliyopo Kata ya Magoroto Wilaya ya Muheza mkoani Tanga. Madarasa hayo pamoja na vyoo yamekabidhiwa kwa niaba ya Benki ya CRDB na Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi, Miranda Mpogolo kwa Mbunge wa jimbo la Muheza ambae pia ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinjuma.

Akizungumza katika makabidhiano hayo, Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Miranda Mpogolo alisema kuwa katika miaka 30 ya uwepo wa benki hiyo imeendelea na jitihada zake za kuwekeza kwenye jamii inayoizunguka kwa kuamini kuwa ustawi wa jamii ndiyo ustawi wa benki ambapo kila mwaka benki hutenga asilimia moja ya faida yake kuwekeza katika jamii.

“Benki ya CRDB ni benki ya kizalendo ambayo inajivunia kuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya jamii ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali pamoja na wadau mbalimbali katika kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili jamii kupitia sera yake ya kuwekeza kwenye jamii ambayo imejikita katika maeneo ya elimu, afya, mazingira pamoja na uwezeshaji kwa vijana na wanawake ” alisema Miranda.

Miranda amesema kwa mwaka jana pekee Benki ya CRDB ilitumia zaidi ya Shilingi Bilioni 2.31 katika miradi ya kijamii huku zaidi ya Shilingi Bilioni 1 sawa na asilimia 44 zikielekezwa katika sekta ya elimu kupitia program ya makhususi ya “Keti Jifunze” ambayo imejikita maeneo ya ujenzi wa madarasa, mabweni, vyoo, ofisi za walimu, maabara, ununuzi wa madawati, viti, meza, kompyuta pamoja na vifaa vingine vya kufundishia ili kuweka mazingira mazuri ya kujifunzia.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Muheza ambae pia ni Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamisi Mwinjuma ameishukuru Benki ya CRDB kwa uwekezaji huo ambao unakwenda kuwapa ahueni wanafunzi wa Kata ya Magoroto ambao walikua wanatembea zaidi ya Kilomita Tano hadi Sita kwa siku kufika shuleni huku wakishindwa kabisa kufika shuleni kipindi cha masika.

“Wazo la kujenga shule hii lilikuja wakati wa kampeni za kugombea ubunge mwaka 2020 ambapo niliweza kujionea changamoto za wanafunzi wanaoishi kata hii na kujiapiza kuwa ntafanya kila lililo ndani ya uwezo wangu kuhakikisha kuwa tunajenga shule hii na nashukuru leo kupitia Benki ya CRDB na wadau wengine wa maendeleo tunakwenda kutimiza kile nilichomuahidi Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan siku chache zilizopita kuwa shule hii itakwenda kukamilika bila kuomba fedha zozote kutoka Serikalini” alisema Mhe. Mwinjuma.

Kupitia katika risala yao, wanafunzi wanaotarajia kuhamia katika shule hiyo, wameishukuru Benki ya CRDB kwa kuweza kufanikisha ujenzi wa madarasa na vyoo katika shule hiyo na kuahidi kuwa watatumia fursa hiyo kusoma kwa bidi ili waweze kutoa mchango katika maendeleo ya Taifa kwa ujumla.