DAR ES SALAAM
Na Mwandishi Wetu
Benki ya CRDB imeendelea kupiga hatua kubwa za kupigiwa mfano katika sekta ya fedha nchini, na sasa inatoa huduma katika maeneo yaliyodhaniwa kuwa yanazifaa nchi za Ulaya pekee.
Ukiacha kushusha riba, kujenga jengo kubwa, la kisasa lenye thamani ya Sh bilioni 163, CRDB imevuka mipaka ya Tanzania na sasa ipo Burundi, ikiwa mbioni kufungua tawi jijini Lubumbashi, katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Aidha, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania na Mkurugenzi Mkuu, Prof. Florens Luoga na Ofisa Mtendaji Mkuu wa CRDB, Abdulmajid M. Nsekela, wameitangazia dunia wiki iliyopita kuwa mbali na Burundi na DRC, CRDB si muda mrefu itakwenda katika nchi nyingine tano kutoa huduma za kibenki.
Si kwamba CRBD inalenga masoko ya kimataifa pekee, bali hata hapa nchini benki hii iko karibu na wananchi kwa kiwango cha kutoa mafao ya gharama za mazishi na mkono wa pole wa kati ya Sh milioni mbili hadi Sh milioni 15 kwa wateja wake wa ndani na nje ya nchi pindi wanapofariki dunia au kupata ajali.
Huduma hiyo ya mkono wa pole inayojulikana kwa jina la ‘Bima ya Kava’ imeendelea kutolewa tangu ilipozinduliwa mwishoni mwa mwaka juzi.
Wakati wa uzinduzi wa huduma hiyo, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni Tanzu ya Bima ya CRDB, Wilson Mnzava, alisema waliangalia soko na kubaini kuwa kuna uhitaji ndipo wakaamua kutengeneza Bima ya Kava.
“Bima ya Kava ni huduma ya bima inayotolewa bure kwa wateja wa CRDB wenye akaunti binafsi ambayo itakuwa hai (active account). Kupitia bima hii, benki inatoa mkono wa pole pale mteja anapofariki dunia au kufiwa na mwenza wake au kupata ulemavu wa kudumu,” amesema.
Mnzava amesema mnufaika wa bima hiyo ni mteja mwenye akaunti ya kawaida, wa daraja la juu (Premier) na anayeishi nje ya nchi (diaspora).
“Tuliona wateja wetu wanahitaji kitu cha ziada zaidi pia diaspora wana changamoto hasa pale mwenzao mmoja anapofariki dunia. Kisha tukaangalia mtu akifungua akaunti CRDB anapata nini tofauti ili kumtofautisha na benki nyingine.
“Ndipo timu ya kitengo cha bima cha CRDB ilikaa chini na kutengeneza bidhaa tutakayoiongezea thamani katika akaunti ya mteja wetu,” amesema.
Mnzava amesema huduma hiyo inafanya kazi pindi ikitokea mteja mwenye akaunti CRDB akafariki dunia ndipo benki itatoa mkono wa pole wa Sh milioni mbili na kwa wateja maalumu (premier) itatoa Sh milioni tano na wale wenye akaunti ya Tanzanite wanaoishi nje ya nchi nao watapewa Sh milioni tano.
Vilevile amesema benki hiyo itagharamia safari ya kuutoa mwili kutoka kwenye nchi aliyofia mteja mwenye akaunti ya Tanzanite kuja Tanzania kwa gharama isiyozidi Sh milioni 15.
“Endapo mteja na mwenza wake watafariki dunia, CRDB itatoa mkono wa pole wa Sh milioni nne kwa mteja wa kawaida na Sh milioni 10 kwa mteja wa daraja la juu au mteja anayeishi nje ya nchi. Mkono wa pole ni nyongeza ya faida/huduma ya kusafirisha mwili wa marehemu kutoka nje ya nchi alikokuwa anaishi. Kiasi hiki ni pamoja na tiketi ya kurudi kwa mwanafamilia anayeleta mwili,” amesema na kuongeza:
“Ni rahisi kuwa na Bima ya Kava. Kinachotakiwa ni kufungua akaunti ya CRDB kisha utaanza kufurahia hayo mafao. Wale wanaopata Sh milioni mbili kama amepata ajali na kupata ulemavu wa kudumu tunatoa pia mkono wa pole wa Sh milioni mbili.
“Kuna wale wenye familia; ameoa au ameolewa, ile Sh milioni 2 inakuwa extended kwa mke au mume, wenye Akaunti ya Premier tunaongeza tena Sh milioni tano kwa mke au mume.”
Pia amesema endapo mteja na mwenza wake watafariki dunia nje ya nchi, CRDB itatoa hadi Sh milioni 30 kurejesha miili ikiwa ni nyongeza ya mkono wa pole kwa wateja hao.
Mnzava amesema kinachotakiwa katika mchakato wa kupata mafao hayo ni kwa mteja kwenda katika tawi lililo karibu akiwa na kibali cha mazishi na vitambulisho, kisha atajaza fomu na kuambatanisha uthibitisho na atalipwa mafao yake ndani ya saa 72.
“Huna haja ya kufunga safari kuja makao makuu au kwenda nje ya mkoa mwingine, nenda katika tawi lililo karibu. Kutoa taarifa tangu janga lilipotokea isizidi miezi sita na kuleta viambatanisho vyote isizidi miezi tisa.
“Kitu tunachokiangalia ni kuwa na mteja wakati wa nyakati ngumu, kwa hiyo hii huduma inakuja kumfariji mteja na tunataka ifike mahali wananchi wajue kabisa kwamba CRDB ipo na itasaidia kutoa rambirambi,” amesema.
Kuhusu Bima ya Kava ya ulemavu wa kudumu amesema huduma hiyo inawahusu wateja wa kawaida na ikitokea mteja amepata ulemavu huo uliotokana na ajali, CRDB itatoa Sh milioni mbili.
Majid akizungumzia jengo lililozinduliwa na Rais Samia wiki iliyopita, amesema lina kumbi 60 na ukumbi mkubwa una uwezo wa kuchukua watu 200. Mteja wa CRDB ikiwa ana mkutano wa kibiashara, amesema anapewa ukumbi wa mkutano bure katika jengo hilo.
Jengo hili la kisasa, ghorofa ya kwanza imetengwa mahususi kwa ajili ya kuweka makumbusho ya CRDB na sekta ya fedha na kwamba itatumika kutoa mafunzo kwa wanavyuo juu ya historia na mfumo wa fedha nchini.
Mkurugenzi Mkuu amesema CRDB ina matawi 265 nchi nzima na mawakala 22,000 hali inayowafanya kuwa benki kiongozi. Amesema CRDB inaongoza nchini kwa kukopesha wastani wa Sh trilioni 5.1 kwa mwaka wa fedha uliopita, na sasa wanawalenga wafanyabiashara wadogo na wamachinga kwa vigezo vinavyomwezesha kila mkopaji kupata mkopo anaoutaka.
Katika Sekta ya Kilimo, Mkurugenzi Mkuu Majid amesema CRDB wameshusha riba hadi asilimia 9, huku mikopo ya wafanyakazi wote kwenye sekta binafsi na serikalini riba ikishuka kutoka wastani wa asilimia 18 hadi 13. Kwa Zanzibar, amesema CRDB chini ya mpango maalumu inawakopesha wajasiriamali bila riba. Mikopo kwa vikundi vya wanawake imeshushwa riba kutoka asilimia 20 hadi 14.
Majid amesema CRDB inashiriki kwa vitendo ndoto ya Rais Samia Suluhu Hassan kuifungua nchini, ambapo wanachangia kupatikana kwa mikopo katika ujenzi wa miradi ya kimkakati. Hadi sasa katika reli ya SGR – CRDB imechangia upatikanaji wa mkopo wa wastani wa dola milioni 104 (Sh bilioni 240), dola milioni 200 (Sh bilioni 500) katika Bwawa la Nyerere, dola milioni 40 (Sh bilioni 100) katika ujenzi wa Uwanja wa Ndege Terminal Three na dola milioni 60 (Sh bilioni 150) katika mradi unaosimamiwa na Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Pia CRDB ina mradi wa mabadiliko ya hali ya hewa ambapo imepokea dola milioni 100 (Sh bilioni 240) kutoka Shirika la Mabadiliko ya Hali ya Hewa Duniani (GCF) na CRDB imechangia kiasi sawa na hicho, yaani dola milioni 100 sawa na Sh bilioni 240.
Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, amesema CRDB ni benki kiongozi hapa nchini. Amewataka Watanzania kuitumia benki hiyo kuhifadhi fedha zao, kuheshimu mikopo na taasisi za fedha kuhesibu mali za wateja badala ya kuziuza kwa tamaa.
Rais Samia Suluhu Hassan amesema CRDB ni moja kati ya walipa kodi wakubwa hapa nchin, na amewataka waendelea kurahisisha masharti ya kibenki, huku akiwataka watupie jicho la kipekee kwa wamachinga kwa kuwapa mikopo isiyo na masharti magumu.
“Naomba muwaangalie kwa jicho la pekee na kuwapa kipaumbele Bodaboda, Mama Ntilie na wanangu Wamachinga,” amesema Rais Samia.
Amewataka CRDB kuwezesha sekta isiyo rasmi kutunza hesabu na kukua kifedha, akisema mbali na kupata fedha hizo ni walipa kodi watarajiwa wakiishapata uwezo mkubwa wa kifedha.