Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dodoma

MKURUGENZI Mkuu wa Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), CPA Anthony Kasore ametoa wito kwa vijana na Watanzania kwa ujumla kutumia vyuo vyao ili kuweza kujiajiri.

Aidha amesema kuwa wamejipanga kuhakikisha wakulima nchini wanalima Kilimo chenye tija kutokana na teknolojia mbalimbali zilizobuniwa na Mamlaka hiyo.

CPA Kasore ameyasema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari katika Banda lao lililopo kwenye Maonesho ya Kitaifa ya Wakulima na Wafugaji (Nanenane) yanayoendelea katika Viwanja vya Nzuguni jijini Dodoma.

“Katika maonesho haya, VETA imekuja na teknolojia ambazo zitafanya Kilimo nchini kukua kutokana kwa kupata mashine za gharama nafuu kupatikana. Kama mnavyofahamu mpaka sasa vyuo 80 vimeshajengwa katika Mikoa na Wilaya mbalimbali nchini huku vyuo 65 vipya vinajengwa katika Wilaya na kufanya kila Wilaya kuwa na Chuo cha Ufundi Stadi,” amesema.

Akizungumzia kuhusu maonesho ya Nanenane amesema kuwa katika maonesho hayo wamekuja na mashine ya kutengeneza udongo kwa ajili ya kuoteshea mazao ya bustani ambapo udongo wa kuoteshea ulikuwa unatoka nje ya nchi kwa gharama kubwa ukilinganisha na mashine iliyopo VETA ya gharama nafuu.

Kasore amesema kuwa VETA imegusa fani katika kila Chuo kuendana na mazingira yake lengo ikiwa ni kufanya mhitimu kutafuta soko lake bila kukabiliwa na changamoto.