Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
TUME ya Taifa ya Sayansi,Teknolojia na Ubunifu(COSTECH)imetenga milioni 600 kwa ajili ya kutekelezwa miradi minne ya usalama wa chakula,ikihusisha udhibiti wa magonjwa ya mazao,uboreshaji wa uhifadhi wa chakula na ubunifu wa vyakula vyenye virutubishi vya hali ya juu.
Hayo yamesemwa leo Machi 17,2025 Dodoma na Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH Dkt.Amos Nungu,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Tume hiyo .

Amesema kuwa kwa kuwekeza shilingi bilioni 2.3 kupitia Samia Commercialization Fund,serikali imewapa wabunifu wa Kitanzania fursa ya kuingiza bunifu zao sokoni, hii inasaidia kuondoa changamoto ya kukosekana na dhamana ili kupata mitaji.
Dkt.Nungu amesema kuwa COSTECH imeanzisha na kuziwezesha kongano nane bunifu katika mikoa ya Kigoma, Geita, Mafia, Mbeya, Dodoma, Morogoro, Singida na Pemba ili kusaidia sekta ya viwanda na kilimo.

“Miradi hii imewezeshwa kwa ufadhili wa shilingi milioni 750, kuhakikisha teknolojia bora zinatumika katika kuboresha uzalishaji wa mafuta ya mawese, dhahabu na mazao ya baharini, ” ameeleza.
Licha ya hayo amesema Serikali ya awamu sita imetoa fedha na kuweka mazingira rafiki kwa wanasayansi na wabunifu wa Kitanzania ambapo kupitia mfumo wa ushirikiano wa kimkakati kati ya serikali ya Tanzania na nchi rafiki pamoja na taasisi za kimataifa, COSTECH imepokea shilingi bilioni 5.65 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya utafiti wa pamoja kati ya watafiti wa Tanzania na washirika wetu.
