Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Ofisi ya Hakimiliki Tanzania (COSOTA)
imesema imeandaa mgao wa mapato ya mirabaha kutokana na fedha za tozo ya Hatimiliki unategemewa kunufaisha makundi ya kazi za muziki, filamu, maandishi, sanaa za ufundi na sanaa za maonesho Kila daraja litapata kiwango sawa na madaraja mengine.

Hayo yamwelezwa leo March 21,2025 Jijini Dodoma na wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mwelekeo wa Ofisi hiyo kwa kipindi cha Miaka minne ambapo amesema jumla ya kiasi cha Tsh. 508,791,356.56 kitagawiwa kwa wasanii ambacho ni sawa na asilimia sitini (60%) ya tozo ya hakimiliki, na kiasi cha Tsh. 84,798,559.43 (asilimia 10) kinaenda Mfuko wa Sanaa na Utamaduni ambapo fedha hizo pia ni kwa ajili ya wasanii.

Amesema wasanii na waandishi watanufaika na jumla ya kiasi cha Tsh. 593,589,915.98 zilizokusanywa kwa kipindi cha mwaka 2023/2024.

“Gawio la Serikali ni 142,810,524.14 na gharama ya uendeshaji COSOTA ni 285,621,048.29,muundo wa COSOTA kwa sasa unaruhusu uanzishwaji wa Makampuni ya Wasanii ya kukusanya na kugawa mirabaha (Collective Management Organization – CMO) na COSOTA kubaki kama msimamizi wa masuala ya hakimiliki na kusimamia Kampuni hizo,”ameeleza.

Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa marekebisho ya Sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki ya mwaka 2022 yalipelekea kuandaliwa kwa Kanuni ya Kuanzishwa kwa Makampuni ya kukusanya na kugawa Mirabaha na kuruhusu uanzishwaji wa Makampuni kwa ajili ya kusimamia haki mbalimbali za aina za kazi za Sanaa na Uandishi .

Ameeleza kuwa katika kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu sita COSOTA imetoa jumla ya vyeti 7,679 vya uthibitisho wa umiliki wa hakimiliki kwa wabunifu waliosajili kazi zao.

“Kwa mwaka 2021 – 2025 COSOTA imefanikiwa kufanya migao miwili kama alivyoahidi Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan alipolihutubia bunge mwaka 2021 ambapo alisisitiza katika kipindi cha uongozi wake, serikali itahakikisha wabunifu wote wananufaika zaidi na kazi zao, “amesema

Akifafanua zaidi kuhusu mgao huo amesema Mgao wa kwanza ambao ulikuwa ni mgao wa ishirini na tatu ulifanyika tarehe 28/01/2022 na ulikuwa wa kiasi cha Tshs. 312,290,259,000, ambapo Wasani 1,123 walinufaika, na ulitokana na matumizi ya kazi 5,924 za muziki ambazo zilitumika katika vituo 11 vya redio, ikiwemo redio katika ngazi ya kitaifa, Mkoa, wilaya, kijamii na za kidini.

Amesema Mgao wa pili katika kipindi cha serikali ya awamu ya sita ulifanyika tarehe 21/07/2023 na ulikuwa ni mgao wa ishirini na nne wa mirabaha kwa kazi za muziki na COSOTA iligawa kiasi cha Tshs. 396,947,743.20 na wasanii wa muziki 8,165 walinufaika kupitia kazi zao 61,490.

“Hivi ni viwango vikubwa zaidi kuwahi kufanyika katika migao ya mirabaha ambayo COSOTA imekuwa ikigawa kwa miaka ya nyuma kabla ya uongozi huu wa serikali ya awamu ya sita ambao ulianzisha kampeni ya kusisitiza watumiaji wa kazi za Sanaa katika maeneo ya biashara kulipia matumizi ya kazi hizo,”amesema.

Pamoja na hayo ameeleza kuwa uongozi wa Dkt. Samia umefanya mageuzi makubwa ya kibajeti kwa COSOTA kwa lengo la kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Ofisi kwa kutoa fedha za serikali kiasi cha Tshs. 1.5 bilioni na Fedha hizo zimesaidia kuboresha usimamizi wa hakimiliki nchini, ununuzi wa vitendea kazi na utoaji elimu ya hakimiliki pamoja na ujenzi wa mfumo wa usajili.

Pamoja na mambo mengine ameeleza kuwa kwa kipindi cha miaka minne ya serikali ya awamu ya sita COSOTA imefanikiwa kupokea jumla ya migogoro 136 na kusuluhisha migogoro 118 ambapo migogoro 10 kati ya hiyo haikumalizika na ilifunguliwa kesi mahakamani na migogoro 8 inaendelea COSOTA.

Sambamba na migogoro hii, COSOTA imehusika na kesi za hakimiliki 10 ambapo katika kipindi hicho maandiko ya Itifaki za Kimataifa yaani Itifaki ya Kampala yaani Kampala Protocol on Voluntary Registration of Copyright and Related Rights 2021, Itifaki ya Beijing yaani Beijing Treaty on Audivisial Perfomances na Maandiko ya Mikataba ya mwaka 1996 iliandaliwa na kikao cha kuwakutanisha wadau wa Sanaa katika madaraja mbalimbali na kuwaelimisha wadau kuhusu Itifaki ,”amesema.