Kiwango kizuri kilichooneshwa na Taifa Stars katika mashindano ya COSAFA kwa kuifunga Bafana Bafana na kuiondoa mashindanoni, kumeisaidia kupanda katika viwango vya FIFA vya mwezi Juni mwaka huu kutoka 139 hadi 114.
Stars imeshika nafasi ya 30 kwa Afrika huku nafasi ya kwanza ikishikiliwa na Misri katika ubora, huku wadau wengi wakiliomba benchi la ufundi kuendelea kujijenga kwa ajili ya mashindano yajayo.
Licha ya kuwaondoa wenyeji, timu hiyo ilitolewa katika hatua ya nusu fainali na Chipolopolo ya Zambia na kujikuta ikicheza mchezo wa kumtafuta mshindi wa tatu na kisha kushinda kwa penalti 4-2 dhidi ya timu ya Lesotho.
Kabla ya Stars kuendeleza ubabe kwa timu ya Afrika Kusini, Serengeti Boys iliwahi kuifunga timu ya vijana chini ya miaka 17 ilipokuwa ikitafuta tiketi ya kushiriki fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika yaliyofanyika Gabon kwa 1-1 ugenini na kushinda 2-0 nyumbani.

Wakizungumza na JAMHURI juu ya hali hiyo, makocha na wataalamu nchini wamesema wachezaji na benchi la ufundi wameonesha upambanaji wa hali ya juu kulipigania taifa.
Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, ambaye kwa sasa ni kaimu Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka nchini,  Salum Madadi, amesema hatua ya timu kuingia nusu fainali tena katika nchi ya kigeni ni ya kupongezwa na ni ishara kuwa vijana wameanza kujiamini kwa kila hali.

Amesema pamoja na soka la Tanzania kukumbwa na misukosuko ya hapa na pale, lakini yote hayo ni majaribu ambayo wadau hawana  budi kushikamana na kuvuka wote kwa pamoja kwa manufaa ya mchezo wenyewe.
“Tunachoomba kwao ni utulivu katika kipindi hiki kuelekea katika uchaguzi mkuu wa Shirikisho, na wajumbe kuitumia haki yao kutuletea viongozi makini wenye uwezo wa kuhakikisha soka linasonga mbele,” amesema Madadi.
Kocha mkuu wa zamani wa Taifa Stars, Charles Mkwasa, amesema wachezaji wa Stars wameanza kuzielewa mbinu za mwalimu Salum Mayanga, hali ambayo imeendelea kuchochea hali ya kujiamini miongoni mwao.
“Kinachotakiwa  ni  kuendelea kuziunga mkono timu zetu hasa katika kipindi hiki cha mpito kwa kuhakikisha tunatoa michango ya  hali na mali kwa manufaa mapana ya soka  nchini  kwetu,” amesema Mkwasa.
Amesema maendeleo  ya soka  hayawezi kupatikana kwa watu  kuendeleza malumbano   yasiyo na tija kuanzia ndani ya klabu hadi timu za Taifa – kinachotakiwa ni kushikana wote kwa pamoja kuendelea kuwapa moyo wachezaji.
“Tuanze sasa kujenga vituo vya kukuzia vipaji vya watoto nchini kuliko kuiachia TFF na wadau wachache ambao wamekuwa wakihangaika kuibua vipaji vya wachezaji, bila ya kufanya hivyo tutabaki kuwalaumu walimu kila kukicha,” amesema Mkwasa.

Amesema mipango hiyo itawezekana pale Serikali nayo itakapoamua  kuwekeza rasilimali fedha katika suala  la michezo  na kuhakikisha michezo inachezwa katika shule zote kuanzia ngazi ya chini hadi vyuo vikuu nchini.
“Pia Serikali ipambane na wale wote waliovamia maeneo ya wazi yaliyokuwa yakitumiwa na vijana kwa ajili ya michezo kuanzia vijijini hadi mijini ambako maeneo hayo yamevamiwa na kugeuzwa makazi binafsi ya watu,” amesema Mkwasa.
Amesema kuna haja ya kuelekeza nguvu kubwa  sehemu kama Chuo cha Maendeleo ya Michezo cha  Malya na vyuo vingine kama tunahitaji kuendeleza mchezo wa soka na mingine kwa manufaa ya vijana wa leo na kesho.
Amesema katika nchi zilizoendelea kama Nigeria, Afrika Kusini, Misri na nchi nyingine linapokuja sulala la Timu ya Taifa kushiriki katika mashindano yoyote, Serikali za nchi hizo hutoa michango ya hali na mali kuzihudumia timu zao.
Kocha Mkuu wa Stars, Salum Mayanga, akizungumza na vyombo vya habari baada ya mechi na Lesotho, amesema kitendo cha timu kufikia hatua ya nusu fainali katika mashindano hayo huenda kikaanza kufungua milango kwa baadhi ya vijana kupata timu za kuchezea nje ya nchi.
“Mashindano haya yalikuwa yakitazamwa na mawakala wengi kutoka sehemu mbalimbali – ndani na nje ya bara hili, hali inayowaweka vijana katika nafasi nzuri ya kuweza kupata klabu za kuchezea nje ya Tanzania,” amesema Mayanga.