Wakati dunia ikihangaika kuokoa maisha ya watu kutokana na maambukizi ya virusi vya corona, kwa upande wa pili uchumi umeendelea kutikiswa na ugonjwa huo.





Hatua ya kuwataka watu kutotoka majumbani kama njia ya kukabiliana na kusambaa kwa virusi vya corona kumesababisha maduka mengi kufungwa, hivyo kuathiri biashara.

Umoja wa OECD tayari umeshaonya kuwa virusi hivyo vinaleta hatari kubwa katika uchumi wa dunia tangu mdororo wa kifedha ulioshuhudiwa mwaka 2008.

Shirika la Biashara la Umoja wa Mataifa (UNCTAD), nalo limeonya kuwa kudorora kwa uchumi wa dunia kutafikia asilimia mbili mwaka huu na kusababisha hasara inayofikia dola trilioni moja za Marekani.

Kura ya wachumi iliyoendeshwa na London School of Economics ilibainisha kuwa asilimia 51 ya wachumi wanaamini kuwa dunia inakabiliwa na mdororo mkubwa sana, hata kama COVID-19 haitaua watu wengi kama yanavyoua magonjwa mengine ya mafua kila mwaka. Ni asilimia tano tu ya wachumi hao ndio walisema wanaamini kuwa virusi hivyo havitasababisha matatizo makubwa kiuchumi.

Hadi kufikia mwishoni mwa wiki iliyopita kulikuwa na wagonjwa wapya 170,000 waliothibitika sehemu mbalimbali duniani kuambukizwa virusi hivyo ambavyo viliibuka mwishoni mwa mwaka jana katika Jimbo la Wuhan nchini China.

Biashara nyingi zimeanza kushuhudia kushuka kwa mapato kutokana na kupungua kwa mauzo na mifumo ya usambazaji bidhaa imeathirika sana baada ya viwanda vingi nchini China kufungwa.

Wiki kadhaa baada ya China kupiga marufuku safari kwa mamilioni ya watu wake, Italia nayo imejiunga nayo kwa kupiga marufuku safari zote, zikiwamo za ndani ya nchi huku Ufaransa na Hispania nazo zikipiga marufuku ya kusafiri.

Hadi mwishoni mwa wiki iliyopita, nchi nyingi barani Ulaya na Afrika nazo zilitangaza marufuku kama hizo ikiwa ni pamoja na kusitisha shughuli za biashara, ukiacha zile muhimu tu.

hata hivyo, inaelekea hali imeanza kutengemaa nchini China kwani Machi 11, mwaka huu wafanyabiashara katika Jimbo la Euhan walitangaziwa kuwa wanaweza kuanza uzalishaji katika viwanda vyao. Hiyo ilikuwa ni siku moja tu baada ya Rais wa China, Xi Jinping, kufanya ziara katika jimbo hilo kwa mara ya kwanza tangu kulipuka kwa ugonjwa huo.

Mdororo

China ni nchi ya pili kwa ukubwa kiuchumi duniani ikiwa inaongoza katika biashara, kwa hiyo kuathirika kwake na COVID-19 kutaathiri maeneo mengi duniani.

Katika kura iliyoendeshwa na Reuters kati ya Machi 3 na 5 mwaka huu, wachumi wabobezi walieleza kuwa mlipuko huo umeshusha uchumi wa China kwa asilimia 50 katika robo hii kulinganisha na robo iliyopita.

Kura hiyo iliyowahusisha zaidi ya wana uchumi 40, walio ndani na nje ya China, inabashiri kuwa ukuaji wa uchumi utaporomoka kwa wastani wa asilimia 3.5 katika robo hii kutoka asilimia sita katika robo ya nne ya mwaka 2019, ikiwa ni asilimia moja zaidi ya ilivyokadiriwa katika kura iliyofanyika Februari 14, mwaka huu.

“Kama upo katika jiji ambalo kimsingi lilifungwa kabisa au katika jiji ambalo watu wake wamezuiliwa majumbani, hauwezi kutoka mtaani, hauwezi kwenda kwenye jumba la sinema, mgahawani… mambo ambayo kwa kawaida ndiyo huchechemua uchumi, ni lazima uchumi utadorora tu,” anasema Rob Carnell, mkuu wa utafiti wa ING katika eneo la Asia na Pacific.

Ingawa shughuli zimeanza tena, lakini wataalamu wa uchumi wanaamini kuwa uchumi wa China utaendelea kuathirika kwani nchi hiyo haitaweza kupeleka bidhaa zake katika nchi nyingine ambazo hivi sasa zinapambana kukabiliana na ugonjwa huo.

Takwimu zilizotolewa Machi 16 zilionyesha kuwa uzalishaji katika viwanda vya China umeshuka kwa kasi kubwa katika miezi miwli ya kwanza mwaka huu, ikiwa ni ushukaji wa kasi sana katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita. Hiyo inaonyesha suhukaji mkubwa kuliko hata ule uliotabiriwa awali.

“Kwa kutumia takwimu hizi, mtikisiko wa uchumi wa China kutokana na janga la corona ni mkubwa zaidi ya mtikisoko uliotokana na mdororo wa kifedha wa mwaka 2008,” anasema Zhang Yi, mchumi mkuu wa Zhonghai Shengrong Capital Management.

Marekani yachukua hatua

Ili kukabiliana na madhara ya virusi vya corona kwa wafanyabiashara, Benki Kuu ya Marekani imechukua hatua kadhaa ili kuhakikisha wafanyabiashara hawaathiriki sana.

Machi 15, mwaka huu Benki Kuu ya Marekani ilishusha riba ya mikopo hadi karibu asilimia 0.

Hata hivyo, hatua hiyo, ambayo ilichukuliwa pia na Japan, Australia na New Zealand, jambo ambalo halijawahi kutokea tangu mdororo wa kifedha wa 2008, haikusaidia kuimarisha hali ya uwekezaji duniani kama ilivyotarajiwa.

Mathalani, bei ya mafuta iliendelea kushuka hadi chini ya dola 30 za Marekani kwa pipa mnamo Machi 16 na thamani ya hisa katika masoko la hisa Marekani ikashuka kwa asilimia tisa.

China ndiye mwagizaji mkubwa wa mafuta duniani. Kwa kuwa virusi vya corona vimeathiri uzalishaji viwandani na usafirishaji, International Energy Agency (IEA) inakadiria kuwa dunia itashuhudia kushuka kwa kiasi kikubwa kwa mahitaji ya mafuta duniani katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.

“COVID-19 kimesambaa nje ya China na makadirio ya mahitaji ya mafuta kwa mwaka 2020 yameporomoka kwa mapipa milioni 1.1 kwa siku. Kwa mara ya kwanza tangu 2009, mahitaji yanatarajiwa kuendelea kushuka, makadirio yakiwa kuwa itashuka kwa mapipa 90,000 kwa mwaka,” inasema IEA katika ripoti yake ya mwezi Machi.

Machi 9, mwaka huu, bei ya mafuta ilishuka kwa zaidi ya theluthi moja ya thamani yake – ukiwa ni mporomoko mkubwa zaidi tangu mwaka 1991 wakati wa vita ya Ghuba, wakati Saudi Arabia na Urusi zilipobainisha kuwa zitaongeza uzalishaji wakati tayari soko likiwa na bidhaa nyingi kuliko mahitaji. Nchi hizo zilitangaza uamuzi huo baada ya kushindwa kufikia muafaka katika makubaliano yao ya miaka mitatu.

“Tangazo la WHO (Shirika la Afya Ulimwenguni) kutangaza corona kama janga la dunia na kusitishwa kwa safari kati ya Marekani na Ulaya kunazidi kushusha mahitaji ya mafuta duniani, ikichangiwa na mapambano ya bei kati ya Saudi Arabia na Urusi,” anasema Margaret Yang, mchambuzi wa masuala ya masoko wa CMC Markets ya Singapore.

Mtu yeyote anayetarajia kuwa fedha mtandao (cryptocurrencies) zinawea kuwa salama katika kipindi hiki naye ataachwa na bumbuwazi.

Sarafu maarufu ya mtandaoni,  Bitcoin, ilipoteza thamani yake kwa zaidi ya asilimia 30 mwanzoni mwa mwezi Machi, ukiwa ni mporomoko mkubwa zaidi ya ule wa bei za mafuta na masoko ya hisa.

Athari katika usafiri

Machi 5, kabla Marekani haijatangaza kufuta safari kati yake na nchi nyingi za Ulaya, Shirika la Usafiri wa Anga Duniani (IATA) lilikadiria kuwa mlipuko wa COVID-19 utayagharimu mashirika ya ndege kiasi cha dola bilioni 113.

“Sekta ipo katika hali mbaya sana,” anabainisha Brian Pearce, mchumi mkuu wa IATA. “Kuna mashirika mengi ya ndege ambayo yamepata faida ndogo sana na kuwa na madeni makubwa na hii itayasababishia baadhi yake hali mbaya sana,” anaongeza.

Machi 16, Shirika la Ndege la Uingereza lilitangaza kuwa litapunguza safari zake kwa asilimia 75 mwezi ujao na Mei. Mashirika mengine ya ndege nchini Uingereza yakiwamo Virgin Atlantic na easyJet nayo yalitangaza kupunguza safari zake.