Kutangazwa kuwapo nchini kwa ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona kumesababisha kusuasua kwa huduma katika baadhi ya masoko jijini hapa.

JAMHURI limetembelea masoko ya Kariakoo, Karume na Kisutu ambayo aghalabu huwa na idadi kubwa ya watu wanaouza na kununua vitu na kushuhudia watu wachache tofauti na kawaida.

Wiki iliyopita serikali ilitangaza kuwapo nchini wagonjwa sita katika miji ya Arusha, Dar es Salaam na Zanzibar, taarifa iliyoambatana na maelekezo kadhaa ya namna ya kuchukua tahadhari kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa huo.

Miongoni mwa biashara zilizodorora ni ya kuuza na kununua nguo, ikidaiwa kuwa kwa sasa watu wengi wananunua zaidi chakula.

“Hali ni mbaya katika hizi siku baada ya ugonjwa kufika nchini. Tunaomba serikali ijitahidi kuudhibiti ili hali irejee kama kawaida,” anasema mfanyabiashara wa nguo wa Kariakoo, Francis Senga.

Senga anasema japokuwa ugonjwa haujasambaa sana ni vema serikali itenge fungu la fedha kwa ajili ya kununua chakula cha kutosha kuwasambazia wananchi masoko yatakapolazimika kufungwa.

Anasema hofu yake kubwa kwa sasa si mdororo wa biashara, bali afya ya Watanzania iliyopo hatarini kutokana na virusi hivyo.

“Biashara ipo tu ndugu yangu, mimi ninaona muhimu ni kuchukua tahadhari ugonjwa usisambae zaidi, kwa sababu ukiisha tutafanya biashara,” anasema Senga.

Katibu wa Fedha na Maafa katika Soko la Kisutu, Suleiman Sungura, ameliambia Gazeti la JAMHURI kuwa biashara katika soko hilo kwa sasa ni ngumu.

Anasema wateja wa Soko la Kisutu ambao kwa idadi kubwa ni Watanzania wenye asili ya Asia pamoja na raia wa China wanaoishi nchini, kwa sasa wanaogopa kwenda kununua bidhaa sokoni hapo na kusababisha mitaji ya wafanyabiashara wa mboga kukatika kutokana na mboga hizo kuharibika.

“Wahindi na Wachina waliposikia tangazo la serikali kuhusu kuwapo kwa corona, walinunua chakula kingi cha kutosha hadi kwa wiki mbili. Kwa hiyo sasa hivi hawaji kabisa sokoni,” anasema Sungura.

Hali hiyo imesababisha mapato ya soko hilo kupungua, hivyo kukosa michango ya kulipia ankara za umeme na ulinzi sokoni hapo.

“Kila mfanyabiashara huchangia Sh 200 tu. Lakini hauwezi kuamini, kwani tangu ugonjwa huu ulipotangazwa hiyo Sh 200 inachangishwa kwa shida sana,” anasema Sungura.

Wiki iliyopita serikali ilitangaza kusitisha masomo na kufunga shule kuanzia zile za awali hadi vyuo vikuu nchi nzima kwa muda wa siku 30.