Baada ya waandishi wa habari kuniuliza nini kitatokea endapo janga la corona litaenda hadi wakati wa Uchaguzi Mkuu, nimeona ni vema kuandika maoni yangu kupitia uchambuzi wa kisheria.
Ni kweli kwamba ugonjwa huu ukizidi kuwa mkubwa nchini, mazingira ya kwenda kwenye uchaguzi miezi mitatu ijayo wakati watu wanakufa yatakuwa magumu sana.
Kipindi cha uchaguzi ni kipindi kinachoyaleta pamoja makundi ya watu kwa wingi sana kuanzia kwenye teuzi ndani ya vyama, kampeni, wakati wa kupiga kura hadi kutangaza matokeo.
Mlipuko wa ugonjwa ukiwa mkubwa kwa viwango kama vya Italia, China, Iran, Ufaransa na Afrika Kusini, kufanyika
uchaguzi kwa mtindo wa mikusanyiko itakuwa ni hatari kubwa kwa taifa.
Kinachoweza kufanyika ni kupeleka kila kitu katika mfumo wa kidijitali, kitu ambacho sidhani kama tunaweza
kiuweledi, kitaaluma na kiuchumi. Yaani kuanzia uteuzi, kampeni hadi upigaji kura na utoaji matokeo ama uende
kimtandao au uchaguzi usogezwe mbele.
Kuna faida na hasara za kusogeza mbele uchaguzi ingawa hii si hoja yangu leo. Faida mojawapo ni kama kweli tuna nia ya kuboresha sheria za uchaguzi na Tume Huru, huu ndio muda unaoweza kutumika kufanya hayo. Hasara ni
nyingi, mojawapo ni watawala wa sasa kutumia mwanya huo kubaki madarakani kama katiba itawaruhusu.
Turejee kwenye hoja ya msingi. Je, kisheria na kikatiba uchaguzi unaweza kusogezwa mbele kwa sababu ya corona? Je, viongozi wa sasa, yaani madiwani wabunge na rais wanaweza kuendelea kikatiba muda wao ukiisha?
Katiba inasemaje kuhusu muda wa urais?
Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara ya 42 (2); Rais isipokuwa labda
atafariki au kujiuzulu, atakuwa na muda wa miaka mitano katika nafasi yake toka siku anapochaguliwa.
Katiba inatuambia kuwa ndani ya siku saba baada ya kuchaguliwa rais mpya anapaswa kuwa amekwisha kuapishwa na kuingia Ikulu. Katiba yetu inatuambia kuwa rais aliyeko madarakani ataendelea kuwepo madarakani kwa muda usiozidi siku saba tangu Rais Mteule atangazwe; lakini katiba hiyo haijakaa vizuri kuelezea endapo itachukua muda mrefu tangu kura zimepigwa kumpata Rais Mteule.
Suala hili la muda gani baada ya uchaguzi kufanyika, si hoja ya leo. Ni wazi kuwa Katiba yetu imeweka ukomo wa rais kuwa madarakani ni baada ya miaka mitano kwisha. Kuongeza muda wake iwe kwa sababu yoyote ile au kupunguza muda wake inabidi uwe ni mchakato wa kikatiba wenye kufuata misingi ya katiba na muundo wake.
Katiba inasemaje kuhusu muda wa Bunge?
Ibara ya 65 (1) ya Katiba inaelekeza kuwa maisha ya Bunge yatakuwa ni miaka mitano. Maisha ya Bunge yanaanza mara moja baada ya uchaguzi kukamilika na Bunge jipya kuitishwa na kukutana na huisha pale Bunge linapovunjwa ili mchakato wa Uchaguzi Mkuu uanze.
Muda wa mbunge kuwa ofisini
Ibara ya 71(1) imetaja mambo ambayo yatasababisha kukoma kwa muda wa mbunge kuwa ofisini. Ibara ya 71(1) (g)
inasema muda wa ubunge wa mbunge utakoma pale Uchaguzi Mkuu unapoitishwa. Baada ya uchaguzi rais ataliitisha Bunge kama alivyoelekezwa na Ibara ya 90 (1) ya Katiba.
Kwa mujibu wa Katiba, Tume ya Uchaguzi inapoanza mchakato wa uchaguzi viti vya wabunge hubaki wazi lakini rais bado ataendelea kubaki ofisini kwa sababu yeye muda wake huisha pale Rais Mteule anapoapishwa.
Katiba inaruhusu kusogeza mbele uchaguzi?
Ndiyo. Kwa mujibu wa Ibara ya 42 (4) ya Katiba, uchaguzi unaweza kusogezwa mbele kwa mchakato utakaopelekwa
bungeni. Katiba inaelekeza kuwa Tanzania itasogeza uchaguzi mbele kwa sababu moja tu ambayo ni endapo uchaguzi utaangukia kipindi cha vita na nchi nyingine.
Bunge limepewa mamlaka kupitisha azimio la kusogeza mbele uchaguzi kwa muda usiozidi miezi sita. Corona au mlipuko wa magonjwa haikutajwa kama sababu ya kusogezwa uchaguzi mbele! Kwa maana hiyo uchaguzi utaendelea kufanyika kama ilivyoelekezwa na Katiba na Sheria za Uchaguzi.
Ili Bunge liwe na mamlaka ya kusogeza mbele uchaguzi ni lazima kwanza tuunde Bunge la Kikatiba kubadili vifungu hivi na kuongeza ‘milipuko ya magonjwa’ kama sababu ya kusogeza mbele uchaguzi. Misingi mikuu ya kikatiba na
demokrasia inapendelea mabadiliko yoyote ya msingi yanayogusa misingi ya kikatiba na muundo wa kikatiba (basic
structures) yaamuliwe na wengi. Najua kwa hali ya utawala wa sheria ilivyo sasa nchini, wanaweza kulazimisha kutumia Bunge la sasa kusogeza mbele uchaguzi kinyume cha Katiba na ili waweze kufanya hivi, inabidi wafanye mapema kabla muda wa maisha ya Bunge haujaisha miezi mitatu tu ijayo.
Katiba inaruhusu kusogeza mbele muda wa Bunge?
Katiba ya Tanzania ndiyo imeruhusu kupeleka muda wa Bunge mbele baada ya miaka mitano ya kikatiba kukamilika.
Je, ni sababu zipi zimewekwa na kuruhusu maisha ya Bunge kuongezeka?
Muda wa Bunge utahesabiwa kuwa umekwisha na limevunjwa mara baada ya muda kwisha hata kama rais hatalivunja. Ibara ya 90(3) ya Katiba imetoa sababu moja tu ambayo inaweza kutumika kuongeza maisha ya Bunge
kama ilivyo kwa uchaguzi. Sababu hiyo ni endapo Tanzania itakuwa vitani.
“Bunge litahesabiwa kuwa limevunjwa baada ya muda wa maisha yake kumalizika, isipokuwa… Jamhuri ya
Muungano imo katika vita, Bunge linaweza kuongeza maisha ya Bunge… kwa muda usiozidi miezi 12…” Ibara ya
90(3).
Kwa mujibu wa Katiba, hakuna sababu nyingine inayoweza kurefusha maisha ya Bunge. Kwa maana hiyo hata suala hili la corona haliwezi kuwa sababu.
Ndiyo hapa Watanzania mtuelewe vizuri, kwanini tunataka katiba mpya. Katiba ya sasa ina kasoro nyingi zinazotokana na ukweli kuwa ilitungwa katika mazingira ya mfumo wa chama kimoja.
Uchaguzi ukisogezwa nani atashika nafasi ya Rais?
Swali jingine tata ni kuhusu endapo watafanikiwa kusogeza mbele uchaguzi, nani atakuwa Rais na Makamu wake
kwa kuwa wote kikatiba watakuwa wamemaliza muda wao?
Kwa Mujibu wa Katiba, Ibara ya 37 (3), watu wanaoweza kushika nafasi za urais ikiwa rais hayupo kwenye kiti chake kwa sababu kadhaa ni Makamu wa Rais na Waziri Mkuu. Hawa kwa mujibu wa Katiba pia muda wao ni miaka mitano.
Maana yake ni kwamba baada ya Oktoba 25, 2020, Tanzania itakuwa haina Rais, Makamu wala Waziri Mkuu halali
kikatiba.
Wakati huo huo tusisahau kuwa Ofisi ya Rais haipo wazi kama ilivyo kwa wabunge, mazingira haya ni kama vile
uwepo wa mamlaka ya urais yasiyorasimishwa na kifungu chochote cha Katiba. Nchi nyingine wakati wa uchaguzi Ofisi ya Rais hukaliwa na watu wengine wasioshiriki uchaguzi kipindi chote cha uchaguzi endapo rais naye ni
mgombea.
Maana yake ni kuwa Katiba isipozingatiwa, rais anaweza kuendelea kuwa rais hadi atakapochoka akiamua kutoitisha uchaguzi au kutokuruhusu Rais Mteule kuapishwa.
Maana yake tukitaka hawa watu waendelee, hatuna budi kurudi kwenye Bunge la Katiba kurekebisha vifungu hivi
au kutumia Ibara ya 98 (1)(b) ambayo inahitaji theluthi mbili ya wabunge kutoka Bara na theluthi mbili ya wabunge kutoka Zanzibar kuunga mkono badiliko hilo. Kati ya mambo yaliyotajwa katika orodha ya pili ni kuhusu uwepo
wa Bunge na uwepo wa Ofisi ya Rais wa Jamhuri ya Muungano. Huwezi ukazungumzia suala la kusogeza uchaguzi bila kuzungumzia Bunge na nafasi ya urais. Hivyo tunapokuwa tunajadili haya kama taifa tuyajadili kwa pamoja.
Hitimisho
Kwa ujumla kikatiba na katika kufuata misingi yake ni vigumu sana kusogeza mbele uchaguzi kwa sababu ya corona. Corona inaweza kuwa sababu nzuri ya kusogeza mbele uchaguzi endapo hali itakuwa tete zaidi, lakini Katiba hii tuliyotaka kuibadilisha wachache wakakataa, ndiyo itazuia mabadiliko haya kufanyika. Katika Bunge la leo ni vigumu sana kupata theluthi mbili ya wabunge kwa Bara na Zanzibar katika hali ya sasa ya uhasama baina ya upinzani na chama tawala.
Tunaweza kuwa na jambo la msingi kitaifa lakini kwa kuwa kuna kundi moja limefananishwa na corona, itakuwa
vigumu kuafikiana kubadili Katiba kwa lengo la kukabiliana na corona halisi. Kwa maana hiyo kikatiba corona haiwezi kuwa sababu ya kusogeza mbele uchaguzi kwa kuwa Bunge na Rais wanafikia kikomo cha madaraka mwaka
huu. Wapinzani wana kura ya turufu bungeni kuamua haya mabadiliko yafanyike au yasifanyike. Wakati mwingine ndiyo siasa inanoga na kufanya uamuzi uwe na umakini unapokuwa na Bunge lenye mchanganyiko wa vyama.
Haya ni maoni yangu yenye jicho la uchambuzi na si jibu la mwisho la maswali ya Watanzania na waandishi katika suala hili.
Makala hii imeandikwa na Mratibu wa Taifa wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Onesmo Olengurumwa, na kufanyiwa uhariri kuweka ufasaha wa lugha ya Kiswahili – MHARIRI