Dunia inatetemeka! Habari kubwa kwa sasa ni juu ya virusi vya corona ambavyo vimetapakaa karibu ulimwengu wote. Havichagui jina wala umaarufu. Wale watu maarufu zaidi nao kwa sasa wamo katika karantini katika mikakati ya kuzuia kusambaa kwa virusi hivyo.

Tuizungumzie michezo. Kwa sasa virusi vya corona vimeitikisa sekta ya michezo na vimewaumiza wengi kuanzia juu mpaka yule anayependa ‘ku-bet’, wote wanalia juu ya virusi hivi ambavyo tunaomba Mungu tu atunusuru na janga hili.

Wakati wengi ‘walitaka kuchana mikeka’ wakashangaa kusikia Ligi Kuu England michezo yote ya mwishoni mwa wiki inasimamishwa kutoka na virusi hivyo kuvamia pia watu kadhaa katika sekta ya michezo.

Ligi Kuu England imesimamishwa hadi Aprili 3, baada ya timu tano zinazoshiriki ligi hiyo kudai baadhi ya wachezaji wao wamo katika karantini. Ikabainika hata Meneja wa Arsenal, Mikel Arteta, amekumbwa na virusi hivyo, pamoja na winga wa Chelsea, Callum Hudson-Odoi.

“Nimepata virusi hivi siku kadhaa zilizopita, kwa sasa ninaendelea vizuri, niliamua kufuata masharti yote na kujiweka karantini mwenyewe. Naamini nitawaona karibuni,” alisema Hudson-Odoi.

Tayari Mwenyekiti wa Chama cha Soka England (FA), Greg Clarke, ameshatoa taarifa kwa timu zote za Ligi Kuu akisema haoni kama ligi hiyo itamalizika msimu huu, huku akisisitiza kila kitu ‘kimekaa vibaya’.

Nalo Shirikisho la Soka Ulaya (UEFA), limeahirisha mechi zote za Ligi ya Mabingwa na Europa League kutokana na kujaribu kupambana kuzuia kuenea kwa virusi hivyo.

Shirikisho la Soka Afrika (CAF) halipo nyuma, limeamua pia kuahirisha michezo yote ya kufuzu AFCON ili pia kupambana na kuenea kwa virusi hivyo vinavyoitikisa dunia kwa sasa. Wakati unazungumzia hayo, bado usisahau kuna michuano ya Olimpiki, ambayo nayo imo katika hatihati ya kufanyika.

Mbali na Ligi Kuu England, ligi zote maarufu unazozifahamu duniani hazikufanyika mwishoni mwa wiki, kutokana na tatizo la virusi hivyo. Hiyo ni kuanzia Bundesliga ya Ujerumani, Ligue 1 ya Ufaransa, La Liga ya Hispania, Serie A ya Italia ambayo ilisimamishwa muda mrefu.

Nchi nyingi zimesimamisha matamasha kadhaa ya michezo mpaka burudani, hii yote ni kujikinga na kuenea kwa virusi vya corona.

Kusimamishwa kwa ligi, matamasha na michuano mikubwa kumewaumiza wengi, kuanzia kampuni za ku-bet, wachana mikeka, mabanda ya mipira, mpaka wazee wa miundombinu.

Kampuni za kamari

Moja kati ya kampuni kubwa zaidi ya kamari duniani ya William Hill iliyopo Marekani, imetoa taarifa yake na kusema ‘ni wakati mgumu kuliko wote’, maneno yaliyosemwa na Ofisa Mtendaji Mkuu wa kampuni hiyo, Joe Asher.

Hii ni baada ya michezo yote kusimamishwa na wamekiri kwa sasa hawajui cha kufanya zaidi ya kutazama na kuomba virusi vya corona vipotee ili mambo yaendelee.

“Huu ni wakati mgumu ambao hatujawahi kuupitia, tulishuhudia mchezo mmoja ukifungiwa na mambo yanaendelea, lakini kwa sasa tunapita katika kipindi kigumu mno. Hatujui hata mlango wa kutokea,” alisema.

Kampuni kadhaa za kamari ndani ya Uingereza pia zimekiri kwa sasa zimeanguka na zinapunguza wafanyakazi wake, hii yote ni kutokana na michezo mingi kusimamishwa na hakuna wa ‘kuchana mkeka’ tena.

Wamiliki wa mabanda

Wengi wa wamiliki wa mabanda yanayoonyesha mipira wanalia kutokana na hasara wanayopata kwa sasa, wengi wanadai walilipia visimbusi vyao mapema kwa kutegemea mechi za ligi kubwa hasa zile za Ulaya, lakini kutokana na kutoonyeshwa wamejikuta katika wakati mgumu.

“Mimi hapa nimelipia ving’amuzi vya kampuni tatu, sasa hizi mbili (akizitaja) ndizo zilizokuwa zinaniingizia fedha, nimepata hasara kubwa na uwezo wa kulipa tena sina, nilikuwa nawatoza wanaokuja ili tusaidiane katika kulipa,” anasema Juma Nassor anayemiliki banda lake maeneo ya Majohe kwa Ngozoma, Dar es Salaam.

Naye Abubakar Bakari anayemiliki banda lake maeneo ya Mbagala Mianzini, Dar es Salaam, anasema wengi wanaomiliki mabanda kwa sasa kwao ni hasara tupu, kwani hakuna tena wanachopata.

“Hili dude la corona kama lingekuwa mtu ningepigana nalo, nasomesha watoto kupitia banda hili, leo hakuna kitu, wengi wetu tumebaki maskini kwa sasa.”

Wazee wa kuchana mikeka

Kamakuna kundi ambalo linalia kwa kiasi kikubwa kwa sasa ni hawa ‘wazee wa kuchana mikeka’ ambao kila siku walikuwa wakikesha katika vibanda kutazama mechi ipi atupe kamari yake.

Vijana wengi wanaojihusisisha na kubashiri matokeo ya mechi wameeleza kuwa virusi vya corona vimewaweka katika wakati mbaya mno kuliko wakati mwingine wowote ule.

 “Braza, kusema kweli tumefika katika wakati mbaya sana, wengi tulikuwa tunaamkia huku, ila corona kwa sasa imetuumbua,” anasema kijana mmoja akiwa katika banda la kuchezesha kamari eneo la Kariakoo, Dar es Salaam.

Wachambuzi wa michezo

Kwa muda sasa ajira za wengi zitatikisika, kwani wengi wa wachambuzi wa michezo kuanzia wale wa kimataifa mpaka wa kwetu, watajikuta katika wakati mgumu wa kutopata ‘posho’.

“Huu ni wakati mgumu kwa kila mtu, michezo imewekwa rehani mpaka kwa wachambuzi, hali ni tete sana,” anasema mmoja wa wachambuzi na aliyepata kucheza soka,  James Lee Duncan Carragher.

Ukweli ni kwamba katika kipindi hiki dunia inapita kwenye wakati mgumu hasa katika michezo.