Nimesimuliwa jinsi abiria wa ndege aliyekaa pembeni ya Mchina kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza alivyoingiwa hofu ya kuambukizwa homa ya corona – COVID-19 – akaamua kusoma gazeti tangu ndege inapaa hadi inatua Mwanza, akiamini gazeti litamkinga kuambukizwa.
Hii simulizi inatuambia mawili; kwanza, inaimarisha unyanyapaa dhidi ya Wachina kuwa ugonjwa huu ni ‘kirusi cha Kichina’ kama anavyopenda kurudia rudia Rais Donald Trump wa Marekani. Pili, kuthibitisha kuwa bado kuna masuala mengi hayaeleweki vizuri juu ya njia za kuambukizwa COVID-19.
Tanzania ina wagonjwa sita tu (hadi mwishoni mwa wiki iliyopita) lakini kuanza kujenga taswira kuwa ni Wachina ndio wabeba virusi wakuu kutasaidia tu kulegeza tahadhari, tukiamini ni Wachina tu ndio waambukizaji.
Katika hatua za awali za mlipuko wa COVID-19 nilikuwa kama Rais Donald Trump wa Marekani nikiamini dunia ilijijaza hofu ambayo haikuwa na mantiki yoyote.
Trump alilaumu vyombo vya habari kwa kutia chumvi juu ya athari za ugonjwa huu, akisema ni ugonjwa ambao hauna tofauti sana na homa ya kawaida ya mafua.
Aliwalaumu wapinzani wake wa kisiasa kwa kugeuza ugonjwa ambao hauna madhara yoyote na kuibua hoja za kisiasa dhidi yake. Aliuita ugonjwa feki.
Bila shaka moja ya sababu zinazomfanya Trump na serikali yake sasa kuchukua hatua madhubuti za kudhibiti maambukizi ya COVID-19 nchini Marekani ni kulinda masilahi ya biashara na uchumi.
Hatimaye, kilichomuamsha ni siasa ile ile ambayo Trump aliwashutumu kuwa inachochewa na wapinzani wake dhidi yake. Hali mbaya ya biashara na uchumi ni sumu kwa mwanasiasa aliyeko madarakani. Hali nzuri ya biashara na uchumi huimarisha uwezekano wa kuchaguliwa tena.
Kusambaa kwa corona, ingawa kumeanzia China, kumeathiri uchumi kwenye nchi nyingi za Magharibi. Athari kama hizi kwa nchi changa huchelewa kuonekana kwa sababu ya kukosekana kwa uhusiano wa karibu wa uchumi wa China na nchi changa, tofauti na ilivyo kwa nchi za Magharibi.
Kampuni nyingi za kimataifa zina viwanda nchini China na kufungwa kwa viwanda baada ya kulipuka ugonjwa kumepunguza ukuaji wa uchumi si tu kwa China, bali pia kwa makampuni haya yenye viwanda China.
Kushuka huku kwa uzalishaji kunapunguza sana mahitaji na uagizaji wa mafuta kwa China na kuathiri kwa kiasi kikubwa biashara zinazotegemea soko la mafuta la dunia.
Aidha, Wachina bilioni 1.4 ni soko kubwa la bidhaa na huduma kwa makampuni mengi nje ya China. Kwa sababu hiyo biashara zinazotegemea soko hilo nazo zimeathirika sana.
Katika kuhimili mtikisiko huu kwa uchumi wa Marekani, Rais Donald Trump alitangaza hivi karibuni hatua za kupunguza makali ya mdororo huu wa biashara na uzalishaji.
Hakuna ubishi sasa kwamba ugonjwa huu unaleta athari – ziwe za biashara na uchumi, au za kiafya. Hata sisi wengine ambao, kama Rais Trump, tuliona kuwa taarifa za ugonjwa huu ni uzushi, tunaona dalili dhahiri kuwa tuanakabiliwa na janga kubwa.
Kama nilikosa chembe ndogo tu ya uhakika kuwa hali imekuwa mbaya, basi uhakika huo umeimarika nilivyorudi Butiama siku kadhaa zilizopita kutoka safari ya Dar es Salaam. Mfanyakazi wa nyumbani kakaa mbali sana na mimi kama alivyohofiwa yule abiria Mchina. Na hapo zingatia kuwa wameripotiwa wagonjwa sita tu walioambukizwa virusi vya corona nchini.
Kwa sababu hizi, hatuna budi kuanza kuchukua tahadhari kabla hali haijawa mbaya zaidi. Mamlaka za afya Marekani zinatuarifu kuwa mara taarifa za awali za kutokea ugonjwa kuanza kufahamika, mamlaka hizo zilianza kuweka tahadhari za afya, tofauti na nchi ya Italia ambayo ilichelewa sana kuchukua hatua.
Athari za kuzembea huko kunaonekana leo. Wakati ninaandika makala hii maambukizi nchini Marekani yalikuwa 19,774 wakati nchini Italia yalikuwa 47,021. Vifo nchini Italia vilikuwa 4,032 wakati nchini Marekani vilikuwa 275 tu.
Nahisi zipo jitihada za kutosha rasmi za kudhibiti ugonjwa huu nchini. Lakini hizo hazitoshi. Zipo hatua ambazo mtu mmoja mmoja anaweza kuchukua. Kama unakohoa na una homa, kaa nyumbani, usichagamane na watu, na acha kumangamanga bila sababu ya msingi ukasababisha janga kuwa balaa.
Tuweke tahadhari ya kuepuka taarifa na kinga za uongo. Zipo taarifa nyingi za vijiweni ambazo zinapotosha ukweli. Usinawe mikono kwa kutumia vodka au gongo, kama baadhi ya waongo walivyoshauri ukadhani utafanikiwa kujikinga na ugonjwa huu. Vodka ina asilimia 40 tu ya kileo. Dawa ya kunawia inapaswa kuwa na asilimia 60 ya kileo.
Wengine wamesema vitunguu swaumu vinasaidia kujikinga dhidi ya COVID-19. Hakuna ushahidi kuwa hilo ni kweli. Ukila vitunguu swaumu utafanikiwa kuchafua tu hewa kwa yeyote aliyekukaribia.
Njia nzuri na ya uhakika kwa nchi kujikinga dhidi ya ugonjwa huu ni kufunga mipaka yake ili kuzuia wasafiri kutoka nje, hasa kutoka nchi ambazo zinaongoza kwa maambukizi – China, Italia, Hispania, Ujerumani na Marekani – kuingia nchini mpaka maambukizi mapya duniani yatakapodhibitiwa.
Labda wakati wake bado, lakini hatuwezi kusema kuwa haitatokea.
barua pepe: [email protected]