Kwamba ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona upo nchini; hii inafahamika kwa watu wengi kwa sasa, lakini kubwa linalosisitizwa na wataalamu ni kuwa ugonjwa huu si sawa na mafua ya kawaida kama wengine wanavyodai.
Utafiti unaonyesha kuwa virusi hivi ambavyo vinapoingia mwilini mwa binadamu huenda kwenye mapafu na kusababisha homa, kikohozi kikavu na maumivu ya viungo, vinasambaa kwa kasi zaidi kuliko virusi vinavyosababisha mafua ya kawaida.
“Huu ugonjwa ni hatari zaidi mara 10 ya mafua ya kawaida kwa kuwa hauna chanjo. Mafua ya kawaida yana chanjo na pia miili yetu ina kinga ya kuzaliwa nayo dhidi ya magonjwa haya.
“COVID-19 ni ugonjwa mpya. Miili yetu imeshitukizwa, haijajiandaa. Hatari zaidi ni kuwa kama una magonjwa mengine kama saratani, ugonjwa wa moyo au shinikizo la damu, kisukari ukipatwa na corona, uwezekano wa kufariki dunia unakuwa mkubwa zaidi,” anasema mtaalamu wa afya na Mkurugenzi wa Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Profesa Mohamed Janabi.
Profesa Janabi anasema maambukizi ya ugonjwa huu ni ya kasi kuliko mafua ya kawaida, akisema virusi hivi vikitoka kwa mtu kwa njia ya kukohoa vina uwezo wa kukaa kwenye meza, sakafu au mlango kwa hadi siku tatu na iwapo mtu atagusa eneo hilo na kuvichukua virusi kisha akajigusa mdomoni, puani au machoni, huambukizwa ugonjwa huo.
Anasema aliyeambukiza kwa njia hiyo naye anaweza kumuambukiza mwingine kuanzia siku ya saba hadi ya 14 wakati mwenyewe wala hana dalili yoyote.
“Na kila mtu mmoja ambaye ameambukizwa huu ugonjwa na hana dalili yoyote ana uwezo wa kuambukiza watu wengine kati ya wanne hadi sita,” anasema profesa huyo.
Hofu kubwa ya mtaalamu huyo wa afya na magonjwa ya moyo ni hatari ya kuwa na wagonjwa wengi watakaolazwa hospitalini na kuhitaji mashine za kuwasaidia kupumua wakati idadi hiyo inazidi idadi ya mashine hizo au hata idadi ya wahudumu wa afya.
Profesa Janabi hana hofu na uwepo nchini wa mashine hizo, lakini iwapo idadi ya wagonjwa ikizidi, hali huwa mbaya.
“Hii ndiyo iliyotokea Italia. Wagonjwa walikuwa wengi wakati vitanda kwa ajili ya kuwahudumia na kuwapa mashine za kuwasaidia kupumua havitoshi,” anasema.
Katika hali kama hiyo, taarifa zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 700 walikufa ndani ya siku mbili juma lililopita, huku mwishoni mwa juma nchi hiyo ilirekodi wagonjwa zaidi ya 800 wakifariki dunia ndani saa 24, idadi ya kutisha kuwahi kutokea katika enzi hizi za mapinduzi makubwa ya kiteknolojia na huduma za afya duniani.
Eneo lililoathirika zaidi kwa corona nchini Italia la Lombardy sasa limepiga marufuku matembezi hata mazoezi ya mtu mmoja mmoja mitaani.
Hatua hizo zimechukuliwa na kiongozi wa eneo hilo, Attilio Fontana. Hadi Jumamosi jioni, takriban vifo 3,095 vilikuwa vimetokea eneo la Lombardy pekee, wakati nchi nzima ya Italia ikiwa na vifo 4,825.
Hata hivyo, Profesa Janabi anaamini Tanzania hatutafika kiwango hicho, kwa kuwa hatujachelewa kuchukua hatua, akiwataka wananchi kufuata maelekezo yanayotolewa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Wizara ya Afya pamoja na Kamati ya Taifa ya Kupambana na Corona iliyoundwa wiki iliyopita.
Miongoni mwa maelekezo hayo ni watu kuacha tabia ya kushikana mikono, kujenga tabia ya kunawa mikono mara kwa mara, kuacha kujishika usoni na kuepuka safari au mikusanyiko isiyo ya lazima kwa kipindi hiki.
Mataifa yafunga mipaka, viwanja vya ndege
Mataifa kadhaa duniani tayari yamesimamisha safari za ndege kwenda katika nchi zenye maambukizi makubwa ya corona kama China, Italia na Iran.
Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa Rwanda na Uganda ni miongoni mwa mataifa jirani yaliyoamua kufunga mipaka.
Taarifa iliyotolewa na Waziri Mkuu wa Rwanda, Edouard Ngirete, inasema kuanzia Jumamosi iliyopita hakuna mgeni atakayeruhusiwa kuingia nchini humo isipokuwa raia wao wanaorejea nyumbani.
Ngirete pia amepiga marufuku watu kutembeleana bila sababu huku akielekeza wafanyakazi wa umma na sekta binafsi kufanyia kazi nyumbani; miamala ya malipo mbalimbali kufanyika kwa mtandao, baa kufungwa na hoteli na migahawa kutoa huduma ya ‘take away’.
Nchini Uganda imepiga marufuku raia wa mataifa yaliyoathirika kwa corona kuingia nchini humo huku ikielekeza wageni wanaoingia Uganda kutengwa au kujiweka katika karantini kwa siku 14 kabla ya kuingia uraiani.
Nchini Afrika Kusini, serikali inafanya utaratibu wa kujenga uzio kati ya taifa hilo na Zimbabwe ili kuzuia muingiliano wa raia wa mataifa hayo mawili.
Ujumbe kutoka China kwa JAMHURI
Wakati Italia na dunia zikiyaanza mapambano dhidi ya corona kati ya Februari na Machi mwaka huu, nchini China ambako ugonjwa huo ulizuka Desemba mwaka jana, hali imeanza kudhibitiwa.
Kwa siku mbili mfululizo wiki iliyopita, Wuhan, ambako ndiko ugonjwa ulikoanzia hakukuwa na kifo hata kimoja huku maambukizi mapya nayo yakiwa ni sifuri kwa wenyeji.
JAMHURI iliwasiliana na Mtanzania mmoja anayeishi nchini China ambaye alichukua nafasi hii kuwatia moyo Watanzania na kuwashauri nini cha kufanya.
“Kwanza niwatoe hofu huko nyumbani Tanzania. Msiwe na hofu, tutakipita kipindi hiki salama. Jambo la muhimu ni kufuata masharti yanayotolewa na serikali na kumuomba Mungu aliepushe janga hili lisisambae zaidi.
“Niwashauri katika kipindi hiki, mbali na kwenda kwenye majukumu yenu ya kikazi kutafuta riziki, epukeni kwenda maeneo yenye misongamano, epukeni vikao visivyo vya lazima na tumieni zaidi njia mbadala za mawasiliano kama simu/skype na email.
“Kila mmoja azingatie kanuni za usafi; kunawa mikono kila mara baada ya kushika chochote. Kama una barakoa (mask) ni vizuri kuivaa kama unakwenda maeneo ya hospitali.
“Kwa ujumla tutunze afya zetu. Kunywa maji mengi (ya moto au vuguvugu), kula chakula bora, matunda na juices kupata vitamin C. Kama unaweza nunua supplements za vitamin C.
“Kwa hakika kupata corona si death sentence (hukumu ya kifo). Ukizingatia kanuni za usafi na kujikinga hautapata. Ukila chakula bora, matunda na multivitamins utakuwa na immunity (kinga) itakayowezesha mwili kupambana na virusi vya corona.
“Maelfu ya waliopoteza maisha China, Iran, Italia na Marekani ni wazee (mara nyingi kinga zao ni dhaifu) na watu ambao tayari wana magonjwa kama kisukari, moyo na kifua kikuu.
“Ndiyo maana hata ukiangalia hapa China, mfano Jimbo la Hubei, maambukizi yalipoanzia, idadi ya waliougua hadi kulazwa ni ndogo sana ikilinganishwa na wingi wa watu.
“Population ya Hubei ni watu milioni 50. Mji Mkuu wa Jimbo, Wuhan, kuna watu milioni 11. Lakini jumla ya watu waliougua ni 85,000 tu. Waliopoteza maisha hawazidi 4,000. Ndiyo maana maelfu ya wanafunzi kutoka nje (ya China) waliopo Hubei wakiwemo Watanzania, hakuna hata mmoja aliyeugua au kufa; ukiachilia yule wa Cameroon aliyeugua na kupona.
“Siri ya usalama wao si nyingine bali ni kufuata masharti yanayotolewa na serikali na wataalamu. Kwanza, kunawa mikono kila wakati; pili, kuepuka misongamano; tatu, kutoshika uso baada ya kushika eneo jingine au kabla haujanawa mikono; nne, kuacha kupeana mikono; tano, safisha mara kwa mara kitu unachotumia kama simu, remote control au ufunguo; sita, kula chakula bora na matunda ili kupata Vitamin C kwa wingi kwa ajili ya kujenga kinga mwilini.
“Mambo mengine ni kufanya mazoezi na kubwa zaidi ni kuepuka mvua ya habari feki kutoka kwenye mitandao zenye lengo la kutisha watu. Sehemu sahihi za kupata taarifa ni Wizara ya Afya na tovuti ya WHO,” anamaliza salamu zake Mtanzania huyo kutoka China.
Tahadhari zaidi
Wakati masomo katika shule na vyuo mbalimbali yakisitishwa, Watanzania wametakiwa kutoruhusu watoto kucheza na kutembea ovyo mitaani ili kuwakinga na maambukizi ya virusi vya corona.
Wazazi pia wametakiwa kuwaelekeza watoto kutumia muda huu kujisomea majumbani; kutopokea kitu ambacho mwenzake amekula kama matunda, ice cream au barafu.
Wakati huo huo, katika kuwakinga wafanyakazi wake dhidi ya maambukizi ya corona, Mhariri Mtendaji wa Gazeti la JAMHURI, Deodatus Balile, amesema kuanzia sasa wafanyakazi wa gazeti hilo wataanza kufanya kazi kwa njia ya mtandao.
Balile amesema hatua hiyo itapunguza uwezekano wa wafanyakazi hao kuambukizwa virusi hivyo wawapo njiani au ofisini.
“Tayari tumenunua sanitizer kwa ajili ya wageni na wafanyakazi wetu. Lakini hii haitoshi, ndiyo maana tumeamua kuunga mkono mapambano dhidi ya corona kwa kuwaelekeza wafanyakazi wetu kufanyia kazi nyumbani,” anasema.
Magufuli ahutubia taifa
Jumapili mchana, Rais John Magufuli alihutubia taifa na kukumbusha kuhusu umuhimu wa wananchi kujikinga na ugonjwa wa corona, huku akiwatoa hofu kwa kusema ushindi utapatikana.
“Baada ya kuibuka ugonjwa wa corona, serikali ilianza kujipanga kutoa elimu. Nashukuru wizara na vyombo vya habari kwa kushiriki katika kutoa elimu,” anasema Rais Dk. Magufuli.
Anasema serikali iliandaa madaktari kwa ajili ya kukabiliana na ugonjwa huo, iliimarisha ukaguzi wa afya maeneo ya viwanja vya ndege na mipakani.
“Hadi sasa, nchi yetu imethibitika kuwa na wagonjwa 12, huku wanne wakiwa ni kutoka nje ya nchi. Wagonjwa wote wanaendelea vizuri, tunashukuru Mungu bado hatujapata kifo.
“Hata mgonjwa wetu wa kwanza leo ameonekana hana ugonjwa,” anasema.
Rais Magufuli anasema serikali imeunda kamati maalumu kukabiliana na ugonjwa huo ikiwa chini ya waziri mkuu na kwamba kuanzia sasa wasafiri wote wanaoingia nchini watatengwa kwa siku 14 kwa gharama zao.
Pia ameitaka Wizara ya Afya kuboresha maabara na vituo vya kuhudumia wagonjwa huku akielekeza vyombo vya usalama kuimarisha ulinzi mipakani.
Anasema vibali vya safari za nje kwa sasa vimesitishwa huku akiwataka wananchi waliopo katika maeneo ambayo mikusanyiko haiepukiki kama nyumba za ibada, hospitali na makambini kuchukua tahadhari stahiki kujikinga na corona.
“Nawasihi Watanzania kuacha utani na mzaha juu ya ugonjwa huu. Watu watakaobainika wachukuliwe hatua. Nawasihi kuepuka hofu zisizo na msingi. Kama tukifuata ushauri wa wataalamu, tutamshinda adui huyu kama tulivyowashinda maadui wengine,” anasema Rais Magufuli huku akitoa rai kwa wananchi kuendelea kuchapa kazi ili kulinda uchumi wa taifa.