Vita sasa ni kusaka chanjo
Miezi mitatu baada ya virusi vya corona kuibuka nchini China na kusambaa duniani kote, wanasayansi hivi sasa wamejikita katika kutafuta chanjo ya ugonjwa huo.
Tayari majaribio ya chanjo hiyo kwa binadamu yameanza wiki iliyopita katika maeneo mbalimbali. Taasisi moja huko Marekani na taasisi nyingine Ulaya zilitangaza kuanza majaribio hayo na China nayo ilishaanza kufanya majaribio hayo kitambo.
Hata hivyo, kwa mujibu wa utaratibu wa kisayansi, itachukua hadi miezi 18 kabla chanjo hiyo haijathibitishwa kuwa salama kutumika.
Ingawa kwa upande mmoja inaonekana kuwa wanasayansi ‘wanakimbizana’ kutafuta chanjo kama njia ya kuokoa watu wasiendelee kufa, lakini kwa upande mwingine ‘mashindano’ hayo yanachochewa na hamu ya wataalamu hao kuwa wa kwanza kupata haki miliki ya chanjo hiyo.
Huko China wanasayansi 1,000 wanafanya kazi ya kutafuta chanjo hiyo na tayari wameshapiga hatua kubwa. Wataalamu katika taasisi ya Academy of Military Medical Sciences, tayari wameshapata chanjo ambayo imeshaanza kuonyesha mafanikio makubwa na sasa wameshaanza kuwatumia watu kufanya majaribio.
“China haiwezi ikawa nyuma ya nchi nyingine,” anasema Wang Junzhi, mtaalamu wa baiolojia katika chuo kikuu kimoja cha afya nchini humo.
Hata hivyo, kumekuwa na propaganda nyuma ya juhudi hizo, kwani picha iliyosambaa mitandaoni ikimuonyesha Chen Wei, akichomwa chanjo hiyo imebainika kuwa ni ya uongo.
Picha hiyo ilipigwa zamani kabla mwanamke huyo hajaenda Wuhan, jimbo ambalo ugonjwa huu ulianzia.