Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekataa katakata wito uliotolewa na Umoja wa Afrika (AU) kucheleweshwa kutangazwa kwa matokeo ya uchaguzi wa urais.
AU wanasema kuwa wana wasiwasi mkubwa kuhusu uadilifu wa matokeo ya mapema ambayo yalimpatia ushindi, Felix Tshisekedi.
Kiongozoi mwingine wa upinzani, Martin Fayulu, ameitaka mahakama ya kikatiba kufutilia mbali matokeo hayo akidai kwamba ndiye mshindi wa uchaguzi huo.
DR Congo imetakiwa kuchelewesha matokeo ya uchaguzi. Ni wazi kwamba wito wa AU wa kufutilia mbali matokeo hayo umeikasirisha serikali.
Msemaji wa Serikali, Lambert Mende, amesema kuwa mahakama ya kikatiba ilikuwa huru na hakuna mtu mwenye haki ya kuielekeza.
Mwenyekiti wa AU, Rais wa Rwanda, Paul Kagame na viongozi wengine wataelekea Kinshasa kutafuta suluhu ya mgogoro huo.
Mende amesema ujumbe huo unakaribishwa, lakini akasisitiza kuwa matokeo hayo ya baada ya uchaguzi hayatabadilishwa.
Hiyo inamaanisha kwamba kuapishwa kwa Felix Tshisekedi kutafanyika katika kipindi cha siku chache zijazo iwapo mahakama ya kikatiba itaunga mkono ushindi wake.
Awali AU iliitaka DRC kuahirisha kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu. Muungano huo unaonuia kuhimiza umoja na demokrasia, unasema una “shaka kubwa” kuhusu matokeo ya awali yaliyotangazwa wiki iliyopita.
Matokeo hayo yalimpa ushindi mgombea wa upinzani, Felix Tshisekedi, lakini mpinzani wa utawala uliopo, Martin Fayulu, anasisitiza kuwa yeye ndiye aliyeshinda.
Kumezushwa maswali mengi kuhusu uhakika wa matokeo hayo huku zikiwepo shutuma kwamba Tshisekedi anapanga mpango wa kugawana madaraka na Rais anayeondoka, Joseph Kabila.
Baadhi ya viongozi katika Umoja wa Afrika na serikali walikutana katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa Alhamisi na kutoa tamko kuhusu uchaguzi huo wa Desemba 30 unaopingwa na nchi za kigeni ikiwamo Ufaransa.
“Kumekuwa na shaka kubwa kuhusu namna matokeo ya awali yalivyokusanywa, kama ilivyotangazwa na Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi kwa kura zilizopigwa,” taarifa ya umoja huo imesema.
“Kadhalika, AU imetaka kuahirishwa kutangazwa kwa matokeo ya mwisho ya uchaguzi mkuu huo,” iliongeza taarifa.
Fayulu anatuhumu kwamba ushindi wa Tshisekedi alikubaliana na rais anayeondoka madarakani Joseph Kabila.
Kabila amekuwa rais kwa miaka 18 na matokeo, iwapo yatathibitishwa, yataidhinisha kukabidhi madaraka kwa uongozi kwa mpangilio tangu taifa hilo lipate uhuru kutoka kwa Ubelgiji mwaka 1960.
Tume ya uchaguzi imesema Tshisekedi alishinda kwa 38.5% ya kura, ikilinganishwa na 34.7% alizoshinda Fayulu. Mgombea wa muungano wa serikali, Emmanuel Shadary, alipata 23.8%.