Nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo na waasi wa M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, siku ya Jumatano waliahidi katika taarifa iliyotolewa baada ya mazungumzo nchini Qatar kutafuta amani baada ya ghasia kupamba moto mwezi Januari huko Mashariki mwa Congo, na kuzusha hofu ya vita vya kikanda.
Makubaliano hayo yameibua mwanga wa matumaini kwamba ghasia huenda zikapungua.
Kila upande ulitoa taarifa kivyake baada ya wajumbe wao kuondoka Qatar mapema wiki, kufuatia majadiliano ya zaidi ya wiki moja.
“Pande zote mbili zinathibitisha dhamira yao ya kusitisha uhasama mara moja, kukataa matamshi yoyote ya chuki, vitisho, na kutoa wito kwa jamii kutekeleza ahadi hizi,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo ilielezea mazungumzo yao kuwa ya “ukweli na yenye kujenga,” lakini haijafahamika ni lini duru nyingine ya mazungumzo itafanyika.
Kundi la M23 limesonga mbele na kuteka miji miwili mikubwa mashariki mwa Congo katika vurugu ambazo zimeua maelfu ya watu na kuzusha hofu ya kutokea kwa vita vya kikanda.
Mazungumzo ya amani ya Qatar yanakuja baada ya nchi hiyo ya Ghuba kufanikisha mkutano wa mwezi uliopita kati ya Rais wa Congo, Felix Tshisekedi na Rais wa Rwanda, Paul Kagame. Viongozi wote wawili walitoa wito wa kusitishwa kwa mapigano baada ya mkutano huo.
Kikao hicho kinaonekana kilifungua njia kuelekea mazungumzo ya moja kwa moja kati ya Congo na M23. Congo ilikataa kwa muda mrefu wazo la kufanya mazungumzo na M23, na kulitaja kundi kuwa la kigaidi.
Rwanda kwa upande wake imekanusha kwa muda mrefu kuisaidia M23, ikisema vikosi vyake ni kwa ajili ya ulinzi dhidi ya jeshi la Congo na wanamgambo wa Kihutu wanaohusishwa na mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 yaliyoua takriban watu milioni 1, wengi wao wakiwa Watutsi.
