Na Nizar K Visram

Jumanne Aprili 6, mwaka huu, Blaise Compaoré, Rais wa zamani wa Burkina Faso, amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa mauaji ya Thomas Sankara, rais wa nchi hiyo aliyeuawa Oktoba 1987.

Hukumu ilitolewa na mahakama ya kijeshi katika mji mkuu wa nchi hiyo, Ouagadougou, na imehitimisha kesi ya mauaji ya Sankara ambayo ilianza kusikilizwa miezi sita iliyopita. Compaoré aliyekuwa komredi wa Sankara, alishitakiwa pamoja na watu wengine 14.  

Mmojawapo ni daktari aliyeshitakiwa kwa kusaini cheti akisema Sankara alikufa kifo cha kawaida. Compaoré hakuwa mahakamani kwa sababu amekimbilia Ivory Coast baada ya kupinduliwa na wananchi mwaka 2014. 

Mahakamani alikuwapo Mariam, mjani wa Kapteni Sankara, ambaye amesema hatimaye haki imetendeka na majaji wametekeleza wajibu wao. Hata hivyo, amesema ingekuwa vizuri kama Compaoré angekuwepo mahakamani. 

Kesi hii chanzo chake ni kampeni iliyoanzishwa mwaka 1997 na asasi ya kimataifa iitwayo ‘Haki kwa Sankara’ (Justice for Sankara) ikiwa na lengo la kuwawajibisha wauaji wake. Walianza kampeni yao nchini Burkina Faso lakini wakati huo mahakama ilikuwa imetekwa nyara. 

Hata hivyo, harakati ziliendelea hadi mwaka 2013 asasi hiyo ikawasilisha kesi katika Bunge la Ufaransa, ikijenga hoja kuwa Ufaransa ilihusika katika kuuawa na kupinduliwa kwa Sankara, kwa hiyo inawajibika kufanya uchunguzi.

Kwa vile Burkina Faso ilikuwa ikitawaliwa na Compaore, hakuna hatua iliyochukuliwa, lakini mara tu Compaore alipopinduliwa hatua zikaanza kuchukuliwa. Mwili wa Sankara ukafukuliwa na kesi ikafunguliwa mahakamani.  Mwili wake ukaonekana umejaa risasi.

Sankara na wenzake 12 waliuawa kwa kumiminiwa risasi. Baada ya hapo wasaliti waligombea madaraka na matokeo yake urais ukachukuliwa na Compaoré aliyekuwa mwandani wa Sankara. 

Sankara alikuwa mwanamapinduzi na mwanamajumui wa Afrika aliyeamini kuwa mali asili za Burkina Faso zinapaswa kuwanufaisha wananchi badala ya kuporwa na kampuni za kibeberu kutoka Ufaransa na kwingineko.  

Ufaransa ikamtumia kibaraka wake, Fêlix Houphouët-Boigny, aliyekuwa Rais wa Ivory Coast, kumuondoa Sankara. Compaoré aliyekuwa mshauri mkuu wa Sankara alifanya kazi hiyo. Zawadi yake akiwa kukalia kiti cha urais kwa miaka 27 hadi 2014 wananchi wenye hasira walipomtimua na akakimbilia kwa Houphouët-Boigny.

Wakati wa utawala wake, Compaoré aligeuza sera za Sankara kwa kubinafsisha migodi ya dhahabu. Kampuni za kigeni zikaruhusiwa kuchukua madini kwa bei ya kutupwa. 

Mwaka 2014 akapinduliwa na mwaka 2015 uchunguzi ukaanza. Mwaka uliofuata serikali ya Burkina Faso ikatoa hati ya kimataifa ya kumkamata Compaoré na kumfikisha mahakamani. Serikali ya Ivory Coast ilikataa kumrejesha kwa kisingizio kuwa sasa yeye ni raia wa Ivory Coast. Hata hivyo akafunguliwa mashitaka akiwa nje ya nchi. 

Thomas Sankara aliingia madarakani mwaka 1983 baada ya vurugu za kijeshi, akiwa kapteni katika jeshi la ulinzi. Akiwa na umri wa miaka 33 alikuwa rais mwenye umri mdogo kuliko wote barani Afrika. Alipewa jina la ‘Che Guevara wa Afrika’, akiwa na lengo la kufuta fikra za kikoloni, kukomesha ukandamizaji na kuifanya Burkina Faso iwe nchi huru.

Mwamajimui huyo wa Afrika ambaye aliingia madarakani mwaka 1983, aliuawa akiwa na umri wa miaka 37, akiwa kikaoni pamoja na maofisa wengine wa serikali. Kabla ya hapo alikuwa amefika ofisini kwake akitumia gari lake aina ya Peugeot 205.

Katika uongozi wake wa miaka minne, alijaribu kubadili mfumo kwa kugawa ardhi kwa wakulima maskini pamoja na kutoa huduma za kijamii kama elimu na matibabu bila malipo. Akapiga marufuku ukeketaji wakati akitoa fursa sawa za uongozi kwa wanawake. 

Alipinga sera za kikoloni mambo-leo, hasa sera ya Ufaransa ya kuyakandamiza na kuyanyonya makoloni yake ya zamani (France-Afrique). Alipinga pia sera za kinyonyaji kupitia ‘misaada’ ya kigeni inayotolewa na mashirika ya kimataifa, akisema ‘misaada’ hiyo ni mtego kwa nchi za Kiafrika.

Akabadili jina la nchi yake kutoka jina la kikoloni la Upper Volta na kuwa Burkina Faso, ikiwa na maana ya ‘nchi ya watu wenye maadili’.

Almuradi alikuwa Rais mwenye dira, maono na mwelekeo wa kitaifa. Msimamo huu ulimfanya aungwe mkono barani Afrika na kwingineko. 

Sankara alielewa jinsi mfumo wa unyonyaji wa kimataifa unavyoendeshwa. Alipokuwa akiuhutubia mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa (UN) mwaka 1984, alisema ni ‘jasho na damu ya Afrika’ ndiyo iliyojenga mfumo wa kibepari huko Ulaya. 

“Matokeo yake ni kuminya maendeleo ya Afrika na kulifanya bara hili liwe tegemezi na ombaomba,” akasema Kapteni Sankara.

Si tu aliyasema haya bali aliyatekeleza akiwa Rais wa Burkina Faso. Hakuruhusu kampuni za kigeni kumiliki ardhi na migodi. Alikataa masharti ya mikopo. Akataka nchi tajiri zifute madeni yao kwa nchi za Kiafrika. Akatumia mapato ya ndani kuwapatia wananchi wa Burkina Faso elimu na matibabu bila malipo na nyumba kwa bei nafuu. 

Aliwahamasisha wananchi wakapanda miche milioni 10 ili kuzuia mmomonyoko na ukame. Operesheni iitwayo ‘Alpha Commando’ ilieneza elimu ya kusoma na kuandika vijijini. Kwa kushirikiana na UN ugonjwa wa upofu wa mto ukadhibitiwa. Akahakikisha kuwa kila mwananchi anapata angalau milo miwili kwa siku pamoja na maji safi na salama.  

Novemba 1984, alianzisha kikosi cha chanjo (Vaccination Commando). Katika muda wa siku 15 tu watoto milioni 2.5 wakapata chanjo za surua, uti wa mgongo na homa ya manjano. 

Vifo vya watoto vikapungua. Operesheni hiyo ilipata mafanikio mpaka wazazi wa nchi za jirani kama Ivory Coast na Mali wakawapeleka watoto wao Burkina Faso kupata chanjo hizo bila malipo.

Ndipo mfano wake ukawa tishio kwa watawala wa nchi za jirani na kwingineko. Ufaransa ikachukia sana sera yake ya kujitoa kutoka ukoloni mambo-leo pamoja na urafiki wake na Libya na Cuba. Ndipo wakapanga njama za kumpindua. 

Mfano mwingine alioonyesha ni jinsi kiongozi anavyoheshimu wananchi  kwa kuishi maisha ya kawaida. Alichukua mshahara wa dola 462 kila mwezi. Mali zake binafsi alizokuwa nazo ni gari moja, baiskeli nne, magitaa matatu na jokofu moja.Ofisini kwake alikataa kuwekewa viyoyozi.   

Burkina Faso ni miongoni mwa nchi za Afrika zinazoongoza katika uzalishaji wa dhahabu. Asilimia 60 ya biashara yake inategemea dhahabu ambayo inadhibitiwa na Kampuni za Canada kama High River Gold, Barrick Gold, Iamgold Corporation, Tajiri, Roxgold, Nexus na Semafo. Baada ya kuuawa kwa Sankara, kampuni hizi zilishirikiana sana na utawala wa Compaoré. 

Kampuni hizi pia zinamiliki dhahabu ya dola bilioni 2.5 nchini Burkina Faso wakati asilimia 40 ya watu wake leo wanaishi maisha ya ufukara na njaa inazidi kuongezeka. Mwaka 2020 mpango wa chakula duniani (WFP) uliripoti kuwa mamilioni ya wananchi wa Burkina Faso wanakabiliwa na njaa.

Mwaka 2016 Burkina Faso ilizalisha dhahabu takriban tani 60 lakini kodi iliyolipwa ni dola milioni 407. Inakisiwa serikali inakusanya asilimia tano tu ya thamani ya dhahabu inayochukuliwa. Sehemu kubwa inatoroshwa nje ya nchi bila ya kulipiwa kodi. 

Mwaka 1987 Umoja wa Afrika ulifanya mkutano wa kilele mjini Addis Ababa ambako wakuu wa Afrika walihudhuria. Sankara alifika akiwa amevaa nguo za khaki. Akatoa hotuba yake ambayo ikawa ndiyo ya mwisho kabla ya kuuawa.

Akawaambia watawala wa Afrika kuwa deni la Afrika halilipiki na halipaswi kulipwa. Kwanza alisema wakopeshaji wamekwisha kuchuma fedha za kutosha, hivyo hawatapata hasara iwapo hatutalipa. Lakini tukilipa basi watu wetu watakufa.

Akasema kwa njia ya kutabiri: “Afrika lazima ichukue msimamo wa pamoja, kwani iwapo Burkina Faso ikikataa kulipa peke yake, mkutano ujao mimi sitabaki madarakani na sitahudhuria mkutano huu.”  

Miezi mitatu baada ya kusema hayo, kina Compaoré wakamuua!

[email protected]