Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Pwani
MKOA wa Pwani unatarajia kuandaa mbio za Coast City Marathon zinazotarajiwa kufanyika Novemba 30, 2024, zikiwa na lengo la kuchangia maendeleo ya miundombinu ya Shule ya Msingi Pangani iliyopo katika Halmashauri ya Mji Kibaha.
Huu utakuwa mwaka wa tatu mfululizo kwa mbio hizi kufanyika, ambapo zinachagiza kukuza sekta ya michezo na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kutatua changamoto mbalimbali kwenye jamii.
Akizindua vifaa vya michezo vitakavyotumika katika mbio hizo, kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kibaha, Theresia Kiala alisema michezo ni muhimu kwa afya na kusaidia kuinua vipaji vya kukimbia.
“Mbio ni afya, zinaimarisha mwili na kupitia mbio hizi tunachangia juhudi za Serikali kuboresha miundombinu katika sekta ya elimu,” alieleza Theresia.
Awali, Mwenyekiti wa Coast City Marathon, Dkt. Frank Muhamba alitaja kuwa wadhamini wa mbio hizo ni pamoja na Tigo, Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), CRDB, Tumbi Hospital, Wajenzi na Davis & Shirtliff.
Naye Balozi wa Coast City Marathon, Twaha Ambiere, aliwahamasisha watu kujitokeza kwa wingi kujisajili. Alieleza kuwa kiingilio kitakuwa Shilingi 35,000, ambapo kila mshiriki atapata kifurushi chenye fulana, medali, na huduma za barabarani kama maji, juisi ya madafu, na pweza.
“Mbio hizi zitahusisha umbali wa kilometa 5, kilometa 10, kilometa 15, na kilometa 21, huku watoto wakishiriki mbio za kilometa 2.5,” alifafanua Ambiere.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa NSSF Mkoa wa Pwani, Hafsa Ally, alisema NSSF ni mdau mkubwa wa mbio hizo kwa kuwa inashiriki kwa mara ya tatu kutokana na mchango wake katika maendeleo ya jamii.