Korosho ni moja ya mazao makuu ya biashara nchini. Kwa sasa zao hili hulimwa zaidi mikoa ya Kusini mwa Tanzania, yaani Lindi na Mtwara ikifuatiwa na Mkoa wa Ruvuma, Pwani na Tanga.
Takwimu kutoka Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) zinathibitisha umuhimu wa zao hilo kwa Taifa, ambapo katika msimu wa 2012/13 zao hilo liliiingizia Serikali kiasi cha Sh bilioni 29.5 kutokana na ushuru wa usafirishaji wa korosho ghafi nje ya nchi.
Pamoja na zao hilo kuwa sehemu ya mhimili mkubwa wa uchumi wa wakulima na Taifa kwa ujumla, bado uzalishaji wake umekuwa ukikabiliwa na vikwazo vingi ukiwamo ukosefu wa pembejeo, kutopatikana kwa wakati na bei juu zinapopatika. Pembejeo hizo ni pamoja na dawa za kutibu, kukinga magonjwa na wadudu waharibifu wa zao hilo na zana zake zikiwamo mashine za kupuliza dawa.
Kikwazo kingine ni wakulima kutokuwa na teknolojia bora ya uzalishaji wa zao hilo, hali inayowalazimu wazalishe zao hilo kwa mazoea, hivyo kuathiri maendeleo yake.
Kutokana na hali hiyo, wadau wa kilimo cha korosho nchini waliona haja ya kuanzisha Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza Korosho (CIDTF) uweze, kwa kushirikiana na wadau wengine, kutatua matatizo hayo.
Katibu Mtendaji wa Mfuko huo, Suleiman Lenga, anasema lengo la kuanzishwa kwa mfuko huo ni kuinua na kugharimia maendeleo ya sekta ndogo ya kilimo cha korosho ambayo ni pamoja na utafiti, uzalishaji wa miche bora, kilimo bora, huduma za ugani, ubanguaji wa korosho na usindikaji wa bidhaa za korosho.
“Kwa kushirikiana na Kituo cha Utafiti wa Mazao na Maendeleo Naliendele, Mfuko unataka kila penye hali ya hewa na ardhi inayostawisha korosho nchini ilimwe zao hili kwa maslahi ya wakulima, Taifa na hata mazingira yetu,” anasema Lenga na kuongeza:
‘‘Ili kuvutia wakulima wengi kulima zao hili, kwa sasa tunatupia jicho masoko ya ndani na nje, pamoja na ununuaji na usambazaji wa pembejeo na viuatilifu vinavyotumika katika sekta ya korosho. Majukumu haya yameanza kutekelezwa mwaka 2011 ulipoanzishwa mfuko.’’
Anasema kikwazo kikubwa kilikuwa ni kutopatikana kwa wakati kwa pembejeo, tatizo ambalo anasema lilipata tiba wakati wa msimu wa 2013/14 ili kuhakikisha tija na uzalishaji wa korosho unafikia kilo 10 hadi 15 kwa mkorosho.
‘‘Hadi kufikia Julai 31, mwaka huu, jumla ya tani 6,512 za salfa ya unga, tani 21,692 za salfa ya maji, lita 61,914 za viuatilifu vya maji na lita 30,142 za viuatilifu vya kuua wadudu vilikuwa vimesambazwa kwa mfumo wa ruzuku ambapo mkulima alipatiwa pembejeo hizo kwa nusu bei,” anabainisha katibu huyo.
Mkulima wa Kijiji cha Mchauru, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara, Rashid Mtingala, anakiri kupokea pembejeo za ruzuku kwa wakati tofauti na misimu iliyopita, hali ambayo anasema inaweza kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
‘‘Mwaka huu ni ajabu kabisa kuona tumepata pembejeo za korosho kwa wakati na bei ya ruzuku ya Serikali… sina sababu ya kutoupongeza Mfuko kwa utendaji unaoonesha kumjali mkulima,’’ amesema Mtingala.
Mkulima mwingine wa Kijiji cha Mtakuja mkoani Tanga, Juma Keno, anasema, ‘‘Pembejeo tumezipata kwa wakati msimu huu wa kilimo, sasa walau watendaji wa Mfuko wameonesha usomi wao… kama nijuavyo mimi, sifa ya msomi ni kutenda jambo kwa wakati mwafaka.”
Lenga anasema kuwa katika msimu wa 2012/13, Mfuko kwa kushirikiana na watafiti wa Kituo cha Utafiti wa Mazao Naliendele, ulitoa mafunzo kwa maofisa ugani 916 wa wilaya zote zinazolima korosho nchini.
“Mafunzo kama hayo yamefanyika Julai mwaka huu, ambapo maafisa ugani 140, wakulima 340, wapuliziaji 170 na wataalamu maalum wa korosho 30 walinufaika… Mpango huu utaendelea mwaka kesho,” anaeleza Lenga na kuongeza:
“Kuhusu kilimo na matumizi ya mbegu bora katika msimu wa 2012/13, Mfuko ulisambaza kilo 9,500 za mbegu bora na miche 30,000 ya mikorosho iliyobebeshwa kwa wakulima wa wilaya za Tunduru, Mbinga, Namtumbo, Mkuranga, Kibaha, Kisarawe, Mpwapwa, Kongwa, Kilosa, Singida, Kyela na Songea. Mpango ni endelevu.”
Mtafiti Kiongozi wa zao la korosho nchini, Dk. Peter Masawe, anasema mafunzo yaliyotolewa na Utafiti wa Mazao Naliendele kwa maafisa ugani na wakulima, yalilenga kuwapatia teknolojia sahihi za uzalishaji wa zao hilo ambazo ni matunda ya kazi za watafiti wa zao hilo.
“Tunazo teknolojia nyingi sana za uzalishaji wa korosho kama upuliziaji, ubebeshaji, upogoleaji na zingine nyingi… watafiti wanaendelea kufanyia utafiti maeneo mapya ya uzalishaji wa zao la korosho nchini, tayari mikoa ya Dodoma, Singida, Mbeya, Morogoro na Iringa tumebaini kuwa inaweza kulima korosho,” anabainisha Dk. Masawe.
Anaongeza; “Kwa mfano, maeneo ya Kanda ya Kati na Kaskazini watapata kuni baada ya kuipogolea, watapata kivuli, watapata chakula cha mifugo kutokana na mabibo, lakini pia watahifadhi mazingira, ingawa lengo kuu ni kuongeza kipato cha mkulima… tunataka kila penye hali ya hewa na udongo unaostawisha korosho basi ilimwe.”
Mkazi wa Kijiji cha Rahaleo wilayani Mkinga, Fahari Mpongole, ambaye ni mkulima na mpuliziaji wa korosho, anasema mafunzo ya upuliziaji bora yamewajengea uwezo wa kupulizia mikorosho kwa kuzingatia utaalamu badala ya mazoea, hivyo kuongeza uzalishaji.
“Nilipata mafunzo kutoka Utafiti wa Mazao Naliendele ya upuliziaji bora wa mikorosho. Kwa kweli kuna tofauti kubwa na nilivyokuwa nafanya zamani, sasa najua ni wakati gani wa kupulizia, namna ya kuendesha hii mashine na hata uchanganyaji wa dawa,” anasema.
Akizungumzia soko kwa wilaya mpya zinazolima korosho, Lenga anasema msimu uliopita Mfuko ulinunua tani nane za korosho kutoka kwa wakulima na kuziuza kwa wabanguaji wa ndani kwa lengo la kuhimiza na kuhamasisha ubanguaji.
“Mfuko umewezesha viwanda vya DEMROS cha Tanga na Southern Jumbo cha Dar es Salaam kununua korosho za kubangua kwa kuviwezesha viwanda hivyo mitaji na wakati huo huo kuwapatia ajira wanawake na vijana, ikiwa ni utekelezaji wa mkakati wa uhamasishaji wa ubanguaji wa ndani,” anafafanua Lenga.
Anasema, hata hivyo, Mfuko unalenga kujenga viwanda vitatu vya kubangua korosho kwa kushirikiana na wawekezaji wengine wa ndani na nje katika maeneo ya Mtwara, Mkuranga na Tunduru vyenye uwezo wa kubangua tani 50,000 kwa mwaka ili kuimarisha mfumo wa soko la ndani.
“Tukiweza kubangua tani 50,000 tutakuwa tumejenga msingi bora wa kukua kwa bei ya zao hili, kwa sasa bei dira ni shilingi 1,000 lakini baada ya viwanda hivi kufanya kazi ni imani yetu kuwa bei itapanda na kuwanufaisha wakulima,’’ anaeleza Lenga.
“Tutajenga maghala mawili yenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 kwa ajili ya kuwezesha utekelezaji wa mfumo mpya wa uuzaji wa korosho kwa utaratibu wa mali pwani (FOB). Pia tutaanzisha mpango wa upandaji mikorosho bora milioni 10 ndani ya miaka mitatu katika maeneo yanayolima korosho kwa wingi na yale mapya,” anabainisha katibu huyo.
Anaeleza kuwa pamoja na mafanikio hayo, bado Mfuko umekuwa ukikabiliwa na matatizo ya ucheleweshwaji wa fedha za ushuru wa usafirishaji korosho ghafi nje ya nchi kutoka Hazina na uaminifu mdogo wa baadhi ya mawakala wa usambazaji wa pembejeo za ruzuku.
“Hawa wakati mwingine huuza pembejeo za ruzuku kwa bei soko, huku ni kumwibia mkulima, na sisi tunafuatilia kwa karibu na tutakapobaini tutachukua hatua kali dhidi yao,” anasema.
Lenga anasema iwapo Mfuko utamaliza changamoto zinazolikabili zao hilo, ni wazi kuwa korosho inaweza kutokomeza umaskini wa kipato kwa wakulima nchini, hivyo ni wajibu wa wadau wengine kuhakikisha wanahamasisha kilimo cha zao hilo la biashara.