Chuo cha Bandari Dar es Salaam kimejiwekea mkakati wa kujenga chuo kikuu kingine kikubwa kitakachohudumia nchi zote zinazozunguka kusini mwa Afrika ifikapo mwaka 2024.

Aidha mikakati mingine ni  kuhakikisha wanaendelea  kuandaa wataalamu  katika sekta ya mafuta na gesi kwani chuo hicho ni chuo cha kimkakati kinachotoa mafunzo mbalimbali ikiwemo kozi za usalama katika sehemu  za kusimamia maswala ya gesi pamoja na wataalamu wanaoendesha dhana  nzito.

Hayo yamesemwa  jijini Arusha na Mkuu wa chuo cha Bandari Dar es Salaam ,  Dk Lufunyo Hussein  wakati wa akizungumza na waandishi wa habari katika maonesho ya mafunzo ya ufundi stadi    yanayoendelea katika viwanja vya  Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.

Dt Lufunyo amesema kuwa ,wamekuwa wakitoa kozi za muda mfupi na muda mrefu katika    kuwaandaa  wataalamu katika maswala ya  mafuta na gesi ambao wamebobea katika kufanya shughuli hizo kwa ufanisi na umakini mkubwa .

Amebainisha kuwa, chuo hicho  ni chuo pekee ambacho kimejengea uwezo Bandari ya Zanzibar na kimekuwa kinafanya nao kazi kwa karibu sana katika maswala mbalimbali.

“Chuo hiki kimejiwekea mikakati ya kuingia mashirikiano na Taasisi za mafunzo katika Bandari  zilizopo nchi za nje lengo kubwa likiwa ni kubadilishana uzoefu.”amesema .

Aidha ameongeza kuwa,tayari wataalamu kutoka Antwerp -Ubelgiji walishakuja kwetu kwa ajili ya kuhamisha  ujuzi wao na maarifa mbalimbali na namna wanavyofanya kazi zao.

Akizungumzia kuhusiana na  uwiano wa wanafunzi wa kike katika chuo hicho amesema idadi ya wanaume ni kubwa kuliko wanawake ambapo wasichana ni asilimia 40 huku wavulana wakiwa ni asilimia 60   kutokana na dhana ya hapo awali kulionekana ubebaji wa mizigo ulikuwa ukitumia nguvu,wakati sasa hivi wanatumia teknolojia maalumu.

Aidha amesema kwa sasa wanawakaribisha wanafunzi wa kike katika kuendesha zana nzito pamoja na kazi zingine za bandari kutokana na sasa shughuli nyingi hufanywa kwa kutumia mitambo.

Aidha ametoa wito kwa vijana kuitumia mitandao vizuri kwa kujifunza maswala mbalimbali ya teknolojia badala ya kuitumia kwa maswala ya tofauti ambayo mwisho wa siku inawaharibia malengo yao.