CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema suala la uwekezaji kwenye bandari si la Rais Samia Suluhu Hassan, lipo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho ya mwaka 2020-2025.

Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo amesema hayo mjini Korogwe, Tanga jana kwenye mkutano wa hadhara wenye lengo la kuelimisha wananchi kuhusu uwekezaji wa bandari.

Hivi karibuni serikali za Tanzania na Dubai zilisaini makubaliano ya kushirikiana uwekezaji katika bandari.

“Mkataba huo una tija, kama usingekuwa na tija tusingekutana hapa leo kuelezana haya, tunajua yaliyopo yana tija kwa wananchi kwa hiyo lazima tupiganie ili kupata matokeo chanya,” amesema Chongolo.

Aliongeza: “Lazima mjue kuwa haya sio maagizo ya Rais Samia, hiki kitabu (Ilani) kiliandikwa mwaka 2020 mama Samia ndio alikuwa rais? Mwenyekiti wa CCM alikuwa yeye? Kiliandikwa na wana-CCM chini ya Rais na Mwenyekiti John Magufuli.”

Chongolo alitaja mambo yaliyotajwa kwenye ilani hiyo kuhusu uwekezaji katika bandari kuwa ni ujenzi wa gati, usimamiaji kupakua mizigo na kuboresha miundombinu ya chuo cha bandari ili kutengeneza wataalamu.

Alihimiza wananchi wasisikilize maneno ya wapinzani kwa kuwa hawafurahishwi na jitihada zinazofanywa na serikali.

“Lakini kikubwa nawasisitiza ni amani, CCM imebeba amani tuitunze amani yetu watu wamevuja jasho kuileta hii amani, angalia wenzetu jirani moto unawaka, tusiache amani ipotee hatuna pa kukimbilia… wenzetu wanapo pa kukimbilia si mnaona miaka michache iliyopita walikimbia,” alisema Chongolo.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo alisema hakuna asiyependa uwekezaji na kwamba kila mtu mwenye akili timamu atahitaji jambo hilo.

“Kutokana na mabadiliko ya wakati tunakubaliana kuwa ni muhimu sekta binafsi ihusishwe katika kujenga uchumi, huko ndipo tulipo,” alisema Profesa Mkumbo.

Aliongeza: “Uwekezaji hata wakulima wanafanya, unalima leo heka moja, kesho unalima ya pili, unanunua mbuzi wa kike leo, kesho unataka apate dume ili mbuzi aendelee kuzaa.

“Huo ni uwekezaji kwa hiyo hata katika nchi ili iendelee kukua lazima tuwe na uwekezaji na unaweza kufanywa na serikali ama sekta binafsi.”

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu alisema Rais Samia ni mama, hivyo anaguswa na shida za wananchi na anataka kuboresha maisha ya Watanzania.

“Sisi wabunge 15 kutoka Tanga tumebariki makubaliano hayo kwa sababu yanaleta tija kwa Watanzania wote na nataka niwaambie, Tanga sisi ni werevu tunajitambua na tuna akili hatutakubali jambo linalokwenda kuboresha maisha yetu likwamishwe,” alisema Ummy.

Mwanasiasa mkongwe nchini, Stephen Wasira alisema Rais Samia hawezi kuuza nchi kama wanavyosema wapinzani na kwamba hayo ni maneno ya kumchonganisha na wananchi.

“Rais Samia amejenga madaraja Tanzania nzima, ameboresha shule sasa watoto wakimaliza darasa la saba wote wanakwenda sekondari na tena wanasoma bure kwanini auze nchi… halafu huyo anayesema nchi imeuzwa yeye sasa mtumwa wa nani mbona yeye bado yupo kama nchi imeuzwa,” alisema Wasira.

Alisema kauli zinazotolewa na wapinzani kuhusu kupinga uwekezaji huo ni siasa za majitaka ambazo hazitawasumbua wana CCM.

“Unajua kuna watu wanautaka urais wa mwaka 2025, wengine wako upinzani hawa walikimbia nchi wakasingizia wanamkimbia Magufuli, Samia amewaita warudi nyumbani wanakuja na siasa za majitaka,” alisema Wasira.

Aliongeza: “Hawa wapinzani Samia aliposhika madaraka walisema hawezi kufika kokote, walisema wanampa miezi sita tu atashindwa, lakini sasa wanamuona yupo anazidi kufanya vizuri.”

Please follow and like us:
Pin Share