Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo ameziagiza Wizara ya Fedha na Wizara ya Tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI) kukutana kumaliza ujenzi wa stendi ya kisasa ya Ngangamfumini Manispaa ya Moshi.
Chongolo ametoa agizo hilo jana wakati alipokuwa akiwahutubia wananchi wa Wilaya ya Moshi katika mkutano wa ndani uliofanyika ukumbi wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, ambapo alisema kuwa ujenzi wa stendi hiyo ulianza mwaka 2018 ukitarajiwa kukamilika mwaka 2020 lakini cha kushangaza mpaka sasa haijakamilika.
“Bado wasafiri wanajibana katika stendi ya zamani huku sababu za kutokamilika kwa stendi mpya ya kisasa zimeenda huku kumerudi hapa kumeenda pale hadithi haisaidii kutatua changamoto kwa wakati naagiza sasa Wizara husika ya Fedha na Tamisemi kaeni chini na kukubaliana namna ya kumaliza ujenzi huu” amesema Katibu Mkuu Chongolo.
Chongolo amesema kuwa, wananchi hawataki maneno na hadithi wanachotaka ni huduma iliyokusudiwa itolewe kwa wakati na tuliahidi kuwajengea stendi ujenzi umeanza fedha zimetolewa sasa ujenzi ukamilike.
Chongolo amezitaka Wizara hizo mbili kuhakikisha stendi hiyo inaondoka kuwa hadithi sasa iwe ni uhalisia wananchi waanze kuitumia mapema iwezekanavyo na kuwaahidi wananchi waliojitokeza katika mkutano huo kulibeba jambo hilo.
“Niwahakikishie jambo hili ninalibeba na kwenda kuzungumza na wahusika na agizo langu najua litawafikia kabla sijafika huko sisi ndio wenye Ilani hatupo tayari mwaka 2025 kuja kuulizwa tena stendi ya Ngangamfumuni nataka stendi hii ikamilike watu waanze kuingia tuanze mipango mingine na sio hadithi ya muda mrefu hiyo ndio kazi.
“Mimi nimepewa dhamana ya kumsaidia Mwenyekiti na yeye kwa dhamana ya kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania hawezi kukubali kuja kukutana na maswali ambayo majibu yake ni rahisi ni utekelezaji tu, niwahakikishie tutashikana mashati huko huko ili waje kutekeleza hili lifike mwisho” amesema.
Amesema kuwa, hawawezi kuwa na miradi ambayo inakaa kwenye makaratasi kwa muda mrefu, inakaa chini bila kutekelezwa kwa muda mrefu hivyo ni lazima kufikisha ukomo ili kuangalia mambo mengine.
“Hili ni wajibu na nalibeba mimi kesho mniulize mimi nitaenda kule kukaa nao na nitaendelea kulisukuma nikiona linanishinda nitapita mpaka kwa Mwenyekiti Ndugu Samia kumwambia watu wako Hawa wananishinda” amesema Katibu Mkuu Chongolo.