Na Mwandishi wetu,JamhuriMedia,Kilolo

Wananchi wa Kijiji cha Uhambingeto, Jimbo la Kilolo mkoani Iringa, wamempokea Katibu Mkuu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM),Daniel Chongolo kupokelewa na wananchi kwa kilio kwa kudai kukwama kwa mradi wa maji.

Kilio hicho kimekuja wakati diwani wa Kata ya Uhambingeto, Tulinumtwa Mlangwa alipokuwa akitoa taarifa ya kukwama mradi huo wa maji wa Uhambingeto unaotekelezwa na Mkandarasi Mshamind Co LTD, kwa gharama ya Bilioni 2.1 huku Bilioni 1.3 zikiwa tayari amekabidhiwa.

Diwani wa Kata ya Uhambingeto Tulinumtwa Mlanga ameshindwa kujizuia na kuangua kilio mbele ya Katibu Mkuu CCM Dainiel Chongolo kutokana na kutokamilika kwa wakati mradi wa maji na kupelekea wananchi kuendelea kutumia maji ya bwawa ambayo siyo safi na salama.

Mlanga amesema kuwa mkandarasi amekuwa mwiba mkubwa kwa wananchi wa kata hiyo na kupelekea chuki kwa chama na Serikali kutokana na ucheleweshwaji wa mradi huo.

“Ndugu katibu mkuu kuna miradi ya maji ambayo iliukuta mradi huo unatekelezwa na imeshakamilika,tunahitaji nguvu ya ziada ili kuokoa afya ya wananchi” amesisitiza Mlanga”

Amesema mkandarasi alifika kijijini hapo kujitambulisha akiahidi mpaka Februari,utakuwa umekamilika.”Lakini alirudi mwezi wa nne akasema watakamilisha mradi huo,wananchi wa Uhambingeto wanachotaka ni maji, wasipopata maji tutarudije 2025?” amesema.

Baada ya kusikia malalamiko hayo,Chongolo alisema “Haiwezekani fedha itolewe na mradi huo ushindwe kukamilika wakati wananchi wanahitaji maji hivyo Waziri wa Maji afike Uhambingeto ndani ya siku kumi ili atoe pole kwa wananchi kwa kuchelewa kwa mradi huu lakini pia atengeneze utaratibu wa wananchi wapate maji.

Kutokana na malalamiko hayo Chongolo ametoa siku 10 kwa Waziri wa Maji,Jumaa Aweso kufika kijiji cha Uhambingeto ili kutatua tatizo hilo ambapo alitaka ifikapo Septemba 30, mwaka huu wananchi wawe wamepata maji.

“Sijaridhishwa na huu mradi,hatuwezi kwenda namna hii,tatizo hapa ni mkandarasi twende tukakae tuchukue hatua. Cha msingi hapani maji,” amesema Chongolo.

Kwa upande wake mbunge wa Kilolo, Justine Nyamoga amesema ameshahangaika kufuatilia mradi huo bila majibu yoyote yale.

“Bei ya maji ya kunywa sasa inafika Sh.5000 kwa ndoo, Serikali ilitenga bajeti lakini mkandarasi ndio tatizo kubwa,” amesema Nyamoga.