Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Daniel Chongolo amefunguka kuhusu upanuzi na uendelezaji wa huduma za bandari Tanzania ambapo amesema mradi huo una manufaa kwa maendeleo ya Taifa huku akisisitiza nchi inapaswa kusimama imara katika masuala ya msingi.
Amesisitiza kuwa mradi huo utaongeza tija kwa ukuaji uchumi wananchi pamoja na ongezeko la ajira katika nyanja mbalimbali hususan sekta ya uchukuzi wa mizigo.
Akizungumza katika siku ya kwanza ya ziara yake wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma jana, Chongolo amekemea baadhi ya watu wenye tabia ya kutaka kusikilizwa kile wanachokisema pekee bila kutoa fursa ya kusikiliza kile wanachoelezwa.
“Mwaka 2000 tuliingia mkataba na TICTS yani leo TICTS wamemaliza tunaweka mwingine imekuwa jambo jipya kama halijawahi kutokea.
Amesisitiza kuwa: “Wakati TICTS wanaingia tulikuwa chini sana kwenye ufanisi, lakini baada ya kuingia tulipandisha ufanisi wakafikia uwezo wao hadi imefika tukasema hapana. Tunataka ufikie kwenye tija zaidi.”
Katibu Mkuu wa CCM ameeleza kuwa baada ya kampuni hiyo kushindwa kufikia lengo ambalo serikali inahitaji, ikaamuliwa itafutwe kampuni nyingine yenye uwezo.
Amesema lengo la serikali ni ifikapo mwaka 2032 mapato yatokanayo na sekta ya bandari yafikie sh. trilioni 26 kiasi ambacho ni sawa na nusu ya bajeti ya nchi ya sh. trilioni 44.
Chongolo ameeleza kuwa fedha hizo zikipatikana zitasaidia kutekeleza shughuli muhimu za maendeleo ya wananchi zikiwemo huduma za maji, nishati, miundombinu na afya.
“Sasa tunatoa makontena 600,000 tunataka kwenda makontena milioni 2.5, tutahitaji maroli zaidi ya mara nne ya kubeba makontena yaliyopo sasa. Lazima serikali iendeleze tabia ya kusikiliza wananchi na wananchi wajenge tabia ya kusikiza serikali. Sio wewe unataka usikilizwe bila kusikiliza,” amesisitiza.
Kuhusu mkataba alisema mkataba kama huo wa makubaliano ulisainiwa mwaka 2016 baina ya serikali ya Tanzania na Uganda kutekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoani Tanga.
“Tulisaini mkataba kama huu mwaka 2016 wa bomba la mafuta, lakini kuna mataifa yakadhani hawa jamaa wakitengeneza bomba wakapata mafuta sisi huku mambo yetu hayatokwenda.
“Tulikuwa na mradi wa umeme Malagalasi, wakasema huu mradi ukitengenezwa kuna samaki maalum ambao hawapatikani mahali popote duniani. Wakifa hao tutakuwa tumeondoa viumbe adimu duniani, umeme tukakosa samaki wapo pale.
Aliongeza kuwa: “Tukiliwa tunataka kujenga Bwawa la Mwalimu Nyerere wakasema unajua hii ipo katika urithi wa dunia, watu wakapiga kelele na wenzetu wakaanza kuingia kwenye hoja hiyo.”
Amesema eneo ambalo limechukuliwa kwa ajili ya mradi wa kufua umeme kwa nguvu ya maji ni dogo kuliko eneo la hifadhi lililotengwa.
“Tumeligusa eneo hata uwezi kuhisi kwamba kuna eneo pale limeguswa, tukawaleza haya maji yana faida kwa wanyama Tembo ambao wamekuwa wakihangaika kutafuta maji ambapo sasa maji watayapata hapa.
“Wananchi kule kwenye vijiji watatumia maji katika kilimo cha mpunga, sasa hivi maji tunayadhibiti na yanakwenda kwa wananchi. Akili za kuambiwa changanya na zakwako, lazima kwenye mambo ya msingi tunatakiwa kusimama imara kama taifa moja,” amesisitiza Katibu wa CCM Mkuu Chongolo.