Na Mwandishi Wetu
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo amepokea malalamiko ya wananchi ambao wanajihusisha na wakulima wa miwa Kilombero mkoani Morogoro ambao wamedai kukosa imani na Kiwanda cha sukari Kilombero kwa jinsi wanavyopima kiwango cha utamu wa miwa wauzayo kiwandani hapo.
Kwa mujibu wa wakulima hao ni kwamba malipo ya fedha yamekuwa yakitolewa kwa utamu wa miwa ,hivyo wamekuwa wakilipwa malipo madomo ambayo yamekuwa yakisababisha malalamiko hayo.
Wametoa malalamiko hayo leo kwa Katibu Mkuu Chongolo ambaye yupo mkoani Morogoro kwa ziara ya kikazi ya siku tisa akiwa ameambatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC )ya Chama Cha Mapinduzi ( CCM) Sophia Mjema ambapo pamoja na kukugua uhai wa Chama wameendelea kusikiliza changamoto na kuzitafutia ufumbuzi.
Akizungumza kwa niaba ya wananchi wa Kilombero, Mbunge wa Kilombero, Abubakar Assenga, amesema changamoto kubwa ni mgogoro baina ya wakulima wa miwa na kiwanda cha Kilombero.
Ameongeza kwamba mgogoro mkubwa umekuwepo kwenye kiwango cha utamu wa muwa (Sucrose), malipo ya mkulima anayekwenda kuuza miwa yake kiwandani hapo yanategemea utamu wa muwa, sasa wakati kupima hakuna mkulima anayepewa fursa ya kujua bali anaambiwa utamu wa muwa ni mdogo na malipo yanakuwa madogo.”Mgogoro huo ni wa muda mrefu na viongozi wengi wamepita, lakini tatizo liko palepale.”
Akizungumza kuhusu malalamiko hayo, Chongolo amemtaka Mkuu wa Mkoa wa Morogoro kutengeneza utaratibu wa kukaa na Vyama vya Ushirika wa Kilimo na Biashara(Amcos), viteue wakulima mmoja mmoja wafundishwe jinsi ya kufahamu upimaji wa kiwango cha utamu wa sukari, ili kuondoa manung’uniko yao.
Katibu mkuu wa CCM Daniel Chongolo kwenye Ziara hiyo ameambatana na Katibu wa halmashauri kuu ya CCM Taifa itikadi na Uenezi Sophia Mjema pamoja na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Oganaizesheni Issa Haji Gavu kwa ajili ya kukagua Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama hicho pamoja na kuzungumza na Makundi mbalimbali.