1-mhandisi mkazi(kulia)Dejene na MagufuliWatawala makini, kwa maana ya wafalme, marais na mawaziri wakuu, huwa na namna ya kuendesha nchi na falme ambazo wao ni vinara.

Kila mfalme, rais na hata waziri mkuu hutafuta njia iliyo bora anayoona inafaa kuendesha nchi yake kwa manufaa ya wananchi.

Katika kufanya hivyo kiongozi aliye makini hubuni kaulimbiu zinazoweza kuhamasisha ili kumsaidia kufanikisha alichokilenga.

Mfano, tunakumbuka Mzee Jomo Kenyatta wa Kenya alivyokuja na kaulimbiu ya ‘Harambee’, hiyo ilikuwa inawahamasisha Wakenya kufanya kazi kwa pamoja na kwa moyo wa kujituma ili kuharakisha maendeleo ya nchi yao.

Mpaka sasa, karibu miaka 40 baada ya kifo cha mwasisi huyo wa taifa la Kenya, bado kaulimbiu hiyo ya harambee inaendelea kutumika ikiwahamasisha Wakenya kufanya kazi kwa pamoja na kwa bidii kuliletea maendeleo taifa lao.

Nchini Zambia  nako, Kenneth Kaunda, mwasisi wa taifa hilo, alikuwa akiwahamasisha Wazambia kwa kaulimbiu ya ‘One Zambia one nation’ yaani Zambia moja taifa moja, ikitumika kuwafanya Wazambia kujiona ni kitu kimoja na kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuiletea maendeleo nchi yao.

Katika nchi ya Malawi, mwasisi wa taifa hilo, Ngwazi Dk. Kamuzu Banda, alikuwa na kaulimbiu ya ‘Kwacha’ yaani kumekucha, ili kuwafanya Wamalawi waamke na kuanza kuchapa kazi.

Tukija hapa nchini kwetu ndipo tunapoona utitiri wa misemo yenye kuwatia hamasa wananchi ili wakaitumikie nchi yao kwa moyo mmoja tangu tunajipatia uhuru. 

Mfano, Uhuru na kazi, Kukata mirija, Kilimo cha kufa na kupona, Kazi ni Maendeleo, Ujamaa na Kujitegemea na kadhalika na kadhalika.

Lakini kuna kipindi ambacho Tanzania imekuwa kama imejisahau, ikafikia mahala ikawa kama vile imepoteza dira na kuanza kuelekea kusikojulikana.

Nchi ambayo mwanzo ilijitambulisha kama nchi ya kijamaa, ikiwa inaamini katika siasa za Ujamaa na Kujitegemea, ikaanza kwenda kibepari na kuamini katika siasa za kila mtu na lwake! Kujitegemea kukaisha na kuanza kuamini katika kuombaomba!

Nchi ikawa haieleweki kama inasonga mbele au inarudi nyuma, kujitegemea kukaisha kila kitu kikawa kinafanywa na kushangiliwa kwa kutanguliza neno ‘kwa hisani ya’. ‘Tunafanya hivi kwa hisani ya Wamarekani’, ‘kwa hisani ya Wajapani’,’ kwa hisani ya Wajerumani’! Ndipo baadhi ya watu wakaanza kujiuliza kwamba ina maana bila hisani ya watu hao Tanzania haiwezi kuwapo? Sababu inaonekana Tanzania ipo kwa hisani ya watu wa mataifa ya nje.

Kwa mwenendo huo si ajabu tunapumua kwa hisani ya watu wa mataifa ya nje! Hiyo ni hatari sana, sababu siku watu hao wakichachamaa na kufuta hisani zao uhai wa Watanzania ni lazima uwe mashakani.

Kwa maana hiyo, Watanzania walikuwa wakiomba wampate kiongozi ambaye angeweza kuwarudishia imani ya kwamba walau wanaweza kujifanyia mambo bila kutegemea sana wahisani.

Hilo ndilo lililokuwa ombi la Watanzania walio wengi kwa Mwenyezi Mungu. Kwamba wampate kiongozi ambaye angeweza kuwafanya walau wakapumua bila ya kuwategemea wahisani, ili ule mtindo wa kwamba tunapumua kwa hisani ya watu wa Marekani upungue au ukome kabisa.

Sasa tumempata kiongozi ambaye anatuhakikishia kwamba hilo la kujiendesha, kwa maana ya kuendesha uhai wetu bila kulazimika kusema (kwa hisani ya) kunawezekana.

Kiongozi huyo ni Rais wa Awamu ya Tano, Dk. John Pombe Joseph Magufuli. Yeye kaja na kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ huku akijiweka sawa kuhakikisha anawashughulikia watu wote waliokuwa wamejigeuza kikwazo katika mustakabali mwema wa nchi yetu, watu ambao walishakuwa kama majipu kwenye mwili wa binadamu.

Na sote tunaelewa kwamba mwili ukishakuwa na majipu utendaji kazi wake ni lazima uwe dhaifu.

Sasa Magufuli yeye kaamua kujitoa mhanga kwamba anayatumbua majipu. Ni kama alivyosema Mwalimu Nyerere wakati wa vita dhidi ya wahujumu uchumi, kwamba watu hao kama walikuwa wanajiona wana serikali yao basi waelewe kwamba kuanzia wakati huo serikali yao ilikuwa imepinduliwa. 

Na ndivyo anavyoonesha Magufuli kwamba watu hao waliokwishakuwa majipu makubwa ndani jamii ya Watanzania, wakijiona wana serikali yao, sasa anayatumbua majipu hayo kuyaonesha kuwa serikali yao imepinduliwa.

Jambo la kushangaza ni kwamba wapo, hasa wapinzani, wanaosema kwamba hilo halifai. Kwamba anachokifanya Magufuli ni kwenda nje ya njia yake. Kwamba ameyachukua hata yale yaliyokuwa yakisemwa na wapinzani! Eti ni bora akasema kwamba anatekeleza sera za upinzani basi.

Sidhani kama hapa kuna cha sera za upinzani. Sababu, kwa mfano, kama sehemu ina uchafu haiwezekani uchafu huo ukaonekana tu kwa wapinzani.

Kwa hiyo, mtu yeyote akiamua kuufagia uchafu huo ionekane amekuwa mpinzani. Kama mpinzani kauona uchafu hata asiyekuwa mpinzani anauona vilevile na anaweza kuusafisha. Lengo ni uchafu utoke, kwa nini mpinzani autumie uchafu kama mtaji wake?

Kama suala ni kuusafisha, basi sehemu ikishakuwa safi hata mpinzani inambidi apongeze, maana uchafu umetoka.

Kwa hiyo, mambo yanayochomekwachomekwa na wapinzani wakidai kwamba Dk. Magufuli anakwenda nje ya njia yake yanapaswa kuangaliwa kwa makini. Sijaona popote alikopotea njia Rais Magufuli. Bado yuko kwenye njia sahihi kulingana na mahitaji yaliyokuwapo katika uendeshaji wa nchi yetu.

Anaposema ‘hapa kazi tu’ maana yake ni kwamba kila aliye kwenye utumishi wa umma anapaswa ajihesabu kwamba anawajibika kufanya kazi ipasavyo, hapa hakuna kuremba.

Afanye kazi kwa lengo la kuitumikia nchi yake kwa maana halisi ya utumishi wa umma. Hicho ndicho kilichokuwa kikitakiwa na wananchi kwa muda mrefu, kinyume chake mtu huyo aachie ngazi ikizingatiwa kwamba katika idadi ya wananchi wanaokaribia milioni 50 wenye uwezo wa kuimudu nafasi hiyo ni wengi sana.

Haileti maana mtu kuwa kwenye nafasi ya utumishi wa umma akaanza kuichezea nafasi aliyopo kwa gharama ya wananchi halafu aachwe tu kuendelea kuwa pale eti kwa kuogopa minong’ono ya wapinzani, atakayejifanya jipu ni lazima atumbuliwe mara moja. Wapinzani wajiepushe na malalamiko yanayogeuka kuwa kama laana – hapa kazi tu.