Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, ametangaza msimamo wa Tanzania kuhusu mgogoro wa mpaka kati ya Taifa letu na Malawi. Kwa mara nyingine, Serikali kupitia kwa Membe imeitaka Malawi, kampuni na makundi mengine, kuacha mara moja kuendelea na shughuli za utafiti wa mafuta na gesi katika Ziwa Nyasa. Kama alivyosema, Malawi wanadai kwamba mpaka wa haki kati ya Tanzania na Malawi ni pwani ya ziwa hilo kwa upande wa Tanzania.
Kwa maneno mengine ni kwamba binadamu ambao kwa miaka mia kadhaa wamekuwa wakitumia maji ya ziwa hilo kwa upande wa Tanzania, sasa hawana haki ya kuyatumia tena bila kibali cha Malawi. Kinachoudhi hapa ni kwamba chokochoko zote hizi zinatokana na mipaka iliyowekwa na wakoloni na watawala majahili wa kikoloni. Mwaka 1884-1885 wakoloni walikutana Berlin, Ujerumani, wakagawana Afrika kana kwamba haikuwa na wenyewe.
Ni kwa mipaka hiyo isiyozingatia uhalisia wa maisha ya Waafrika kwa wakati huo, wakoloni wakaweza kuwaaminisha Wamalawi kuwa ndugu zao walio Tanzania si ndugu wamoja! Wakawafanya Wakurya wa Tanzania wajione si ndugu wamoja na wenzao wa Kenya Wakafanya hivyo hivyo katika mikoa ya Kagera, Kilimanjaro, Arusha, Tanga, na hata Zanzibar ambako sasa kuna “ulevi” wa kuvunja muungano uliowarejesha ndugu pamoja.
Pamoja na ukweli kwamba mipaka ya wakoloni iliwekwa bila kufuata matakwa ya Waafrika, bado mipaka hiyo ni muhimu katika suala zima la utawala wa nchi. Hii inathibitishwa na ukweli kwamba hata kama kabila linakuwa moja, kunakuwapo mipaka ndani ya kabila hilo ! Kwa msimamo wa Malawi ulivyo kuhusu suala hili, tunaona kuna dalili za kuelekea kwenye mapigano. Vita si kitu cha kuomba au kujivunia, hasa kwa mataifa yetu haya ambayo hayana japo uhakika wa kuwalisha wananchi wake.
Tumepigana Vita ya Kagera. Madhara yake bado yanatusumbua miaka 30 baadaye. Vita si jambo la kuliomba. Malawi wanaweza kuwa na kiu ya vita kwa sababu hawajawahi kupigana vita kali iliyowagharimu. Wasidhani kuwa vita ni lelemama.
Kinachopaswa kufanywa na majirani zetu ni kutumia busara tu kutambua kuwa kando ya Ziwa Nyasa wapo binadamu, tena ndugu zao, wanaoihitaji maji ya kunywa, kilimo na kuendesha shughuli zao za kiuchumi. Wawatambue kuwa kabla ya wakoloni kutugawa, hapakuwapo zuio lolote la mtu wa upande mmoja kuyatumia maji ya ziwa hilo kwa upande wake, na hata kwa upande wa pili.
Malawi ni ndugu zetu wa damu. Wanatutegemea kwa mambo mengi. Kama kuna kiburi cha wakubwa (tunaambiwa Uingereza wana kampuni za utafiti mafuta), wajue kuwa mwisho wa siku waathirika ni sisi Waafrika wenyewe. Watatugombanisha wakati wao wakiendelea kuchimba mafuta na gesi yetu (kama kweli vipo).
Lakini Malawi watambue kuwa kama njia za kidiplomasia zitashindikana, hakuna njia nyingine isipokuwa kuikomboa nchi yetu kwa mtutu wa bunduki. Tunaposema kuwa ukubwa wa Tanzania ni kilomita za mraba zaidi ya 945,000 tunamaanisha pamoja na nusu ya Ziwa Nyasa. Ni wakati wa Malawi kutafakari njia sahihi ya kuumaliza mgogoro huu.