China imerudisha ndege ilizoagiza kutoka Marekani ikiwa ni tukio la hivi karibuni la kulipiza kisasi ushuru wa Trump, mkuu wa kampuni ya kutengeneza ndege ya Boeing amesema.

Kelly Ortberg alisema ndege mbili tayari zimerudishwa na nyingine itafuata baada ya mvutano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili kuongezeka.

Afisa mkuu mtendaji wa Boeing aliiambia CNBC kwamba ndege 50 zaidi zilipaswa kwenda China mwaka huu lakini wateja wao walisema hawatazipokea.

Marekani iliweka ushuru wa 145% kwa uagizaji kutoka China huku China ikijibu kwa kuweka ushuru wa 125% kwa bidhaa za kutoka Marekani.

Akizungumza katika Ikulu ya Whitehouse siku ya Jumanne, Trump alisema ana matumaini kuhusu kuboresha uhusiano wa kibiashara na China, akisema kiwango cha ushuru alichoweka “kitashuka sana, lakini hakitakuwa sifuri”.

Hata hivyo, Bw Ortberg alisema China “imeacha kabisa kuagiza ndege kwa sababu ya ushuru” uliowekwa.

Boeing ndio muuzaji mkubwa zaidi wa Marekani na takriban 70% ya mauzo yake ya ndege za kibiashara ni nje ya Marekani.