Na Ruja Masewa, Jamhuru Media

Chama cha Ukombozi wa Umma (CHAUMA) kimesema, Wakurugenzi na Watendaji wa Halmashauri nchini, “Wanatuharibia Uchaguzi“.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mwenezi wa CHAUMA Ipyana Samson Njiku (leo) Aprili 7, 2025 mkoani hapa, wakati akitoa tamko la kutosusia uchaguzi wa Oktoba 2025, kwamba Kitashiriki uchaguzi huo asilimia 100.

Akitoa msimamo wa CHAUMA mbele ya Waandishi wa Habari Ipyana amesema, ” Ni heri Rais Samia Suluhu aongezewe muda hata miaka 10 mbele ili afanye mabadiliko ya Changamoto zinazoharibu uchaguzi nchini ikiwemo Katiba Mpya“.

Aidha Ipyana amevijia juu vyama vyenye Wabunge bungeni kuvidharau vyama vyao vidogo visivyo na Wabunge mjengoni kwani navyo vina usajili halali kama vyao.

Amedai, hakuna kinachowaudhi kama kuambiwa wao ni Mawakala, ni Chawa wanaotumika na Chama cha Mapinduzi (CCM).

Hata hivyo wametoa mapendekezo kadhaa wakidai, wanataka Wakurugenzi wa Halmashauri wasiwe wasimamizi wa uchaguzi kwa sababu wao ni watumishi wa Umma na Makada wa CCM, kwani hawatatenda Haki

Amesema Wasimamizi wa vituo wasiwe watumishi wa Umma, Walimu na Watendaji wa Kata, na mwisho Mawakala wetu wa vyama vya upinzani wasibughudhiwe na wasimamizi wa uchaguzi.

CHAUMA kimetoa wito na kuwakaribisha Wanachama wa vyama vingine wanaotaka kugombea Udiwani, Ubunge na Urais, kwenda kwenye chama chao kuchukua fomu bure bila gharama kama vyama vingine vinavyofanya.

Pamoja na Kauli hiyo, Ipyana amedai, Sera yao ya Ubwabwa na Maendeleo bado ipo palepa na sasa imehamishiwa kwenye shule, vyuo na hospitalini ili kuwaondolea wananchi mzigo wa gharama.