Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma
Zaidi ya wakulima 1000 wa zao la Mbaazi wa wilaya za Chemba na Kondoa Mkoani hapa wameiomba Serikali kuona haja ya kuutazama upya mfumo wa stakabadhi ghalani kwani unakiuka malengo ya kumkomboa mkulima na badala yake umekuwa unawanyonya na kuwafilisi.
Wakulima hao wameeleza kuwa licha ya kulima kwa kujitegemea na kupata mazao mengi hali zao kiuchumi zinabaki kuwa duni kutokana na toza za ushuru wanazotozwa kutoendana na soko lilivyo jambo linalowafanya kunyonywa kwa kigezo cha stakabadhi ghalani.
Hayo yamezungumza leo,Septemba 4,2024 na wakulima hao wakati wakizungumza na Waandishi wa habari Jijini hapa
ambapo wamedai kuwa Serikali ya Mkoa wa Dodoma imewatelekeza na kuendelea kuendesha zoezi la unyang’anyi wa mazao kwa wakulima hao pindi wanapohoji ukiukwaji wa mfumo huo.
Akizungumza kwa niaba ya wakulima wengine,Zabibu Yusufu amesema kuwa wao kama wakulima wanapata hasara kubwa kwani huwalazimu kutoka Kondoa kwenda kuuza mazao Chemba na kwamba toka tarehe 27 mwezi wa nane hadi tarehe 2 mwezi wa tisa ambapo bado wanazuia kuuza mazao yao jambo lililowafanya kuuza kwa Shilingi 1840 badala ya 2060 ambayo ni halali .
“Tikianza kufuata sheria tunakamatwa mfano ni hivi karibuni gari 14 zimekamatwa zikiwa na tani 180 kuna wakulima ambao wamepewa mitaji na wanunuzi ili waweze kulima wapate mazao waje wawauzie wale waliowapa mitaji lakini kuna wengine wamekopa benki na wengine wamekodi gari hawajalipia wengine wanawagonjwa wanawatoto wanataka ada , hii ni zuluma, “anaeleza
Mkulima huyo anaeleza kuwa mbali na kukamatwa kwa mazao yao kuna wakulima wengine wamepigwa na kupelekea kulazwa hospitali jambo linalowarudisha nyuma kwenye mapambano kiuchumi.
“Kuna wengine wamepigwa kuna kijana mmoja hadi sasa amelazwa kwa kupigwa kwa kosa tu la kuchukua picha wakati magari na wakulima wanakamatwa ,haijaishia hapo tu kuna wengine wamebeba mazao kwa malikauli kule vijijini kwasababu mbaazi kwa mkoa wa Dodoma asilimia kubwa wanaolima mbaazi ni Kondoa vijijini lakini wamezuiliwa Chemba ni hasara, “anafafanua na kuongeza;
Tunaiomba Serikali iufumue huu mfumo wa stakabadhi ghalani, unatuumiza mana kila siku watendaji wake wanabuni mbuni mpya za ukandamizaji, ” anaeleza mkulima huyo anayeitwa Zabibu.
Kutokana na hayo Chama Cha Ukombozi wa Umma(CHAUMMA)kimemuomba Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan kuingilia kati suala hilo na kumuomba kuwasaidia wakulima ambao magari waliyokodi kubebea mbaazi kukamatwa mkoani Dodoma kwa vigezo vya kukiuka vigezo vya stakabadhi ghalani.
Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho,Kayumbo Kabutari amedai kuwa Serikali ya Mkoa wa Dodoma imeendesha zoezi hilo kingume na sheria na kufananisha suala hilo kuwa ni unyang’anyi kwani wakulima wamenyanyaswa vya kutosha.
“Jambo hili limekuwa likiwaumiza sana wakulima kwani serikali ya mkoa wa Dodoma imekuwa ikipora na kunyang’anya mazao ya wakulima bila kuangalia athari inayomkuta mkulima na kweli lipo neno stakabadhi ghalani lakini lina utaratibu wake,”amesema Kabutari.
Akirejea vifungu vya sheria ya stakabadhi ghalani,amesema kuwa sheria na.10 ya mwaka 2005 na sheria na.3 ya mwaka 2015 na marekebisho yake ya mwaka 2016 juu ya stakabadhi ghalani imeweka mambo vizuri kabisa ambapo amesema stakabadhi ghalani inaendana sambamba na uanzishaji wa vyama vya ushirika vya wakulima ambapo Dodoma hakuna.
“Sasa leo unapoenda kumuanzishia mtu ghafla aliyehangaika toka kuandaa shamba lake yuko peke yake kazi zote za shamba anazifanya mkulima peke yake kwenye mazao unakuja kumwambia kuna kitu kinaitwa stakabadhi ghalani inakuwa siyo sawa,”amesema Kibutari.
Amesema kuwa lengo la stakabadhi ghalani ni kwajili ya kumsaidia mkulima asipatwe bei ya dira bei ambayo ya mtaani kwamba wanamuanzishia hizi stakabadhi ghalani ili mkulima aweze kunufaika na bei nzuri itakayopatikana.
“Lakini kabla hujafika kwa mkulima lazima awe amewezeshwa kwani moja ya kazi za stakabadhi ghalani ni kusimamia na kuhamasisha matumizi ya mfumo wa stakabadhi ghalani jambo hili serikali ya mkoa wa Dodoma haijafanya.
“Nakatika kusimamia huku kuendane sambamba na uwepo wa vyama vya ushirika visipofanyika hivyo kinachofanyika ni kwenda kuwapora wananchi mazao yao kitu ambacho siyo lengo wala dhamira ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambaye lengo lake kubwa ni kutaka kuwainua wakulima kwenye kilimo siyo kuwakandamiza.,”amesisitiza.
Na Kuongeza “Mfano tarehe 27 mwezi wa nane mwaka huu wakulima wa mbaazi wakiwa wametoka na gari 14 zikiwa na tani zaidi ya 150 zikitoka Kondoa zikiwa na Mazao ya Mbaazi gari 11 na dengu gari 3 wakiwa wametoka Halmashauri ya Kondoa kuchukua ushuru wa hayo mazao wanaleta mjini sokoni na Kondoa hakuna chama cha ushirika wa kukusanya hayo mazao na wanalipa ushuru wa hayo mazao wanaleta sokoni Dodoma mjini wanafika Chemba wakulima wanakamatwa wanaambiwa stakabadhi ghalani.
“Magari yazuiliwa ambapo siku hiyo bei ya soko ilikuwa kilo moja ya mbaazi ilikuwa 2060 lakini yakazuiliwa Chemba na wanatoka Kondoa Halmashauri nyingine wanafika Halmashauri nyingine wanazuiliwa waambiwa stakabadhi ghalani,kwanini haikuanzia walipotoka ili wakulima waufahamu na kwanini Halmashauri ya Kondoa isiwazuie wakulima kutoka kondoa,”amesema.
Tarehe 2 mwezi wa 9 kuna mnada umefanyika Chemba kilo imeuzwa kwa 1840 tofauti na bei waliyokuwa wanaitarajia ya 2060 na hawajawalipa wakulima.
“Stakabadhi ghalani inasema pale mnunuzi anapopatikana anatakiwa kulipa pesa yote palepale na mkulima anatakiwa apewe haki yake lakini hadi sasa toka tarehe 2 Septemba mnada umefanyika kwa kilo 1840 badala ya bei waliyokuwa wanaifukuzia ya kilo 2060 mpaka leo mkulima hajapewa hela yake na amekodi gari kuleta mzigo mjini na amlipe mwenye gari huu ni unyanyasaji,”
Aidha ameitaka Serikali ya mkoa wa dodoma wajipange kwabi amedai wanamharibia Rais kazi yake kwani mfumo wa stakabadhi ghalani unaendana na vyama vya ushirika na kanuni inasema katika mfumo wa stakabadhi ghalani malipo yanafanyika katika chama kikuu cha ushirika hayafanyiki kwenye vyama vya msingi na Dodoma hakuna chama cha ushirika.