Wakati mjadala wa bajeti ya Sh trilioni 33 kwa mwaka wa fedha 2019/2020 ukiendelea bungeni, JAMHURI limeelezwa kuwapo kwa chanzo kikubwa kipya cha mapato kilichopuuzwa kwa miaka takriban mitatu.
Wataalamu wa masuala ya soko la mtandaoni wanasema Tanzania ikiwekeza katika uendelezaji wa soko la mtandao, inaweza kupata hadi dola bilioni 10 kama kodi, sawa na Sh trilioni 23.
“Ni bahati mbaya hapa kwetu tumepata hii fursa ya kuanzisha soko la mtandaoni, ila baadhi ya wanasiasa na watoto wa wakubwa wakaingilia mchakato na kuuteka tangu mwaka 2015 tumekwama.
“Nchi kama Marekani, Uingereza na China zinapata mamilioni ya fedha kutoka soko la mtandaoni ila sisi hapa tunachezea fursa,” amesema mmoja wafanyabiashara aliyeomba jina lake lihifadhiwe kwa maelezo kuwa soko la mtandaoni ni vita kubwa.
Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilipitisha muswada wa sheria ya chanzo hicho kipya cha mapato mwezi Mei, mwaka 2015, sheria ikatiwa saini na hata kanuni zimekwisha kutengenezwa.
Chanzo hicho cha mapato kilichopuuzwa kwa miaka hiyo mitatu ni Soko la Kimataifa la Bidhaa la Mtandaoni (Electronic Commodity Exchange), ambalo Tanzania ilikwisha kupata kibali cha kuingia kwenye soko hilo.
Katika soko hilo, bidhaa mbalimbali zinaweza kuuzwa ndani na nje ya nchi katika mazingira ya uwazi, nafuu na yenye tija kwa taifa. Kinachofanyika ni kutoa taarifa za bidhaa husika kwenye mtandao huo uliounganishwa na mitandao mingine mikuu ya masoko duniani.
Kwa Tanzania, na hasa katika kipindi hiki cha bajeti, katika mwaka wa fedha 2019/2020 mabilioni ya fedha yanaweza kupatikana kutoka katika chanzo hiki cha mapato, hivyo kuiongezea nguvu zaidi bajeti ya serikali.
Tanzania ilivyonasa fursa
Ushawishi wa Tanzania hadi kuingizwa kwenye mtandao wa soko hilo ulifanyika mwaka 2011 na Mtanzania aliyeongoza jopo la Watanzania katika uwasilishaji (presentation) maombi ya Tanzania, John Chaggama, na timu yake walishiriki kikamilifu.
Chaggama alikuwa kiongozi wa timu hiyo kwenye mkutano wa Cape Town, 2011 kuiomba Benki ya Dunia, Shirika la Fedha la Kimataifa (IFC), Jukwaa la Uchumi la Dunia (WEF) na jumuiya ya wafadhili kukubali na kuiruhusu Tanzania kupewa kibali kuanzisha soko hilo la mtandao.
Tanzania ndiyo nchi pekee katika Afrika Mashariki iliyopewa kibali hicho baada ya uwasilishaji na utetezi wa maombi ya Tanzania ulioongozwa na John Chaggama, kwa hiyo nchi inaweza kunufaika zaidi endapo itaanza kulitumia soko hilo rasmi.
Manufaa ya soko hilo
Balozi Chaggama amesema mfumo huo wa soko la kimataifa la mtandaoni ni wenye manufaa makubwa kwa taifa hili kama ilivyo kwa nchi nyingine ambazo ni pamoja na India au Marekani.
“Sasa hivi madini yanauzwa kwenye masoko mikoani. Ukisha kuyakusanya na kuyahifadhi Benki Kuu unaweza kuyauza. Kwa mfano, unaitangazia dunia kwamba leo unaweka sokoni kilo 100 za dhahabu, taarifa hizo zikiwamo kwenye mtandao wa soko la kimataifa, ndani ya nchi watakuwa wanafahamu na dunia yote inajua kwamba kuna kiwango fulani cha madini kinauzwa Tanzania.
“Baada ya kuweka taarifa hizo sokoni, anatokea mteja kutoka labda nchini Brazil, ananunua kwa njia hiyo hiyo. Si lazima dhahabu inayonunuliwa itoke ndani ya nchi kwenda nje, kinachofanyika ni kwenda kwenye hifadhi ya Benki Kuu, kufanya derivatives (nyambuo) kwa uangalizi wa nchi kama Balozi wa Brazil, kisha fedha za mhusika zinahamishiwa Benki Kuu kwetu kwa njia ya mtandao na dhahabu inaendelea kubaki pale Benki Kuu tunailinda inaendelea kutulipa pango,” amesema.
Soko la Mauzo ya Bidhaa Mtandaoni la Tanzania ingawa bado halijaanza rasmi, sheria ya uendeshaji wa soko hilo ilikwisha kupitishwa Mei, mwaka 2015.
Bidhaa nyingine zinazoweza kuingizwa kwenye soko hilo kwa mujibu wa kibali cha Tanzania ni pamoja na zile za mazao kama kahawa, korosho, ufuta, mchele, alizeti na mahindi.
Kwa mantiki hiyo, badala ya kumtegemea mnunuzi mmoja, unapata wateja kutoka kila kona ya dunia na unabaki kutengeneza faida ya mamilioni, huku mazao yakiwa kwenye maghala na kila mteja anaponunua anasafirishiwa kiasi anachohitaji hadi aliko.
Bajeti 2019/2020
Sera ya bajeti ya mwaka wa fedha 2019/20 imeeleza kuhusu shabaha za uchumi jumla ambazo ni pamoja na Pato la Taifa kukua kwa asilimia 7.1 mwaka 2019 kutoka ukuaji halisi wa asilimia 7.0 mwaka 2018, na mapato ya ndani kufikia asilimia 15.8 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 14.3 mwaka 2018/19.
Mbali na hayo, vilevile nakisi ya bajeti inakadiriwa kufikia asilimia 2.3 ya Pato la Taifa mwaka 2019/20 kutoka matarajio ya asilimia 2.0 mwaka 2018/19.
Na kwa kuzingatia shabaha, malengo pamoja na sera za bajeti kwa mwaka 2019/20, sura ya bajeti inaonyesha kuwa jumla ya Sh trilioni 33.11 zinatarajiwa kukusanywa na kutumika. Jumla ya mapato ya ndani (ikijumuisha mapato ya halmashauri) yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 23.05, sawa na asilimia 69.6 ya bajeti yote. Kati ya mapato hayo, serikali inalenga kukusanya mapato ya kodi ya jumla ya Sh trilioni 19.10 sawa na asilimia 12.9 ya Pato la Taifa.
Akiwasilisha mapendekezo ya bajeti hiyo, Waziri wa Fedha, Dk. Philip Mpango, amewaambia wabunge kuwa, mapato yasiyo ya kodi kwa mwaka 2019/20 yanatarajiwa kuwa Sh trilioni 3.18 na mapato kutoka vyanzo vya halmashauri ni Sh bilioni 765.5.
“Serikali inatarajia kukopa shilingi trilioni 4.96 kutoka soko la ndani. Kati ya kiasi hicho, Sh trilioni 3.46 ni kwa ajili ya kulipia hatifungani na dhamana za serikali zinazoiva na kiasi cha Sh trilioni 1.50 sawa na asilimia 1.0 ya Pato la Taifa ni mikopo mipya kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.
Kwa lengo la kuongeza kasi katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu, serikali inatarajia kukopa Sh trilioni 2.32 kutoka soko la nje kwa masharti ya kibiashara.
Katika Bajeti hiyo ya Sh trilioni 33, Serikali ya Tanzania imetenga Sh trilioni 12.2 kwa ajili ya kugharamia mpango wa Maendeleo wa Taifa mwaka 2019/2020.
Kati ya fedha hizo Sh trilioni 9.7 ni fedha za ndani na Sh trilioni 2.5 ni fedha za nje. Fedha hizo za maendeleo ni sawa na asilimia 37 ya bajeti yote ya mwaka 2019/2020.
Bajeti hii imeweka msisitizo mkubwa katika kuendeleza ujenzi na ukarabati wa miundombinu hususan reli, bandari, nishati, barabara, madaraja na viwanja vya ndege, pia kutekeleza uboreshaji wa mazingira ya biashara yawe rafiki na yenye gharama nafuu.
Dk. Mpango amesema: “Mheshimiwa Spika, matumizi ya maendeleo yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 12.25, sawa na asilimia 37.0 ya bajeti yote, ambapo kiasi cha shilingi trilioni 9.74 ni fedha za ndani na shilingi trilioni 2.51 ni fedha za nje.
“Kati ya fedha za maendeleo zilizotengwa, shilingi trilioni 2.48 ni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa reli kwa kiwango cha Standard Gauge; shilingi trilioni 1.44 ni kwa ajili ya mradi wa kufua umeme Mto Rufiji; shilingi bilioni 788.8 ni kwa ajili ya mifuko ya Reli, Maji na REA.
“Shilingi bilioni 450 ni kwa ajili ya mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu; na shilingi bilioni 288.5 kwa ajili ya elimu msingi bila ada. Aidha, serikali imetenga jumla ya shilingi bilioni 600.0 kwa ajili ya kulipa madeni yaliyohakikiwa ya watumishi, watoa huduma na makandarasi wa barabara, maji na umeme.”
Bajeti hii imependekeza kufanya marekebisho ya mfumo wa kodi ikiwemo baadhi ya viwango vya kodi, tozo na ada zinazotozwa chini ya sheria mbalimbali na pia taratibu za ukusanyaji na usimamiaji wa mapato. Serikali zamu hii haikuongeza kodi kwenye soda, bia, sigara, vinywaji baridi na mvinyo kama ilivyozoeleka.
Katika sheria ya Kodi ya Ongezeko la Thamani, Dk. Mpango amependekeza kufanya marekebisho kusamehe VAT kwa wakulima wanaoingiza makasha yenye majokofu kwa ajili ya kilimo cha kisasa cha mbogamboga kwa wakulima watakaoingiza makasha hayo kutoka nje.
Pia amependekeza kusamehewa kodi kwa vifaa vya kukausha nafaka ili kuchochea ongezeko la kilimo cha nafaka.
Serikali imependekeza kurekebisha Sura ya 160 ya Sheria ya Usalama Barabarani kuongeza muda wa leseni za udereva kutoka miaka mitatu hadi mitano, na kupandisha malipo ya leseni kutoka Sh 40,000 hadi 70,000.
Lakini pia kuna ongezeko la ada ya usajili wa kadi za gari kutoka Sh 10,000 hadi 50,000, ambapo pikipiki za magurudumu matatu, yaani bajaji kadi ya usajili kwa sasa imefikia Sh 30,000 kutoka Sh 10,000.
Pikipiki za kawaida usajili wa kadi zake umetoka Sh 10,000 hadi Sh 20,000.
Katika masuala ya urembo, serikali imependekeza ongezeko la ushuru wa nywele za bandia uwe asilimia 10 kwa zile zinazotengenezwa ndani ya nchi na asilimia 25 kwa zile zinazotoka nje.
Dk. Mpango amependekeza kupunguza kiwango cha Kodi ya Ongezeko la Thamani kutoka asilimia 18 mpaka asilimia 0 kwenye huduma za umeme unaouzwa kutoka Tanzania Bara kwenda Zanzibar ili kuwapunguzia gharama za maisha wananchi.
Serikali imekusudia kuongeza kasi ya ukusanyaji wa mapato na kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kuwezesha kukamilisha miradi mikubwa kama miundombinu na huduma za jamii.
Kurekebisha viwango vya kodi kwa lengo la kuhamasisha uzalishaji na kulinda viwanda vya ndani dhidi ya ushindani kutoka nje.
Kuboresha mazingira ya kufanya biashara kuvutia wawekezaji na ukuaji wa biashara ndogo na za kati ili kupanua wigo wa kodi na mapato mengine ya serikali.
Kuboresha mazingira ya ulipaji kodi kwa hiyari ili kupanua wigo wa kodi na matumizi ya TEHAMA katika usimamizi wa kodi.
Kuimarisha usimamizi wa sheria za kodi ili kutatua changamoto za ukwepaji kodi na kupunguza upotevu wa mapato pamoja na kuweka mkazo zaidi katika kutoa elimu kwa mlipa kodi.
Kuimarisha makusanyo yasiyo ya kodi kwa kuhimiza matumizi sahihi ya mifumo ya TEHAMA.
Maoni ya wadau
Miongoni mwa wadau waliozungumzia bajeti ya mwaka ujao wa fedha ni Dk. Omari Mbura ambaye amesema bajeti hii imegusa maeneo mengi yenye masilahi kwa wananchi wa kawaida.
Ameyataja maeneo ambayo yamegusa moja kwa moja wananchi kuwa ni hatua ya kuondolewa tozo kadhaa ambazo zilikuwa chanzo cha kuongeza bei za bidhaa.
Kwa mujibu wa msomi huyo, kutoongezwa kwa kodi katika bidhaa kama vinywaji baridi kunaweza kuchochea ongezeko la wawekezaji kwenye sekta ya vinywaji kwa kuwa hofu ya kodi isiyotabirika haitakuwapo.
Kwa upande wao, baadhi ya wabunge wamesema bajeti kwa namna fulani imepunguza utegemezi, kwa mujibu wa Dk. Raphael Chegeni wa Jimbo la Busega.
Lakini wakati Chegeni akiwa na maoni hayo, Mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi, anasema bajeti hiyo imekuwa katika mizania iliyo sawa, aliyoiita ya kung’ata na kupuliza, huku Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, akisema bajeti hiyo ni nzuri na imeakisi matakwa ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM inayoendelea kutekelezwa sasa na Serikali ya Awamu ya Tano.
Dk. Lucas Katera akizungumzia bajeti hiyo hivi karibuni amesema ni bajeti iliyogusa maisha ya Watanzania wa kawaida.
Akitoa mfano, amesema wafugaji wa kuku na wavuvi wameondolewa tozo za kero zilizokuwa zikitozwa na baadhi ya mamlaka za serikali kama Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania (TFDA) au Mkemia Mkuu wa Serikali.
Kwa upande wake, Profesa Haji Semboja, amesema kuna tofauti kubwa kati ya bajeti ya mwaka ujao wa fedha na bajeti zilizopita.
Amesema bajeti zilizopita zimekuwa ni bajeti za kuongeza ama kupunguza na kwamba hapakuwa na maelewano ya kutosha kati ya serikali na sekta binafsi.
Mwenyekiti wa Kampuni ya Info Tech Investment Group Ltd, Ali Mufuruki, licha ya kusifu bajeti hiyo amesema inaunga mkono wafanyabiashara kwa kuwa imejibu maswali yao mengi.
Akitoa mfano wa maswali hayo, Mufuruki amesema ni pamoja na suala la kurahisisha ulipaji kodi na kupunguza gharama za kufanya biashara nchini, kupunguza kodi katika uingizaji wa vifaa mbalimbali hasa vifaa vya uzalishaji. Amesisitiza kuwa matatizo ya uchumi nchini ambayo yamekuwa yakizungumzwa na sekta binafsi yamepata majibu ndani ya bajeti hii.
Naye Profesa Honest Ngowi amesema hakuna jambo jipya katika bajeti hii, hasa kwa watu waliokuwa wakisoma bajeti za miaka iliyopita.
Hata hivyo, kwa namna fulani amesema katika bajeti hiyo kuna maeneo yanamgusa mwananchi wa kawaida, hasa katika uwekezaji kwenye elimu, afya, miundombinu kama ujenzi wa reli na barabara, lakini hiyo ni hatua moja ya awali, hatua kubwa na muhimu zaidi ni umakini katika utekelezaji wa bajeti hiyo.
Nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki Rwanda, Uganda, Kenya na Tanzania zilifanya makubaliano kusoma bajeti zao kwa pamoja kila mwaka.
Bajeti ya Kenya
Nchini Kenya, wiki iliyopita Waziri wa Fedha, Henry Rotich, amewasilisha makadirio ya bajeti ya dola bilioni 31.5, sawa na Sh trilioni 72.4 za Tanzania kwa mwaka wa 2019/2020 ambayo ni bajeti kubwa zaidi katika historia ya taifa hilo.
Waziri Rotich amesema bajeti hiyo imezingatia “ndoto na azimio” la Rais Uhuru Kenyatta kuwekeza katika sekta nne muhimu ili kuliendeleza taifa la Kenya.
Sekta alizoamua kuwekeza ni Afya, Kilimo, Makazi na Uzalishaji wa Viwanda. Sekta hizo zimepewa sehemu kubwa ya mgawo wa bajeti.
Sekta ya Uzalishaji imepewa mgawo wa dola bilioni 12, sawa na Sh trilioni 27.6 za Tanzania kwa nia ya kupanua viwanda vya kuzalisha na kutengeneza bidhaa akilenga kuongeza ajira.
Sekta ya Nyumba imepokea bilioni 1, sawa na Sh trilioni 2.3 za Tanzania, itakayotolewa kama mikopo kwa Wakenya kuwawezesha kujenga.
Sekta ya Afya imepata mgawo wa dola milioni 800, sawa na Sh trillion 1.84 za Tanzania zitakazotumika kuwaajiri madakatari na wauguzi. Pia sehemu ya fedha hizo itatumika kununua vifaa tiba.
Sekta ya Kilimo ambayo inasadikiwa kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Kenya nayo imepokea dola milioni 550, sawa na Sh trilioni 1.265 za Tanzania.
Fedha hizi zitatoka wapi?
Waziri wa Fedha Rotich amesema watakusanya kodi dola bilioni 21, sawa na Sh trilioni 48.3, huku pengo linalobakia likitegemea mikopo kutoka nje na ndani ya nchi.
Katika kutanua wigo wa kodi, Waziri Rotich ameongeza biashara ambazo hazikuwa zinatozwa ushuru awali.
“‘Katika miaka iliyopita huku uchumi ukikua, kumekuwa na ongezeko la huduma zinazotolewa na biashara ingawa baadhi ya biashara hizo hazikuwa chini ya sheria inayoshurutisha kulipa ushuru,” amesema Rotich.
“Bwana Spika, biashara zinazotoa huduma za usalama, usafi, upishi nje ya hoteli na migahawa, usafirishaji wa bidhaa na mauzo [naomba nazo sasa zianze kutozwa kodi],” amesema.
Waendeshaji wa biashara ya kamari sasa watatozwa 10% ya fedha zote wanazokusanya.
Pombe na sigara pia zimeongezewa ushuru wa ziada, huku wandesha pikipiki maarufu ‘Bodaboda’ nao kuanzia sasa watalazimika kuchukua bima itakayowakinga wao na abiria dhidi ya ajali nyingi zinazoshuhudiwa.
Kenya ina deni la taifa linalofikia dola bilioni 54, sawa na Sh trilioni 124.2 za Tanzania na mikopo ya mwaka huu itaongeza deni hilo hadi dola bilioni 60, sawa na Sh trilioni 138 za Tanzania.
Kuna hofu iwapo miradi inayofadhiliwa na bajeti hiyo ina uwezo wa kuleta faida ya kulipa deni hilo. Wadadisi wa uchumi tayari wameonya kuwa hilo haliwezekani.
Nchini Uganda
Bajeti ya Uganda ilipitishwa mwezi Mei, lakini kwa ujumla Waziri wa Fedha wa Uganda, Matius Kassaja, ameangazia zaidi masuala ya ujenzi wa viwanda na amesema bajeti ya mwaka wa fedha wa 2019/2020 inalenga hatua zinazokusudia kuongeza utajiri na ustawi wa Waganda wote.
“Maudhui ya mwaka huu yanaendelea kuwa ujenzi wa viwanda kwa kubuni kazi na ustawi wa watu wote,” amesema Kassaja.
Pia ameongezea kuwa biashara baina ya Uganda na nchi za Afrika Mashariki imeongezeka hadi 59% ya bidhaa zote zilizosafirishwa mwaka 2018.
Amesema katika kipindi hicho soko la Afrika Mashariki liliendelea kuwa kubwa zaidi kwa bidhaa za Uganda huku kipato cha Uganda kwa bidhaa zinazopelekwa Afrika Mashariki kikifikia dola milioni 469, sawa na Sh trilioni 1.07.