Mwekezaji wa kampuni ya utafutaji wa mafuta na gesi kwenye miamba iliyopo chini ya maji katika eneo la kusini mwa Ziwa Tanganyika, amezua tafrani kwa kuwalazimisha wafanyakazi kuchanja dhidi ya magonjwa ya tumbo (typhoid).
Kampuni hiyo ya Beach Petroleum inayomilikiwa na mwekezaji kutoka Australia, Novemba mwaka jana ilitoa chanjo ya typhoid kwa wafanyakazi wake waliopo mikoa ya Rukwa na Kigoma.
Vyanzo vya habari kutoka ndani ya kampuni hiyo vimeidokeza JAMHURI kuwa uongozi wa kampuni ya Beach Petroleum uliwalazimisha wafanyakazi wake kupatiwa chanjo hiyo na atakayekataa angefutwa kazi.
Imeelezwa kuwa Meneja wa Usalama na Mazingira kazini anayefahamika kwa jina moja la Colin, alitoa taarifa kwa wasaidizi wake Oktoba 20, 2014 wangepokea chanjo kwa ajili ya wafanyakazi. Ilisafirishwa kwa boti.
Novemba 18, 2014 mchana, James na mkewe Katherine Ann (raia wa kigeni) wakitokea Kipiri mkoani Rukwa na kufika Katavi, Wilaya ya Mpanda katika Kijiji cha Kalema na kuanza kutoa chanjo kwa wafanyakazi 39 wa Kampuni ya BGP ya Wachina.
Novemba 19, 2014 asubuhi chanjo hiyo iliendelea kutolewa kwa wafanyakazi na walinzi wa kampuni hiyo, ambao ni waajiriwa wa kampuni ya VRM. Wafanyakazi 37 walipatiwa chanjo hiyo.
Baada ya kutolewa kwa chanjo hiyo kwa wafanyakazi waliokuwa eneo hilo, James na Katherine Ann waliondoka na kuacha baadhi ya chanjo zikihifadhiwa kwa ajili ya kutolewa kwa wafanyakazi ambao hawajapatiwa chanjo hiyo.
Vyanzo vya habari vilieleza kuwa kutokana na onyo hilo lililotolewa na uongozi wa kampuni hiyo, wafanyakazi hao walilazimika kupatiwa chanjo hizo bila hiyari yao kwani awali walionywa endapo wangekataa.
“Idadi ya wafanyakazi waliopatiwa chanjo ni 101, na wafanyakazi tuliambiwa iwapo hatutokuwa tayari kupatiwa chanjo hiyo hatuna ajira, ukizingatia ajira ni ngumu tulilazimika kukubali kupatiwa chanjo hiyo. Ila wapo baadhi ya wafanyakazi wenzetu wameathirika lakini hakuna anayejali ingawa wameanza kupatiwa matibabu,” vinaeleza vyanzo vyetu.
Katika nyaraka ambazo JAMHURI imeziona, Beach Petroleum walinunua dawa aina ya Typhoid Vaccine Ad Single Dose (TYPHIM) 200 ambazo zilikuwa na thamani ya kiasi cha Sh milioni 8 kutoka Duka la Dawa la JD lililopo Dar es Salaam.
Stakabadhi ya uthibitisho wa upokeaji (delivery note) ya Novemba 5, 2014 kumbukumbu Na. 901087 inabainisha kupokewa kwa chanjo hizo na kampuni ya Beach Petroleum (T)Ltd Novemba 6, 2014.
Kadhalika, nyaraka ya malipo ya chanjo hizo yenye hati ya malipo Na. 90187 ya Novemba 6, 2014 inabainisha malipo hayo kulipwa na Beach Petroleum (T) Ltd TT 061114 inayobainisha kufanyika kwa malipo ya chanjo hizo.
JAMHURI ilifika Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kupata ufafanuzi kuhusiana na chanjo hiyo, ambako Mkurugenzi Msaidizi Kitengo cha Magonjwa ya Kuambukiza, Dk. Janeth Mgamba, alipohojiwa alionesha kushangazwa.
Dk. Mgamba anasema kuwa chanjo hiyo haipo kwenye mpango wa Taifa, hivyo utoaji wa chanjo hiyo si sahihi na wizara haina taarifa zozote kuhusiana na utoaji wa chanjo uliofanywa na kampuni hiyo ya kigeni.
Anasema kuwa katika sheria za kutoa chanjo hakuna mtu anayelazimishwa kupatiwa chanjo kama kampuni hiyo ilivyofanya kwa wafanyakazi wake. Pia utoaji wa chanjo hiyo haukufuata sheria na taratibu zilizowekwa na Wizara ya Afya nchini. Anasema kuwa pia ni lazima kufanyika kwa kampeni ya chanjo husika, ikiwa ni pamoja na uhamasishaji kwa wale wote wanaotakiwa kupatiwa chanjo na si kuwashtukiza na kuwalazimisha kwa vitisho.
Akizungumzia utoaji wa chanjo hiyo, Meneja Mwakilishi wa Beach Petroleum, Marcus Jacob Mng’ong’o, anasema kuwa walitoa chanjo hiyo baada ya wafanyakazi wake wengi kuugua magonjwa ya matumbo.
Mng’ong’o anasema kwamba jambo hilo lina historia tangu kampuni hiyo ilipoanza kazi nchini mwaka 2010 katika Ziwa Tanganyika.
Anasema wakati wakifanya kazi katika meli ya Mwongozo wakiwa na wanajeshi wa JWTZ Kitengo cha Maji, kulitokea matatizo ya mmoja wa askari hao kuugua ugonjwa wa typhoid na kuhara, ambao uliwasumbua mno na kulazimu kusimamisha kazi kwa zaidi ya saa tano ili kutafuta njia ya kuokoa maisha ya askari huyo.
Anasema kuwa kampuni hiyo ilifanya utafiti wao wenyewe na kugundua Ikola, Kalema na Kipiri maji yake kuwa na matatizo pamoja na typhoid, hivyo walipanga kuwapatia wafanyakazi kinga.
Anaeleza kuwa walitoa chanjo kwa makundi matatu ambayo ni wafanyakazi wa meli ya Mwongozo, Kigoma waliofikia 60, Kambi ya Kipiri wafanyakazi 40 walipatiwa chanjo na Kalema wafanyakazi kati ya 120 na 140 pia walipatiwa chanjo hiyo. Anasema kuwa chanjo hiyo ilinunuliwa kutoka Duka la Dawa la JD la jijini Dar es Salaam baala ya kupata mwongozo kutoka Wizara ya Afya.
“Sisi tunaamini kuwa hii ni kinga kwa ajili ya wafanyakzai wetu, dawa hizi zinauzwa katika duka la dawa. Hatukuona haja ya kutoa taarifa zozote kwa Wizara ya Afya na hatukupewa wala kuomba kibali cha kutoa chanjo hiyo. Tumekuwa tukinunua dawa kutoka JD siku zote, lakini hatukuelekezwa kama kuna kibali cha Serikali kinachohitajika,” anasema Mng’ong’o, na kuongeza: “Hii chanjo imefanyika tangu mwaka jana mwezi wa 11 mpaka 12, lakini hili suala limeibuka sasa, nashangaa.”
Hata hivyo, meneja huyo anaeleza kuwa waliwaambia wafanyakazi wa kampuni hiyo kuwa watawapatia chanjo hiyo ili kuepuka kuugua mara kwa mara, na mfanyakazi yeyote ambaye hatokuwa tayari kupatiwa chanjo hiyo kampuni hiyo wasingefanya naye kazi.
Mng’ong’o anasema chanjo hiyo ilitolewa na mtaalamu na baadaye aliacha chanjo zilizobaki katika kliniki ya Kalema, ambazo zilikabidhiwa kwa muuguzi aliyekuwapo ili aweze kuendelea kutoa chanjo hiyo kwa wafanyakazi wengine ambao walikuwa hawajapatiwa.
“Dawa zilizonunuliwa zilikuwa pakiti 200 na zilipotumika zilibaki 10 tu ambazo zipo camp (kambini) huko Kalema. Tulipozinunua tulizisafirisha kwa ndege ya Shirika la Ndege la Auric Air mpaka Sumbawanga, wafanyakazi wa Beach walikuja kuzichukua na kuzisafirisha mpaka Kipiri kwa boti, kisha zilisafirishwa kwa njia ya maji mpaka Kalema,” anasema.
Anaeleza kuwa yeye binafsi haoni kama kampuni hiyo ilifanya kosa lolote katika utoaji wa chanjo hiyo kwa wafanyakazi wake, zaidi ya kuwasaidia ili wasikumbwe na maradhi.
“Kama hizi dawa zina tatizo kwanini Serikali iruhusu ziuzwe? Sidhani kama wauzaji wanakurupuka tu na kuanza kuziuza,” anasema Mng’ong’o.
Mwanasheria wa Beach Petroleum, Victoria Lyimo, wa Kampuni ya Sheria ya Velma Law, anasema kuwa yeye binafsi hajui lolote kuhusiana na kampuni hiyo kutoa chanjo kwa wafanyakazi wake.
Lyimo anasema kuwa pia hawezi kuzungumzia suala hilo maana mkataba wake na kampuni hiyo haumruhusu kuzungumzia masuala ya mteja wake bila makubadiliano yoyote.
Lyimo anasema yeye si msemaji wa kampuni, hivyo mwenye mamlaka ya kuzungumzia hilo ni Beach Petroleum wenyewe. Ofisa Habari wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), Gaudensia Simwanza, anasema kuwa dawa hiyo ya chanjo iliwahi kusajiliwa awali, lakini ilikoma miaka saba iliyopita.
Anasema kuwa uhalali wa mtoa chanjo hiyo kwa binadamu kama ni daktari halali na amesajiriwa na Wizara ya Afya siyo tatizo, ila kama mtoaji huyo hana vigezo vinavyohitajika ni tatizo maana anaweza kusababisha maafa.
Hata hivyo, anaeleza kuwa utoaji wowote wa chanjo una taratibu zake, hivyo ni lazima zifuatwe. Ni lazima kuwasiliana na TFDA kabla ya kutoa chanjo hizo ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kwa watu wanaotakiwa kupatiwa chanjo hiyo, kuhakikisha kuwa wana afya njema.
Mmoja wa madaktari katika Kitengo cha Chanjo cha Taifa (jina linahifadhiwa), anaeleza kuwa Tanzania iliacha kutoa chanjo hiyo tangu miaka ya 1980 na haitolewi kabisa hapa nchini, alishangazwa na utoaji wa chanjo hiyo kwa kampuni hiyo ya kigeni.