*Lissu: Kauli za akina Gwajima zilikuwapo miaka 100 iliyopita
*Adai ni upotoshaji wa sayansi ya tiba unaofunikwa na msalaba
*NIMR yasema majaribio ya chanjo yalianza kwa wanyama
NA WAANDISHI WETU
Siku chache baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kuzindua chanjo dhidi ya ugonjwa wa corona kwa yeye mwenyewe kuchanjwa, wataalamu wa afya wameanza kutoa elimu kwa umma.
Kwa upande mwingine, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameungana na Rais kuwaondoa hofu wananchi kuhusu chanjo ya ugonjwa huo ambao umetikisa dunia kwa miaka miwili sasa.
Lissu anapingana na kauli ya mwanasiasa na kiongozi wa dini, Josephat Gwajima, anayewataka waumini wa madhehebu yake wasichanjwe, akitanabaisha madhara kadha wa kadha, akisema yanasababishwa na chanjo hiyo.
Lissu anasema: “Hii si mara ya kwanza watu kuhoji ‘efficacy’ (ufanisi) ya chanjo duniani. Hali kama hii ya akina Gwajima imewahi kujitokeza miaka 100 iliyopita.
“Wataalamu wa magonjwa ya milipuko wanasema mwaka 1918 hadi 1920 kulizuka ugonjwa wa mafua unaofahamika kama ‘Spanish Flu’.
“Upotoshaji wa watu kama akina Gwajima ukaanza. Kwa maneno kama haya haya! Kwamba ukichanjwa hauzai, unakuwa hivi – unakuwa vile!
“Hali hiyo imejirudia kwa kila chanjo. Wanapinga tu! Iwe ya polio, TB, tetekuwanga, homa ya manjano; lakini ‘humanity’ (ubinadamu) haijaharibika kwa miaka yote hii.
“Hizi ni propaganda na upotoshaji wa sayansi ya medicine (tiba) unaofanywa kwa kujificha kwenye nguo za kanisa; unafunikwa na msalaba.
“Sasa nini kifanyike. Tumpuuze aendelee na upotoshaji wake? Kauli hizi zimethibitika kwamba hazina ukweli wowote. Maisha ni mali yako. Si mali ya Samia, si mali ya Lissu wala ya Gwajima au Freeman Mbowe.
“Sasa tumuamini nani, watu wanaohubiri ‘apocalypse’ (elimu ya ufunuo wa mwisho wa dunia) au wanasayansi? Mimi ninawaamini wanasayansi.”
Mtaalamu wa afya kutoka Kituo cha Utafiti wa Magonjwa ya Milipuko cha OR Tambo, Profesa Gerald Misinzo, anawaondoa wananchi hofu iliyojengeka kuhusu upatikanaji wa haraka wa chanjo ya corona.
Profesa Misinzo anasema sababu ya kupatikana chanjo haraka ni kuwapo kwa utafiti wa awali wa virusi vya SARS vilivyotokea miaka kadhaa nyuma, akisema vina tabia kama ya virusi vya corona.
Anatoa sababu nyingine kuwa ni kukua kwa teknolojia duniani na kwamba kama isingekuwapo utaratibu wa chanjo kujaribiwa kwa wanyama, basi chanjo ya corona ingepatikana mapema zaidi.
“Lengo la kirusi si kumwangamiza binadamu, bali kuishi katika mwili wake. Lengo la chanjo ni kupambana na kirusi. Kirusi cha corona ni rahisi kudhibitiwa kwa sababu kina silaha moja tu; ‘protini mwiba’. Ndiyo maana tunashauri watu wachanje wapate ‘protini mwiba’ ya asili na ikitokea umepata maambukizi, hautapoteza maisha,” anasema Profesa Misinzo.
Mkurugenzi wa Kituo cha NIMR Mbeya, Dk. Nyanda Ntinginya, anasema chanjo ni mojawapo ya maendeleo makubwa katika ugunduzi wa kisayansi na muhimu sana katika kupambana na magonjwa hatarishi yaliyosababisha madhara na vifo vingi duniani, kwani huufanya mwili kutengeneza kinga ya kupambana na ugonjwa lengwa.
“Faida kubwa kwa chanjo kwa binadamu ni kupunguza wagonjwa wanaohitaji kulazwa hospitalini na vifo vitokanavyo na ugonjwa,” anasema Dk. Nyanda.
Anasema chanjo dhidi ya corona imeonyesha ufanisi katika kupambana na ugonjwa mkali, kulazwa na hata katika mazingira ya virusi anuai (variants) vya COVID-19.
Tangu kuanza kwa afua ya chanjo ya kupambana na COVID-19 kuna faida mbalimbali katika nchi zinazoitumia pamoja na ufanisi wa kudhibiti maambukizi ya COVID-19 kwa kupunguza makali ya ugonjwa.
“Utafiti na udhibiti wa chanjo katika maabara kabla ya kwenda kwa binadamu (research & development, pre-clinical) ni hatua muhimu.
“Kabla ya chanjo kutumika kwa binadamu hujaribiwa kwa wanyama. Si chanjo zote hufanikiwa kupita hatua hii. Zinazoonekana kutoleta kinga iliyokusudiwa au si salama kwa wanyama, haziendelei tena,” anasema Dk. Nyanda.
Dk. Nyanda anazitaja hatua zinazofuata kuwa ni Awamu ya kwanza; kuchanjwa binadamu wachache (makumi) ili kubaini usalama, kutambua dozi inayohitajika na kubaini madhara yatakayojitokeza kwa kutumia chanjo husika.
Awamu ya pili ni chanjo kwa mamia ya watu ili kuendelea kuangalia usalama wa chanjo na kuanza kuangalia ufanisi wake.
Awamu ya tatu ni kuchanjwa maelfu au makumi elfu ya binadamu kuthibitisha ufanisi wa chanjo na kuendelea kuchunguza ikiwa kuna madhara nadra ambayo yanaweza kuonekana.
Awamu ya nne ambayo ni chanjo chache huifikia, huwa ni baada ya chanjo kuthibitishwa kuwa salama na kuwa na ufanisi.
“Kwenye hatua hii, chanjo hupitiwa na mamlaka ya dawa nchini na kupewa usajili kutumika kwa jamii inayohitaji chanjo hiyo.
“Hii huendelea kufuatiliwa katika hatua endelevu kubaini madhara ya muda mrefu yanayoweza kutokea baada ya kutumika kwa jamii.
“Kupitia taratibu zinazowekwa na Mamlaka za Udhibiti wa Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) na ZFDA pamoja na chanjo za ndani.
“Muda unaotumika kupitia hatua hizi mbalimbali hutofautiana kulingana na aina ya chanjo, maendeleo ya teknolojia, ushirikiano na udharura wa matumizi ya chanjo inayokusudiwa; mathalani wakati wa janga, upatikanaji wa rasilimali na miundombinu,” anasema Dk. Nyanda.
Anasema chanjo ya corona si ya kwanza kutumika ndani ya muda mfupi, kwa kuwa moja ya chanjo ya ugonjwa wa mafua makali ya H1N1 ilianza kutumika miezi sita tu baada ya janga hilo kuanza mwaka 2009.
Shirika la Afya Duniani (WHO) lina utaratibu wa kuorodhesha chanjo, dawa na vitendanishi ambavyo havijaidhinishwa kwa matumizi ya kawaida kutumika katika mazingira ya dharura, ambapo kupitia utaratibu huu tathmini ya kina hufanyika kuhusu faida na athari ya matumizi ya dawa.
“Kamati huru ya kitaifa ya ushauri wa masuala ya chanjo (National Immunization Technical Advisory Group, NITAG) ina mamlaka ya kufuatilia madhara ya chanjo hizi kadiri zinavyotumika katika jamii kubwa.
“Kufuatilia pia idadi ya washiriki katika tafiti mbalimbali za chanjo ya COVID-19 zilizofanyika duniani kabla hazijaanza kutumika kwa jamii kubwa,” anasema.
Anasema tangu kuanza kutumika kwa chanjo mbalimbali za corona Desemba 2020:
“Hadi kufikia mwishoni mwa Machi 2021, vifo takriban 10,400 vimezuiwa, kupunguza kulazwa wagonjwa takriban 52,000.”
Dk. Nyanda anasema kama ilivyo kwa dawa nyingine, chanjo zinaweza kuwa na madhara madogomadogo kwa baadhi ya watu.
Anasema mpaka sasa chanjo za COVID-19 zimefanyiwa tathmini ya usalama kupitia tafiti zilizohusisha maelfu ya washiriki duniani na kukubalika kuwa zina faida kubwa.
Tanzania inatumia chanjo aina tisa tofauti dhidi ya magonjwa 13 yanayozuilika.
Moshi bado hali ni tata
Kutoka Moshi tunataarifiwa kwamba mkakati wa serikali kukabiliana na wimbi la tatu la maambukizi ya virusi vya corona umo shakani mjini humo kutokana na baadhi ya maeneo kuwa na mikusanyiko mingi ya watu, hasa maeneo ya starehe pamoja na kwenye masoko, ambako watu wengi wamekuwa hawachukui tahadhari ikiwano kuvaa barakoa.
Moshi na Arusha ni miongoni mwa miji inayotikiswa na ugonjwa wa corona nchini, kukiripotiwa kujaa kwa vyumba vya kuhifadhi maiti katika hospitali zote; za umma na binafsi.
Katika kumbi za starehe wamiliki wengi wanashindana kuvutia wateja, ikiwamo kukodi bendi za muziki kutoka Dar es Salaam kutoa burudani hasa siku za mwisho wa wiki.
JAMHURI imetembelea baadhi ya kumbi hizo na kushuhudia idadi kubwa ya watu kinyume cha maelekezo ya serikali iliyopiga marufuku mikusanyiko isiyo ya lazima.
Hata kwenye masoko, watu hawachukui tahadhari yoyote.
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Steven Kigaigai, anasema msimamo wa serikali kutoruhusu mikusanyiko isiyokuwa ya lazima upo palepale katika maeneo yote ya mkoa huo.
Katika masoko matatu ya mjini Moshi; Mbuyuni, Soko la Kati na Soko la Kiusa maarufu Soko la Juu; JAMHURI limeshuhudia watu wengi wakiingia na kutoka bila kuvaa barakoa, ingawa wachuuzi wengi wanavaa hasa masoko ya Mbuyuni na Manyema.
Kuhusu kasi ya maambukizi ya virusi hivyo mjini Moshi, Kigaigai anasema hali si kama inavyoelezwa na watu wengi, ikiwamo mitandao ya kijamii.
“Idadi ya wagonjwa wa corona si kubwa kama ambavyo watu wengi wamekuwa wakieneza katika mitandao ya kijamii,” anasema RC Kigaigai.
Mmoja wa watu waliozugumza na JAMHURI na kuomba hifadhi ya jina lake ni mkazi wa Machame Mashariki, wilayani Hai, anasema hivi karibuni familia mbili katika eneo hilo zimewapoteza baba na mama.
“Baadhi ya watoto katika moja ya familia hizo wapo katika matibabu Hospitali ya Nkwarungo, Machame. Hali ni mbaya,” anasema mwananchi huyo akipingana na kauli ya Kigaigai.
Kwa mujibu wa Kigaigai, hata hospitali kubwa za KCMC na Mawenzi, idadi ya wagonjwa si kubwa, akiwataka wananchi kupuuza taarifa za mitandaoni na kuwataka waandishi wa habari kutumia vizuri kalamu katika kuhabarisha jamii.
“Taarifa nilizonazo si za kutisha sana kama tunavyosikia. Ni kweli wagonjwa wapo, lakini si kwa kiwango hicho! Hata leo nimezungumza na Mkurugenzi wa KCMC, Dk. Gilliad Masenga. Hali si mbaya. Kwa hiyo ni muhimu mitandao ya kijamii ikajiepusha na taarifa za upotoshaji,” anasisitiza RC.
Hata hivyo, Kigaigai alipatwa na kigugumizi kuzungumzia mikusanyiko katika kumbi za starehe na hatua ambazo serikali inachukua.
Anasema wanaomiliki kumbi hizo wana leseni za kuendesha biashara, hivyo serikali lazima itumie busara kuchukua hatua badala ya kutumia nguvu, kwani hawatapata suluhu sahihi.
Arusha wamulika daladala
Kutoka Arusha, mji mwingine unaodaiwa kulemewa ugonjwa wa corona, tunataarifiwa kwamba Kamanda wa Polisi wa Mkoa (RPC) Justin Masejo, amemwagiza Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani (TRO), Solomon Mwangamilo, kuhakikisha makondakta wa mabasi ya abiria wanakuwa na vitakasa mikono na barakoa ili kujikinga dhidi ya corona.
Akizungumza na JAMHURI, Mwangamilo anasema kutokana na hatari ya corona, magari yote yatatakiwa kubeba abiria waliokaa kwenye viti (level seat), akipiga marufuku kujaza abiria.
“Wananchi nao wanapaswa kufahamu kuwa kuingia kwenye gari ambalo limejaa ni hatari kwa maisha yao na maisha ya wengine,” anasema.
Anashangaa kuwaona watu ‘wakijiondoa ufahamu’ ilhali karibu kila familia inafahamu madhara ya corona.
“Askari wa usalama barabarani tuko wachache, hatuwezi kumlinda kila mtu. Tunaomba wananchi nao wakatae uvunjifu wa sheria ama kwa kutoa taarifa polisi au kuikemea tabia hiyo,” anasema Mwangamilo.
Anasema kwa maelekezo ya RPC, kuanzia sasa wasafiri wanatakiwa kutopanda basi ambalo limejaa na wakikutwa, watashushwa na mwenye gari atapigwa faini.
“Na magari yote. Iwe linakwenda Kwa Morombo, Tengeru, Maji ya Chai au Ngaramtoni,” anasema.
JAMHURI limetaka kufahamu hali ya corona ilivyo mkoani Arusha, lakini juhudi zetu zimekwamishwa na Mganga Mkuu wa Mkoa (RMO), akidai kuwa taarifa hizo hutolewa na Mkuu wa Mkoa pekee.
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, John Mongella, alipoulizwa na Mwandishi Wetu kwa njia ya simu, alimwelekeza kurudi kwa RMO.
Alipoambiwa kwamba RMO anataka ruhusa kutoka kwake ndipo azungumze na mwandishi wa JAMHURI, akajibu: “Nenda, waambie wanipigie ili niwaelekeze kuwa nimekuruhusu wakupe taarifa.”
Mwandishi aliporudi Hospitali ya Mount Meru kupeleka ujumbe huo alikwama baada ya maofisa wa hospitali kumwambia kwamba wanataka maandishi kutoka kwa mkuu wa mkoa.
Habari hii imeandaliwa na Aziza Nangwa (Dar es Salaam), Charles Ndagula (Moshi) na Hyasinti Mchau (Arusha).