Julai 28, mwaka huu Rais Samia Suluhu Hassan amezindua chanjo ya Covid-19 (corona). Katika uzinduzi huo uliofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Samia, amechanjwa chanjo ya Johnson & Johnson inayotolewa kwa dozi moja ili kujikinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa corona.

Pamoja na mambo mengine, Samia, amesema amechanja chanjo hiyo kwa hiari yake mwenyewe baada ya wanasayansi kujiridhisha kuwa ni salama na amesisitiza kuwa asingejipeleka mwenyewe kwenye kifo licha ya kuwa na majukumu mengi katika nchi.

Pia amesema chanjo ni hiari na kwa wale wenye imani potofu wataendelea kuwapa elimu na watahakikisha inapatikana kwa wote walio tayari kuchanja.

Baada ya Samia kuchanjwa, wiki iliyopita Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ikatoa ratiba ya usambazaji wa chanjo katika maeneo mbalimbali ya Tanzania Bara huku viongozi mbalimbali wa serikali na kidini wakiwa wa kwanza ili kuhamasisha watu wengine wanaotaka kuchanjwa kwa hiari.

Gazeti la JAMHURI lilipita maeneo mbalimbali na kushuhudia misururu ya maelfu ya Watanzania wa jinsia, rangi, dini, kabila na rika mbalimbali wakiitikia wito wa kuchanjwa chanjo hiyo kwa hiari.

Sisi tunawapongeza wote walioitikia wito wa kujitokeza kwa wingi kuchanja katika maeneo mbalimbali hapa nchini na huo ni ushahidi wa dhati kwamba wanajali afya zao na wamekataa kuwasikiliza wale wapotoshaji wanaoendelea kuwatisha wenzao kuhusu chanjo hiyo.

Kimsingi, tunawapongeza kwa sababu nasi tunapingana na wale wanaopotosha ukweli kuhusu chanjo hiyo ambayo imethibitishwa na wanasayansi pamoja na Shirika la Afya Duniani (WHO) kwamba ni salama na ina ufanisi wa kuweza kuzuia watu kuugua sana na kulazwa hospitalini.

Licha ya kwamba chanjo ni hiari, tunaamini ni muhimu mno kwa sababu kwa taarifa zilizopo kama zilivyotolewa na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) inaonekana chanjo nyingi huleta kinga ya kutosha dhidi ya aina za virusi vilivyoko, hasa katika kupunguza makali ya ugonjwa, kulazwa hospitalini na vifo, ingawa zinaweza kusababisha athari chache, za  muda  mfupi,  kama  vile  homa  ya  kiwango  cha  chini,  maumivu  au  ngozi  kuwa nyekundu eneo palipochomwa sindano. 

Kwa mujibu wa TMDA, athari hizo ni za kawaida na huisha baada ya siku chache huku madhara makubwa au  ya kudumu  ya  chanjo  yanawezekana  lakini  ni nadra kutokea na hadi sasa tangu watu waanze kuchanjwa madhara  yaliyoripotiwa  ni  ya  wastani  na  yanajumuisha  homa,  uchovu, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, baridi, kuhara na maumivu sehemu palipodungwa sindano, huku yakitajwa kuwa yanatibika kwa kupumzika, kunywa maji mengi na kutumia dawa za kuzuia maumivu.

Pamoja na kwamba chanjo zimekuja kusaidia katika mapambano dhidi ya corona, lakini tunawaomba wote waliochanjwa kuendelea kuvaa barakoa, kunawa mikono mara kwa mara kwa maji tiririka, kukaa eneo lenye hewa nzuri, kuzingatia umbali na kujiepusha na mikusanyiko. 

Kwa kuwa katika awamu hii watu wengi waliochanjwa kwa hiari ni wale walio katika makundi maalumu ambayo yako hatarini yakijumuisha wazee walio na umri wa zaidi ya miaka 50, watumishi wa kada ya afya na wale wenye magonjwa sugu, pia tunawaomba wajitokeze kwa wingi wakachanje kwa hiari pindi awamu ya pili ya chanjo hizo zitakapoanza kutolewa tena na serikali.