Pamoja na Serikali kuonesha nia njema ya kutaka kurudisha huduma za usafiri majini katika maziwa makuu, kwa kutumia vyombo vya umma yaani kuifufua Marine Services Company Limited (MSCL), tatizo bado lipo.
Serikali inategemea kutoa fedha kwa ajili ya kufufua meli mbili katika Ziwa Victoria na kufanya matengenezo makubwa kwa meli moja katika Ziwa Tanganyika.
Serikali inatarajia kutoa Sh bilioni 50.5 kwa MSCL iweze kufufua meli zake na hivyo kuwa na usafiri wa uhakika katika utoaji wa huduma za usafirishaji wa abiria na mizigo kwa maziwa makuu. Meli zinazotarajiwa kufufuliwa ni mv Victoria na mv Butiama zinazofanya safari katika Ziwa Victoria na mv Liemba inayofanya safari katika Ziwa Tanganyika.
Azma hii ya Serikali huenda ikakamilika katika mwaka huu wa fedha wa 2016/2017. Tunasema kuwa huenda azma hii ikakamilika kwa sababu katika miaka iliyopita Serikali katika bajeti zake imekuwa ikitoa taarifa za kutenga fedha kwa ajili ya MSCL, lakini taarifa hizo zimekuwa zikiishia kuwa ni ‘ahadi hewa’ kwani fedha hizo ama zimekuwa haziletwi kabisa, au zinaletwa kiasi kidogo kisichokidhi mahitaji yaliyoombewa fedha hizo.
Mfano mzuri ni katika bajeti ya mwaka wa fedha 2015/2016, Serikali iliahidi kuipa MSCL kiasi cha Sh bilioni 8.5 zitumike kufanya matengenezo makubwa kama ifuatavyo:
1. Kwenye Ziwa Victoria – meli zilizopaswa kufanyiwa matengenezo ni mv Victoria, Butiama na Clarias.
2. Kwenye Ziwa Tanganyika – meli zilizokuwa kwenye ratiba ya bajeti hiyo zilikuwa ni mv Liemba na mt Sangara; na
3. Kwenye Ziwa Nyasa, mv Songea ilikuwa ifanyiwe matengenezo makubwa.
Badala yake, Serikali ilitoa bilioni 1.8 kwa lengo la kuifanyia matengenezo mv Victoria na kulipa madeni kwa mgawanyo huu: kiasi cha Sh milioni 600 kililetwa kwa ajili ya matengenezo ya mv Victoria na bilioni 1.2 zililetwa kwa ajili ya kulipa madeni ya mafuta, bima na vipuri. Kilichotokea ni kuwa mv Victoria haikutengenezwa, wajanja wachache wakafanya mambo yao.
Uchunguzi unaonesha kuwa ujanja huo ulipobainika, wachache wakawajibishwa na wengine wakabaki huku wakipandishwa vyeo na sasa meli hiyo ipo katika Bandari ya Mwanza South, ikiendelea kuchakaa. Wakati mv Victoria ni mbovu na haifanyi kazi, wajanja wengine wakailipia bima kinyume na maelekezo ya bodi (bodi ilikuwa imetoa maelekezo ya kulipia bima meli zinazofanya kazi tu).
Meli ikalipiwa bima kwa kiasi kikubwa kuliko ilivyokuwa ikilipiwa wakati inafanya kazi. Ndiyo kusema kwamba thamani ya meli iliongezeka na hivyo bima yake nayo ikaongezeka. Haya yakifanyika Bodi ya Kampuni imekaa kimya na kadhalika mkurugenzi anayesimamia kampuni amenyamaza kimya na hao wajanja wanaendelea kutukuzwa.
Kilio cha wafanyakazi kwa Serikali ni juu ya ombwe linaloendelea. Mwezi wa sita huu sasa wafanyakazi hawajapata mishahara na jedwali la bajeti katika mwaka huu wa fedha linaonesha kuwa hakuna fungu la mishahara kwa wafanyakazi kwa maelezo kuwa hesabu za kampuni hazijakaguliwa tangu mwaka 1999!
Hili ni jambo la kushangaza kwani miaka yote wafanyakazi wamekuwa wakiona wakaguzi. Wakaguzi hao huja wakakaa wiki au zaidi ya wiki wakikagua vitabu vya hesabu katika vituo vyote vya kampuni. Tunashangaa kuambiwa kuwa hesabu za kampuni hazijakaguliwa kwa miaka yote hii, ni aina gani ya ukaguzi ambao umekuwa unafanywa na wakaguzi hao?
Au ndiyo kusema kuwa huo ulikuwa ni ‘ukaguzi hewa’ na hao walikuwa ni ‘wakaguzi hewa’ na hivyo malipo waliyokuwa wanalipwa wakaguzi hao nayo yalikuwa ni ‘malipo hewa’? Wafanyakazi wameletewa kitendawili cha kusikitisha sana.
Tangu mwaka 1999 kampuni ilipoanzishwa, pamepita Bodi mbili za Wakurugenzi na hii iliyopo kwa sasa ni Bodi ya tatu, Mkurugenzi anayeisimamia kampuni hii amekuwa ni yuleyule miaka yote hii. Nini siri ya kampuni kutokukaguliwa miaka yote hii, ina maana kuwa bodi zote zimekuwa haziyafahamu matatizo ya kampuni kutokukaguliwa?
Huyo mkurugenzi ambaye amekuwa anaisimamia kampuni kwa muda wote amekuwa halifahamu hili? Au ndiyo kusema kuwa bodi, mkurugenzi na wateule wao katika menejimenti wapo kuangalia maslahi yao binafsi na si kuangalia ufanisi wa huduma zitolewazo na kampuni na pia kusimamia na kuhakikisha kuwa kampuni inaendeshwa kwa kufuata taratibu, kanuni na sheria za nchi katika taasisi za umma?
Yapo mambo mengi kwa namna kampuni hii inavyoendeshwa. Usiri mkubwa umetawala. Siri hizo zinajulikana kwa mkurugenzi (anayeisimamia MSCL), Bodi ya Kampuni na Menejimenti ya Kampuni. Ndiyo maana viongozi wa kampuni wanakuwa na ujasiri wa kusema kuwa fedha za kampuni ni siri ya menejimenti!
Maslahi binafsi yamewekwa mbele, wakati sheria haziruhusu mfanyakazi au kiongozi wa kampuni kufanya biashara na kampuni, kwa MSCL ni tofauti kabisa. Watu wanafanya biashara na kampuni kwa wazi na kwa siri kwa kutumia migongo ya ‘kampuni hewa’, mfano ni katika biashara za kampuni zinazo-supply mafuta kwenye meli na bima.
Kampuni haina njozi na hivyo hakuna dira katika shughuli za kampuni, watu wanapewa vyeo wafanye mazoezi ya kuongoza katika Idara nyeti kinyume na miongozo ya sheria za watumishi wa umma.
Kama Serikali italeta fedha kama ilivyoahidi kwa ajili ya matengenezo makubwa ya meli na malipo ya awali (awamu ya kwanza) ya ujenzi wa meli mpya, na menejimenti ikaendelea kuwa hii iliyopo kwa sasa, ni dhahiri kuwa matengenezo hayatafanyika kwa kiwango kinachokusudiwa.
Kuna mchwa wanaokula na kutafuna boti, na ndani ya menejimenti ya MSCL kuna daktari anayetafuta damu kwa wagonjwa waliolazwa katika wodi ya wagonjwa mahututi! Waliteuliwa kwa ujanjaujanja na wanaendesha mambo yao kwa ujanja vile vile, huku wanafanya jitihada kubwa kuwagawa wafanyakazi wafanikiwe kuendelea kubaki katika nafasi za uongozi.
Katika kufanikisha lengo la kuvunja umoja wa wafanyakazi, kuna tetesi kuwa menejimenti inakusudia kutoa likizo bila malipo kwa wafanyakazi, na wengine kuwapunguza kabisa. Lakini hilo ni siri, na chama cha wafanyakazi hakijashirikishwa mpaka sasa.
Wafanyakazi wanamwomba Katibu Mkuu wa Wizara aingilie suala hili kuhakikisha kuwa mpango huu ama unasitishwa, au kama utafanyika basi ufanyike kwa kufuata kanuni za utumishi wa umma na kuzingatia misingi ya haki kwa wafanyakazi.
Katika kipindi hiki ambapo wafanyakazi hawapati mishahara, wanakosa huduma za matibabu hospitalini na wanaostaafu wanasota kwa kutolipwa stahiki zao hata nauli tu ya kuwafikisha makwao, Serikali imekaa kimya.
Wenye dhamana ya kuongoza na kusimamia kampuni walipeleka serikalini mapendekezo ya bajeti ya matengenezo ya meli na mahitaji ya pesa za kuendesha ofisi tu. Ni ajabu kuwa kampuni haina orodha za watumishi wake – huwa haijulikani kuwa mfanyakazi atastaafu lini na aandaliwe nini kutokumwingiza mfanyakazi katika mateso.
Pia inaonekana kuwa hakuna mshauri mzuri wa masuala ya sheria kwa menejimenti, kwani kumuondoa mtu kazini usimlipe haki zake mara moja ni kuandaa bomu. Kampuni inajiingiza katika mazingira mabaya yanayoweza kusababisha ishtakiwe. Ipo mifano mingi ya uzembe wa jinsi hiyo huko nyuma na madhara yake yanajulikana.
Lipo hitaji kubwa la wafanyakazi (mabaharia) kusoma kozi ambayo ni ya lazima kwa mujibu wa mwongozo wa IMO (International Maritime Organization). Menejimenti ya MSCL haikuona umuhimu wa kuomba fungu kwa ajili ya kozi hii (Manila Convention 2010).
Kwa ajili ya usiri uliotanda katika uongozi wa kampuni hii, wafanyakazi wanashindwa kujua aliyeandaa bajeti hiyo na kuipeleka serikalini huku akiacha hitaji la muhimu kama hilo. Mwongozo wa IMO unawataka mabaharia wote kuwa wamesoma kozi hiyo kabla ya Desemba 31, 2016. Kwa maana hiyo Januari 1, 2017, baharia atakayekuwa hajasoma na kubadilisha cheti atakuwa anafanya kosa na kwa hiyo SUMATRA itapaswa kumzuia asifanye kazi kwenye meli.
Katibu Mkuu wa Uchukuzi, Dk. Leonard Chamuliho, alipozungumza na JAMHURI, alieleza kuwa Serikali imetenga Sh bilioni 50.5 kwa ajili ya matengenzo ya meli na malipo ya awali kwa ajili ya ujenzi wa meli mpya.
Ameongeza kuwa mishahara ya wafanyakazi itaombwa pale ukaguzi wa hesabu za kampuni ambazo hazijakaguliwa tangu mwaka 1999 utakapokamilika, ndipo atawasilisha serikalini maombi ya fedha za mishahara kwa wafanyakazi. Amesisitiza nia ya Serikali kuifufua kampuni hii na kuhakikisha huduma za meli zinarejeshwa.